Header Ads

WAMILIKI MTANDAO WA ZE UTAMU WASAKWE

Na Happiness Katabazi

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Chama cha Mapinduzi, karibu wakati wote imekuwa na kasumba ya kutotaka kupokea mawazo na changamoto zinazotolewa na wananchi wake, hata kama mawazo hayo yakifanyia kazi, yataleta tija kwa taifa.

Ni serikali hii kwa miaka kumi sasa, imekataa kabisa kufanyia kazi mawazo ya wasomi na wananchi wa kawaida waliokuwa wakiitaka kwamba, kabla haijakubali kujiingiza kwenye mfumo wa Utandawazi, kwanza ni lazima ihakikishe inaandaa wananchi wake kikamilifu kuingia kwenye mfumo huo.

Miongoni mwa viongozi waliokuwa wakishupalia taifa letu kuingia kwenye mfumo huo, ambao nadiriki kusema ni mzuri, ila haukustahili kuja kabla wananchi kuandaliwa.

Alikuwa, ni Rais mstaafu Benjamin Mkapa na vingozi wa serikali yake ya Awamu ya Tatu na wale chama chake cha CCM.

Naamini, wakati waking’ang’ania jambo hili kuingia nchini bila ya kuwaandaa wananchi kikamilifu kumudu mfumo huo, hawakujua kwamba ipo siku, kunaweza kusababisha kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili, viongozi na wananchi kudhalilishwa utu wao na pengine kuhatarisha usalama wa nchi. Hii inasikitisha mno.

Lakini, Watanzania tukumbuke wakati serikali imeridhia kwenye mfumo huo wa utandawazi, lakini mwaka juzi wakati Dk.Willbroad Slaa alipowasilisha hoja bila mafanikio ya kutaka kuwataja mafisadi uliofanyika katika Benki Kuu ya Tanzania.

Serikali kwa upande wake, ilisimama kifua mbele na kusema kuwa kamwe haifanyiikazi taarifa zinazopatikana katika mtandao.

Baada ya kuona Dk. Slaa amakomalia hoja hiyo na kuamua kwenda kuimwaga pale viwanja vya Mwembe Yanga-Temeke na moto kusambaa nchi nzima na hatimaye serikali ikaunda tume kuchunguza ubadhilifu nayo ikagundua na kisha leo hii tunaona baadhi ya wahusika wa kashfa hiyo wamefikishwa mahakamani.

Sasa basi, wiki hii katika mtandao wa www.zeutamu.com mtandao ambao umejipambanua kwaajili ya kupachika picha za utupu za watu wa kada zote na wanaotembelea mtandao huo uchangia mawazo yanayohusu maisha binafsi ya faragha za watu, hakika hivi sasa umepata umaarufu kutokana watoto, hata watu wazima wenye heshima zao na baadhi ya viongozi kuutembela japo kwa kujificha.

Na wakati mtandao huo ukiendelea kujipambanua mamlaka husika zimekuwa zikiukenulia meno mtandao huu hadi wiki hii ulipotundika picha ya kumdhalilisha rais wetu, ndipo mtandao huo umedhibitiwa kwani hivi sasa hata ukiufungua aufunguki.

Mtandao huo wiki hii ulitundika picha chafu yenye sura ya Kikwete, ambayo picha hiyo inamdhalilisha rais wetu, sisi wananchi anaotuongoza na familia yake kwa ujumla.

Na tayari wataalamu wa masuala ya kompyuta wametanabaisha kuwa picha ile chafu ni ya kutengeneza.

Binafsi, nimekuwa ni miongoni mwa wananchi ambao tumekuwa tukitofautiana kimsimamo na rais na serikali yetu na tumekuwa tukipingana nao kwa kutoa maoni yetu kwa njia sahihi.

Na tumekuwa tukifanya hivyo lengo likiwa moja tu kuikumbusha serikali majukumu yake kwani kuna mambo mengine yanafanyika mitaani na serikali inakuwa haina habari.

Lakini, Watanzania tujiulize hadi kufikia hatua hii ya siyo rais peke yake anadhalilishwa kwenye mitandao huo na wananchi wengine wamekuwa wakidhalilishwa, mamlaka husika zinakuwa wapi ?

Kweli Idara yetu ya Usalama wa Taifa, Interpol na wale wataalamu wa masuala ya kompyuta ambao wamesomeshwa na kodi zetu wanashindwa kudhibiti mfumuko huu wa kutundika picha za utupu kwenye mitandao, halafu tunaendelea kuwacheka.

Aingii akilini kabisa Makachero wetu ambao wamesomea fani ya Sayansi ya Teknolojia wanashindwa kutambua mitandao ya aina hii inamilikiwa na wa kina nani je ni watanzania wenzetu au raia wa kigeni wameamua sasa kuanza kutufanyia chokochoko kuanza kudhalilisha viongozi wetu na wananchi wake au makachero wetu wanashindwa kutumia teknolojia kuidhibiti mitandao ya aina hii?

Katika hili la mfumuko wa mitandao inayotundika picha chafu niwe mkweli kwamba Njagu namba moja IGP-Said Mwema na Shushushu namba moja Othman Rashid mnatuangusha, lakini hamjachelewa bado mnayonafasi ya kuakikisha mnapambana na tatizo hili ama kwakushirikiana na wataalamu wa nchi marafiki wa taifa letu au kuwapeleka vijana wenu kusoma.

Tusinyoshee vidole tu mitandao hiyo,pia kuna baadhi ya magazeti na redio hivi sasa vimevuka mipaka na kuchapicha picha na kutangaza mambo yasiyofaha mbele ya jamii, na mamlaka husika wanafumbia macho.

Nasema kuna haja gani ya kuruhusu mfumo kuingia nchini wakati hatujaandaa watalaamu wakuweza kukabiliana na mfumo huo pindi unapotaka kuleta madhara kwa jamii yetu?

Kikwete siyo kiongozi mkuu wanchi peke yake ambaye amekumbwa na kadhia hiyo, hata Rais mstaafu Mkapa akiwa madarakani mwaka 2005, gazeti hili liliwahi kutoa picha ya kutengeneza ilichotwa kwenye mmoja wa mtandao ilikuwa ikimuonyesha Mkapa amekaa kizimbani na hakimu akimuuliza maneno haya.

“Mr. Mkapa, this is the 3rd time I see you in this court for the same crime, that is asking for loan and not repaying, You should be hanged to death.

Rais Mkapa kwa mujibu wa picha hicho iliyomwonyesha kaketi kizimbani, alimjibu hakimu huyo maneno yafuatayo: “Don’t you give discount to your Regular Clients?
Picha hii iliiponza gazeti hili la Tanzania Daima na kusababisha Idara ya Habari Maelezo, kulifunga kwa siku kadhaa.

Lakini yote hii inatokana mfumo wa mzima wa uongozi, jamii kukosa uzalendo, wameishiwa uwezo wa kufikiria na pia ile zana ya uwajibikaji wa pamoja hakuna tena.

Naamini kama serikali yetu ingekuwa ikiwajibika kwa pamoja na wakaondokana na makundi, visasi na uchumia tumbo mambo yangeenda vizuri na yote haya ingekuwa ni historia.

Leo hii kukaa na watoto au wazazi wako kusikiliza redio, kuangalia Tv imekuwa ni wasiwasi unakutana na matangazo ambayo unasikia na kuona aibu.

Hivyo, napenda kutoa pole kwa Rais Kikwete,na watanzania kwa ujumla kwani ni kiongozi wetu amedhalilishwa, lakini achukulie kitendo hicho kichafu ni changamoto vyombo vya ulinzi na usalama wa vya nchi.

Kwamba, viamke usingizini na viache ubinafsi wa kutumia ujuzi waliyoupata kwa manufaa yao badala ya taifa.

Hata kama kiongozi wetu ana udhaifu wake kiutendaji au ule wa kibinaadamu kwa mambo kadhaa yanayohusu taifa hili, hatupaswi kumdhalilisha kiasi hiki.

Kitu cha msingi ni kuendeleza utamaduni wetu wa kupingana kwa hoja na vielelezo na si vurugu na kutundikana picha za utupu kwenye mitandao.

Kama tutakataa kubadilika sisi wenyewe wananchi tukae tukijua tunaipeleka nchi yetu kuzimu kwasababu, watoto wa sasa wanatumia huduma ya kompyuta kwaajili ya kupataa taarifa mbalimbali za kimasomo au burudani lakini endapo tutaacha kutumia uhuru huu wa kuwa mtandao kujadili matatizo yanayoikabili tukajiingiza kwenye upuuzi huu niwazi hatufiki kokote.

Huru wa kujieleza ambao umeanishwa kwenye Katiba ya nchi yetu kila mtanzania kwa nafasi yake autumie vizuri na si vinginevyo kwani hakuna uhuru usiyo na mipaka.

Wakati tujadili hayo yote, tujiulize je yale madhambi yaliyokuwa yakifanywa na kundi la wanamtandao katika mchakato wa kutafuta mgombea urais mwaka 2005,dhambi ya kupakana matope, kuzuliana kashfa miongoni mwa wagombea, kumuundia Dk.Salim Ahmed Salim picha iliyokuwa ikionyesha yeye aliwahi kuwa mwanachama wa Hizbu,Je ndiyo zimeanza kumtafuna rais wetu?

Mungu Ibariki Tanzania Mungu Ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, April 26, 2009

No comments:

Powered by Blogger.