Header Ads

TANGULIA MEJA LUHWAGO,TUKO NYUMA YAKO


Na Happiness Katabazi

JUZI (Aprili mosi 2009) saa 1:15 asuhubi nikiwa katika ofisi Wakili wa Kujitegemea Alex Mgongolwa iliyopo jengo la Life House Dar es Salaam,kikazi nilipokea ujumbe mfupi kutoka kwa rafiki yangu ambaye ni Ofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi(jina kapuni) akiniarifu kuwa Meja William Luhwago amefariki ghafla usiku wa kumkia siku hiyo.

Kwa kweli sikuweza kuuamini moja kwa moja ule ujumbe mfupi ulioingia katika simu yangu ila nikamjibu Ofisa huyo kuwa mimi siyo mjinga hivyo asinidanganye kwakuwa siku hiyo ilikuwa ni siku ya wajinga duniani.

Na Mgongolwa akaniambia huyo anakudanganya kwani siku hiyo ni siku ya wajinga na kunitaka nisishtuke.

Lakini Ofisa huyo akanitumia tema ujumbe mfumbi yaani (sms) akisema hanitanii ni kweli na kunidhibitishia zaidi aliamua kunipigia simu na kunieleza kuwa Jumanne, usiku Luhwago akiwa nyumbani kwake aliugua ghafla wakampeleka Hospitali ya Tumaini iliyopo Upanga na ndipo alipofia pia akaniambia msiba upo nyumbani kwake Upanga Dar es Salaam.

Ghafla nikapigiwa simu na wanajeshi wengine watatu wakinitaarifu jambo hilo hilo na wakaniambia kuwa wataleta taarifa ya kifo na picha marehemu ofisini.

Hapo ndipo nilipoamini taarifa hizo nilizopewa na yule ofisa wa mwanzo.Na kwa kuwa nilishamalizana na Mgongolwa nilianza safari ya kuelekea eneo langu la kazi ambapo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,huku nikiwa nimenyong’onyea na kububujikwa na machozi.

Nasema taarifa hiyo iliniuma na kunisononesha sana kwa sababu Jumatatu wiki hii, saa 11 jioni Luhwago alipiga simu katika chumba chetu cha habari akitaka kufahamu mwandishi gani amepangwa kuongoza nao kesho (Jumanne) kwenda katika Kambi ya Mafunzo ya Ulinzi wa Amani iliyopo Msata-Bagamoyo, nilizungumza naye akaniambia gari litakuwa Idara ya Habari Maelezo saa moja kamili hivyo niwahi.

Baada ya kuzungumza naye nilimweleza Mhariri wa habari Msaidizi wa gazeti letu, Tamali Vullu, akaniambia niandike kwenye kitabu cha kupangiana kazi ‘Diary’ ya ofisi kama ilivyo ada , kisha asubuhi niende na waandishi wa Jeshi Msata kwa ajili ya kuandika habari ambapo siku hiyo Msuluhishi wa Mgogoro wa Jimbo la Darfur, Dk.Salim Ahmed Salim alikuwa anakwenda kuwafunda wanajeshi 875 wanaokwenda kulinda amani jimboni humo.

Ilipofika Jumanne saa 11:20 alfajiri niliwaomba kaka zangu Liston na Mathayo wanisindikize kituoni ili nikapande basi kweli walifanya hivyo tukiwa njiani kuelekea kituoni mvua ilitunyeshea.Nilipanda basi na kufika Posta saa 12:23 asubuhi nikaingia chumba chetu cha habari nakuanza kuiboresha makala yangu iliyotoka Jumatano iliyokuwa na kichwa cha habari “Malecela,Malecela umenisikitisha sana”.

Baada ya kumaliza kuiboresha nikamkabidhi mwandishi mwenzangu Ruhazi Ruhazi ili amkabidhi Mhariri wa Habari wa Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Charles Mulinda, na kisha saa 1:20 nikafika Maelezo na kukuta gari aina ya Hiace mali ya JWTZ ikiwa na waandishi wa habari wa jeshi na magazeti ya binafsi na serikali wakiwa wameketi na nilipofika gari lilianza kuondoka kuelekea Msata na ndani ya gari hilo nilikuwa mwandishi wa kike peke yangu.

Kama ilivyo kwa wanajeshi wengi wakiwemo wanahabari wa jeshi hilo pindi ninapokutana nao, hupenda kuniita mtoto wao kwa kuwa baba yangu aliwai kulitumikia jeshi hilo na mama yangu Oliva Katabazi anaendelea kulitumikia akiwa ni mtumishi raia hadi sasa.

Wakati tukiwa ndani ya gari tulipiga soga, kubadilishana mawazo na kucheka sana huku marehemu akiwa ameketi kiti cha mbele na ndiye alikuwa mkuu wa msafara huo.

Lakini kabla ya kuketi kwenye nafasi hiyo alinitaka nikae mimi nikakataa nikasema sitaki kwani endapo ajali itatokea mimi ndiyo nitakuwa wakwanza kufa.Walicheka sana akaniambia hivi ‘ujanja wako wote unaogopa kufa’ ,nikamjibu ndiyo kwani mwanangu Queen bado mdogo nikifa atapata taabu.

Tulitumia barabara ya Morogoro lakini ilipofika saa nne asubuhi tukiwa maeneo ya Kongowe- Kibaha gari hilo liliharibika hivyo kusababisha wote kushuka na gari lile likapelekwa kwa fundi kwa matengenezo na matengenezo hayo yalichukua saa moja na nusu.

Wakati gari hilo likitengenezwa, Luhwago alikuwa akipokea simu toka kwa maofisa wenzake waliopo Msata ambao walikuwa wakitaka awajulishe tumefika wapi mbona tunachelewa kufika.

Ndipo nilimsikia akiwajulisha kwamba gari tulilopanda limeharibika na limeanza kutengenezwa, nao walimweleza tayari mgeni rasmi Dk.Salim ameishafika na tunaosubiriwa ni sisi waandishi wa habari.

Lakini maofisa wale waliokuwa Msata walimpigia tena Luhwago na kumweleza kuwa wamefikia uamuzi wa kutuma gari jingine aina ya Defender lituchukue na kwamba gari lile lilokuwa linatengenezwa libakie kwa ajili ya matengenezo.

Wakati tukisuburi gari lile litengenezwe, Luhwago aliniuma sikio na kuniambia kuwa Julai mwaka huu, kutakuwa na maadhimisho ya Vita ya Kagera na itafanyika Mkoani Kagera.

Mimi nilimshauri kwamba kama hivyo ndivyo basi ni vyema Idara yao ishirikiane kwa karibu na vyombo vya habari ili kabla ya kufikia kwa kilelecha maadhimisho hayo, ziwe zinatolewa makala kuhusu Vita hiyo na watu wanajeshi mbalimbali walioshiriki kwenye vita hiyo kupitia vyombo vya habari wasimulie jinsi ilivyokuwa ili wananchi hasa sisi tuliozaliwa 1979 -2000 tuweze kujua kwa mapana jinsi vita hiyo ilivyopiganwa.

Aliendelea kuniambia kuwa Idara yao ina kuza mahusiano na vyombo vya habari kwani baadhi ya waandishi wa habari wamekuwa wakishindwa kufika katika ofisi yao kutafuta habari kutoka na kujengeka kwa ile dhana ya watu kuogopa kuingia kwenye kambi za Jeshi.

Nilimwambia mtakuwa mmefanya vizuri na kumwambia Idara yao warudishe ule utaratibu wa angalau kwa miezi mitatu mara moja kufanya kikao cha mapitio ya magazeti kinakachowashirikisha waandishi wa habari toka vyombo vya habari.

Hata hivyo sikusita kutoa pongezi kwa Idara hiyo kupitia kwake kwani kwa kipindi cha miaka miwili sasa kwa sisi tunaopenda kuandika habari za jeshi hilo tunaona kuna mabadiliko makubwa kwani ule urasimu wa kupata habari toka kwenye jeshi hilo umeanza kutoweka.

Meja Luhwago alikubalina nami na kuniambia kuwa atalifikisha kwa wakubwa wake ili liweze kufanyiwa kazi.

Mungu alijalia kheri ilipofika saa 6:04 mchana, gari lile lilipona na tukaanza safari kuelekea Msata na tulipofika njia panda ya kuelekea kwenye kambi hiyo tulikutana na ile Defenda likaanza kutuongoza hadi kwenye kambi hiyo ambayo ipo porini sana.

Tukafika salama kambini pale na kupokewa vizuri lakini tulikuta Dk.Salim ameishamaliza kuzungumza na wanajeshi hao na akawa anaondoka uwanjani pale na kupelekwa kwenye sehemu iliyotengwa maalum kwaajili ya kupata mlo wa mchana.

Tulimtumia Meja Lwagho ruhusa ili tuweze kuzungumza na Dk.Salim pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi hilo, Luteni Jenerali Abdurhman Shimbo.

Baada ya kufikisha maombi yetu kwa viongozi hao walikubali na kabla ya kuanza kupata mlo wa mchana walitueleza yale waliyozungumza na kikosi hicho kinachokwenda Darfur na kikubwa waliwasisitizia nidhamu, kutokuwa wabaguzi na kutimiza majukumu yaliyowapeleka na si vinginevyo.

Nikiwa huko nilipata fursa ya kufahamiana na kuzungumza na wanajeshi mbalimbali wanaokwenda huko huku wengine nikawatania kuwa kukubali kwao kwenda Darfur kufa , wamekusudia kutelekeza familia zao.

Nilimtania Mkuu wa Kikosi cha wanajeshi wanaokwenda Darfur Luteni Kanali Alli Mzee Katinde na vijana wake kuwa wamedhamiria kutelekeza familia zao ndiyo maana wameamua kujitoa sadaka kwenda huko ili akatolewe roho, yeye na wanajeshi wake walinicheka sana wakaniambia hivi siku ya kufa ikifika,kifo kitamsaka mhusika kokote alipo na siyo lazima kwao wanaokwenda Darfur.

Walinitania kuwa watapiga simu kwa bosi wangu nibaki kule Msata ili wanipe mafunzo kidogo ya kufunga buti na kuvaa kombati na kutembezwa msituni kisha waondoke na mimi Darfur.Nikacheka.

Nilimwomba Luhwago aniombee kwa wanajeshi wale nipige nao picha za kumbukumbu, alifikisha ombi langu na kweli wanajeshi wale walikubali na nikapiga nao picha za kumbukumbu.Siku hiyo waandishi wote akiwemo marehemu tulikuwa ni watu wenye furaha tangu tulipoanza safari yetu asubuhi.

Baada ya kukamilika kwa hatua hiyo tuliagana na wanajeshi wale na kupanda gari letu saa 8:02 na kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam.

Binafsi kambi ya Msata nimekuwa niikisikia tangu nikiwa na umri mdogo lakini sikuwahi kufika kule hivyo nililishukuru Jeshi kuandaa safari ile kwani imesababisha mimi kukanyaga katika ardhi ya kambi ile.

Sikusita kumuuliza maswali ya hapa na pale marehemu na Ofisa Mteule Issa ambaye ni mpiga Picha wa gazeti la Ulinzi, kuwa ile ndiyo kambi ambayo baadhi ya wanajeshi huteuliwa kwenda kule kwa ajili ya mazoezi ,walinijibu ndiyo.

Nilimuuliza pia nilikuwa nikiambiwa kuwa kambi ile awali ilikuwa ikitumiwa na wapigania uhuru wa nchi marafiki wa Tanzania, akasema ndiyo na kuongeza kuwa ila hivi karibuni kambi hiyo imetumika kutoa mafunzo kwa Peace Making kwa walinzi wa amani watakao kwenda Darfur.

Kwakuwa tulikuwa tumeishakula chakula cha mchana tulivyokuwa kwenye gari wengi wetu walikuwa wakisinzia.Natulipofika Kibaha Mhariri wangu Charles Mulinda alinipigia simu akataka nimueleze Dk.Salim amezungumza nini nikamweleza akaniambia ananiwekea nafasi katika gazeti kwaajili ya habari nitakayokuja nao.

Tulipofika Ubungo mataa tairi la gari liliisha upepo, dereva aliyekuwa akiendesha alimweleza marehemu na tukaingia kwenye sheli moja karibu na Ubungo mataa, likajazwa upepo tunaanza safari tukaelekea ofisi za TBC 1, kupeleka mkanda wa tukio la Msata, tulivyokabidhi ofisini hapo tukaanza safari ya kuelekea Posta.

Tukiwa njiani marehemu ambaye nadiriki kutamka kuwa ni miongoni mwa waandishi wa jeshi wachache waliokuwa wanamahusiano mazuri ya kikazi na vyombo vya habari, alisema Idara yao inafanya jitihada kuhakikisha ule urasimu usio wa lazima wa upatikaji habari zisizo hatarisha usalama wa jeshi zinatolewa kwa vyombo vya habari bila vikwazo.

Wakati tukiendelea na mazungumzo hayo alisema ‘Waandishi wa JWTZ siyo malaika na kwamba hali ya vikwazo visivyo vya lazima vya upatikaji wa habari kwa vyombo vya habari nao pia inawakela na watashirikiana wakuu wao kuakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.

Akasema Idara yake ipo mbioni kuandaa ‘Question Air’ ambazo zitapelekwa kwa baadhi ya vyombo vya habari ili waweze kueleza ni matatizo gani yanawakumba wakati wakutafuta habari za jeshi hilo.

Akasema endapo maswali hayo sisi waandishi wa uraiani tukiyajibu kwa ufasaha yataisaidia Idara ya Uhusiano wa Jeshi hilo kujijua matatizo hayo na kisha kurekebisha kasoro hizo haraka iwezekanavyo kwani jeshi hilo ni la wananchi na kwamba wananchi wanaoitaji kujua habari na nini kinafanywa na jeshi hilo.

Basi gari hilo liliwateremsha waandishi wengine maelezo na mimi wakanifikisha hadi ofisi Mtaa wa Mkwepu saa, 11:35 jioni nikashuka na kuingia ofisini na kwenye gari hilo akabakia mpigapicha wa gazeti la Uhuru na Mzalendo, Yasin Kayombo ambaye naye pia walipeleka ofisini kwake Lumumba.

Nakumbuka neno la mwisho aliniambia kesho siku ile ya Jumanne jioni,kuwa atamwagiza askari aniletee picha zilipigwa Msata ili niweze kuzitumia kwenye makala yangu na kunitaka kuzingatia tuliyojadili kwenye safari yetu na kwamba niendelee kufanyakazi yangu ya uandishi wa habari kwa maslahi ya taifa hili na si vinginevyo.Nami nilimjibu nimekuelewa afande nitazingatia hilo.

Kumbe maneno hayo yalikuwa ni maneno ya mwisho kwangu na kwamba siku ile ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kuonana naye hapa duniani.Hakika nakulilia Kaka Luhwago.Mazuri uliyotuachia tunaendeleza.

Hiyo siyo mara yangu ya kwanza kufanyakazi kazi Luhwago kwani mara kwa mara nimekuwa nikienda kwenye ofisi yao kutafuta habari, ukiacha kwenda nae Msata, Machi 4 mwaka huu, nikiwa na waandishi wenzangu na wajeshi aliongoza msafara wetu kwenda kwenye uzinduzi wa Kamandi ya Majeshi ya Nchi Kavu-Kibaha.

Namlilia Luhwago kwani licha ya kuwa mwanajeshi lakini alipenda kupokea changamoto na kuzifanyia kazi tofauti na wanajeshi wengine ambao ukweli kwao ni sumu.Nitamkumbuka Luhwago kwa upole wake na utendaji kazi wake.Tangulia Luhwago kwani tayari umeshatimiza kazi uliyotumwa na mungu hapa duniani.

Natamani Luhwago afumbue macho atimaze waandishi wa habari gazeti la Ulinzi, wanajeshi wenzake,waandishi wa vyombo vya habari vya uraiani,tunavyokulilia.Hakika tumempoteza mtu muhimu ndani na nje ya jeshi.Lakini yote hiyo ni mapenzi ya mungu.

Luhwago hadi anafariki ghafla Jumanne usiku, alikuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano na Mhariri Mkuu wa gazeti la Ulinzi linalotolewa kila mwezi Meja William Luhwago.

Wakati wa uhai wake Meja Luhwago alishika nyadhifa mbalimbali akiwemo Mwandishi wa habari mwandamizi Makao Makuu ya Jeshi, Mhariri Mkuu wa gazeti la Ulinzi, Mkuu wa Kitengo cha Uandishi na Kaimu Mkurugenzi wa habari na mahusiano ya Umma Jeshini wadhifa aliokuwa nao hadi alipofariki Dunia.

Marehemu Luhwago alizaliwa mkoani Iringa Jun 01, 1959 na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Bomalang’ombe baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari Lugalo na kuhitimu mwaka 1985.

Mwaka 1986 alijiunga na Nyegezi Social Training Institute na kutunukiwa Stashahada ya Uandishi wa Habari 1988. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha St Augustino katika Shahada ya kwanza ya Habari Mawasiliano mwaka 2003 hadi 2005 na kutunukiwa Shahada. Mpaka anafariki alikuwa anasomea shahada ya Uzamili katika chuo Kikuu cha SAUTI tawi la Dar es Salaam.

Meja Luhwago alijiunga na JWTZ mwaka 1977, Wakati wa utumishi wake jeshini alipandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali hadi kufikia cheo cha Meja.Katika utumishi wake alishiriki shughuli mbalimbali za Kijeshi zikiwemo kumwondoa Nduli Idd Amini, kulinda amani Nchini Liberia na operasheni ya kuzuia majangiri huko Ngorongoro.

Pia atakumbukwa kwa mchango wake wa uadilifu, uaminifu na uchapakazi alioutoa katika jeshi kwa muda wote wa utumishi wake. Marehemu ameacha mke na watoto watano.

Marehemu atazikwa leo kwa heshima zote za kijeshi katika kijiji cha Bomalang’ombe, kata ya Bomalang’ombe, Wilaya ya Kilolo, mkoa wa Iringa.Tangulia Meja Luhwago, tutakufuata.

Mungu ailaze roho yako mahali pema peponi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, April 3, 2009










No comments:

Powered by Blogger.