Header Ads

MRAMBA AMLIPUA MKAPA

*Adai Ikulu ndiyo iliyotoa vibali vya Alex Stewart
* Wakili wake adai alikuwa mtumishi mwaminifu

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Basil Mramba, amekiri kutoa vibali vya msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart, baada ya Ofisi ya Rais Ikulu kuridhia afanye hivyo.

Mramba ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7, alikiri hilo wakati akisomewa maelezo ya awali ya kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya Mramba ambaye ni mteja wake, Wakili Hurbet Nyange mbele ya Hakimu Mkazi, Henzron Mwankenja, alidai mteja wake alikuwa mwaminifu na kusisitiza kuwa, alitoa vibali hivyo baada ya kuagizwa kufanya hivyo na Ikulu.

Nyange ambaye alikuwa akizungumza kwa ukali, alikiri Mramba kumuandikia barua Gavana wa Benki Kuu ya kumtaka iilipe Kampuni ya Alex Stewart, lakini alifanya hivyo baada ya Ikulu kuridhia, kwani mteja wake hakuwa na mamlaka ya kuidhinisha malipo hayo.

“Kwa faida ya mpelelezi wa kesi hii, nakubali mteja wangu alitoa vibali vya msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo, ila nataka ieleweke hivyo kuwa alitoa vibali hivyo baada ya Ikulu kuridhia.

“Pia nakataa serikali haijapata hasara kwa sababu hasara hiyo imetokana na mkataba wa kijinga wa Kampuni ya Alex Stewart.

“Kwa hiyo, maelezo mengine yaliyosalia hatuyakubali kabisa kwa kuwa yamejaa sukari na chumvi na uongo na ukweli…hatuyakubali, sasa kuna hatari nikiyakubali tutakuwa tunakubali yale ya ukweli na uongo. Kwa usalama wetu tunakataa maelezo yote,” alidai Nyange kwa sauti ya ukali na kusababisha mawakili wenzake kumkatisha mara kwa mara bila mafanikio.

Akisoma maelezo hayo, Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Joseph Holle ambaye alikuwa akisaidiana na Tabu Mzee kutoka Takukuru na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda, alidai Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini katika serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Uchumi na Fedha, Gray Mgonja, walikuwa watumishi wa umma na wenye nyadhifa za juu serikalini, maelezo ambayo washitakiwa wote waliyakubali.

Holle alidai washitakiwa hao wakiwa na nyadhifa hizo, walikuwa na jukumu la kuwa waaminifu na makini katika majukumu waliyokabidhiwa kisheria.

Alidai Machi 3, mwaka 2003 mshitakiwa wa pili (Yona), aliandika barua yenye kumbukumbu namba CDA 111/338/01 inayotaka kibali cha rais, ili wizara yake iweze kuingia mkataba wa kuikodi kampuni ya kutafiti madini ya dhahabu.

Alidai barua hiyo ilikuwa ikimshawishi rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kwamba endapo kampuni hiyo itakodishwa, itakuwa ikisimamiwa na Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania na kwamba inatakiwa kitafutwe chanzo mbadala cha mapato kwa ajili ya kukodisha kampuni hiyo kwa sababu mradi huo haukuwapo kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2003/2004.

Holle alidai wakati mchakato huo ukiendelea baina ya Wizara ya Nishati na Madini, Fedha na Benki Kuu Mei 11 mwaka 2003, Yona alimuandikia tena barua rais, yenye kumbukumbu namba CDA/111/338/01 kumkumbushia ombi lake la kutaka kibali cha kampuni hiyo ya utafiti wa madini kuanza kufanya kazi.

Aliendelea kudai kuwa, Juni 12, 2003, Mramba katika barua yake namba TYC/M/30/2 alimtaarifu Yona kuwa ukodishaji wa kampuni huru ya utafiti wa dhahabu umekuja wakati bajeti ya mwaka wa fedha wa 2003/2004 imeishafungwa na kwamba makusanyo ya mrahaba unaotokana na sekta ya madini tayari umeishaingizwa kwenye matumuzi mengine.

Alidai Mramba alimshauri Yona kwamba, bajeti ya mradi huo itaingia kwenye bajeti ya nyongeza ya mwaka 2003-2004 na kwamba atapeleka pendekezo hilo bungeni kuwa, chanzo mbadala cha fedha za kukodisha mradi huo kitatokana na mrahaba wa madini.

“Lakini mshitakiwa wa kwanza hakupeleka ombi hilo kwenye Baraza la Mawaziri, ili lijadiliwe bungeni na badala yake alimuuliza Mgonja amshauri ni jinsi gani anaweza kuisamehe kodi Kampuni ya Alex Stewart,” alieleza mwanasheria huyo.

Aidha, alidai Mei 15, mwaka 2003, aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Alhaji Abdisalaam Khatib, alimshauri Yona kwamba taratibu za ukodishaji wa kampuni huru ya utafiti wa dhahabu, usubiri hadi wataalamu toka Sekretarieti ya Commonwealth iishauri Serikali ya Tanzania kama itatumia mtindo gani wa kufanya kazi na aina gani ya madini itatafiti.

Aliendelea kudai kuwa, Mei 26, mwaka 2003, Godwin Nyero ambaye alikuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria ya Wizara ya Madini na Nishati, ambaye alikuwa ni mjumbe katika timu ya majadiliano ya serikali, alimshauri Yona kuwa, kampuni hiyo haikuwa wazi kwenye timu yao ya majadiliano na kwamba inakwenda kinyume na mawazo ya Alex Stewart (Assayers) ya mkataba.

Alidai kuwa, Septemba 11, mwaka 2002 Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini na Nishati, B. Mrindoko naye alimshauri Yona afuate Sheria ya Manunuzi ya Umma katika kuingia mkataba na kampuni hiyo.

Licha ya ushauri huo, Juni 12, mwaka 2003 Mramba alimuelekeza aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, marehemu Daudi Balali kupitia barua namba TYC/M/30/2 kuilipa malipo ya awali Kampuni ya Alex Stewart dola milioni moja.

Aliendelea kueleza kuwa, Juni 23, mwaka 2003, Mamlaka ya Mapato (TRA) katika barua yake namba TRA/SB/E/1.3/Vol.XVII/32 ilimtaarifu Mgonja kwamba, kampuni hiyo haimo kwenye orodha ya makampuni yanayosamehewa kodi.

Katika barua nyingine namba TRA/E/1.3/Vol.XVII/31 ya Oktoba 7, mwaka 2003 kwenda kwa Mgonja, ilieleza kuwa kampuni hiyo inatakiwa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchini.

“Kwa masikitiko makubwa, licha ya maagizo hayo ya TRA, Mgonja alimshauri Mramba kuendelea na mchakato wa kusaini vibali vya serikali vya kuisamehe kodi kampuni hiyo, ambapo vibali hivyo vimesababisha serikali kupata hasara ya sh 11,752,350,148,” alidai Holle.

Kwa upande wa wakili wa mshitakiwa wa pili, Joseph Tadayo, alidai mteja wake anakubali jina lake na kwamba alikuwa Wazini wa Madini na Nishati na malezo mengine anayakata.

Kwa upande wa wakili wa mshitakiwa wa tatu, Profesa Shaidi, naye alikubali mteja wake alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na kwamba alikamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani.

Baada ya kusoma maelezo hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Manyanda alidai upande wa mashitaka utakuwa na mashahidi 13 na miongoni mwa mashahidi hao, ni aliyekuwa Naibu wa Waziri wa Fedha wa serikali ya awamu ya tatu, Alhaji Abdisalaam Khatib.

Hata hivyo, Manyanda alidai wamepunguza idadi ya mashahidi kwa sababu upande wa utetezi umekataa sehemu kubwa ya maelezo ya awali.

Baada ya kutoa orodha hiyo ya mashahidi, Nyange alitaka upande wa mashitaka utaje vielelezo watakavyovitumia kwenye kesi hiyo na kwamba sheria inawataka wafanye hivyo.

Hoja hiyo ilipingwa na Manyanda na kueleza hawawezi kutaja vielelezo vya kesi hiyo, na badala yake vielelezo hivyo watavitoa wakati kesi itakapokuwa ikiendelea kusikilizwa, majibu ambayo hayakumridhisha Nyange, ambaye alisimama tena na kushinikiza watajiwe idadi ya vielelezo hivyo.

Ndipo Hakimu Mwankenja aliingilia kati na kumtaka Nyange aonyeshe ni kifungu gani cha sheria kinataka hilo lifanyike. Nyange alishindwa kutaja sheria hiyo.

Akiahirisha kesi hiyo jana, Hakimu Mwankenja alisema kesi itaanza kusikilizwa Mei 18, mwaka huu na kuutaka upande wa mashitaka uhakikishe unakuwa na mashahidi siku hiyo.
Wakati huo huo, Mwankenja amekubali ombi la Mramba la kutaka aruhusiwe kwenda Dodoma kuhudhuria kikao cha Bunge na kumtaka arudi Dar es Salaam Mei Mosi, mwaka huu.

Novemba 25 mwaka jana, washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, wakikabiliwa na mashitaka 12 ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia hasara ya sh bilioni 11.7

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, April 18, 2009

No comments:

Powered by Blogger.