UFISADI WAITIKISA DECI
*Fedha za serikali zadaiwa kupandikizwa
*Wahasibu wa wizara wahaha kuzirejesha
*DCI Manumba aomba jeshi lake lisaidiwe
*Wanaupatu waendelea kupanda na kuvuna
Na Happiness Katabazi
SAKATA la Kampuni ya Development Entrepreneurship Community Initiative (DECI), inayojihusisha na biashara ya kupanda na kuvuna fedha, linazidi kuchukua sura mpya baada ya kuwapo madai kwamba baadhi ya wahasibu wa wizara mbalimbali, wamepandikiza mamilioni ya fedha za serikali.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata, zinasema kuwa baadhi ya wahasibu wa idara mbalimbali serikalini, walichota mamilioni ya fedha za umma na kuzipandikiza kwenye kampuni hiyo, kwa lengo la kuzirejesha baada ya muda mfupi wakishajitengenezea faida.
Watumishi wa baadhi ya wizara serikalini (majina tunayahifadhi), waliliambia gazeti hili kwamba, wahasibu wao walichukua sehemu ya fedha za utawala serikalini, na kwenda kuzipandikiza DECI.
“Hapa kwetu bwana, mhasibu wetu na wasaidizi wake wengine, walichukua fedha za wizara na kwenda kuzizungusha DECI ili wapate faida, halafu wazirudishie kwenye bajeti ya wizara.
Ilikuwa ni katikati ya mwezi wa pili tu mwaka huu,” alisema mtumishi wa wizara moja na kuungwa mkono na wenzake wawili, ambao wote hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini.
Kwa mujibu wa habari hizo, wapo wahasibu waliofanikiwa kupanda fedha za serikali na kuvuna, lakini wapo waliokwama baada ya kuibuka kwa sakata la uhalali wa shughuli za DECI nchini.
Watumishi hao wamemtaka Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, pamoja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, kufanya uchunguzi wa haraka ndani ya idara zote za fedha serikalini, kwani wanaamini mchezo huo utakuwa umefanyika katika wizara zote.
“Yaani nakwambia leo ukifanyika ukaguzi hapa, wahasibu wetu wataumbuka. Maana kuna fedha ambayo watashindwa kuitolea maelezo. Hawawezi kusema waliipeleka DECI, kazi yao si kufanya biashara kwa fedha za serikali. Wewe mwandishi unajua sheria za kazi. Haiwezekani mtu uchukue fedha za ofisi halafu ukazizungushe huko nje. Hata kama utazirejesha, huo bado utabakia kuwa ni ufisadi,” alisema mtumishi huyo.
Alipoulizwa ni lini wahasibu hao wanatarajiwa kuzirejesha fedha hizo, alisema hilo ni vigumu kujua, lakini akasisitiza kuwa wanachojua ni kwamba wamechukua fedha za wizara na kwenda kuzipanda DECI.
“Hiyo ni vigumu kujua, sisi tunachojua ni kwamba walichukua fedha za wizara na kuzipeleka DECI. Siri ilivuja kuanzia ndani ya ofisi yao, hapa bosi hawezi kufanya kitu tusijue. Cha msingi mtusaidie Katibu Mkuu Kiongozi na polisi, akina Manumba wafanye upelelezi haraka,” alisema.
Alisema kuwa ana hofu kuwa mchezo huo wa wahasibu unaweza ukasababisha kuchelewa au kutolipwa madai yao mbalimbali kwa wakati kutokana na fedha nyingi kupandikizwa kwenye upatu wa DECI.
Aidha, vyanzo vyetu ndani ya Jeshi la Polisi pia vilithibitisha kuwapo kwa baadhi ya watumishi wa idara za fedha, waliopandikiza fedha za jeshi hilo DECI, wengi wakiwa wamefanya hivyo kati ya Novemba mwaka jana na Machi mwaka huu.
Akizungumzia kuibuka kwa madai hayo, DCI Manumba, kwanza alishitushwa na taarifa hizo na kuwataka waliozitoa kujitokeza ofisini kwake ili walisaidie jeshi hilo.
Alisema katika suala hilo ambalo alikiri ni mara ya kwanza kulisikia, aliwaomba watoaji taarifa hizo, walisaidie jeshi lake kwa kuwataja wahusika kwa majina ili jeshi hilo lipate pa kuanzia na kuhakikishia kwamba jeshi litatunza siri hiyo.
“Sisi hao waliotoa hizo taarifa tunawaomba wafike Jeshi la Polisi, kuwataja kwa majina hao wahusika, ili Jeshi la Polisi lijue wapi pa kuanzia,” alisema Manumba.
Wakati huo huo, umati wa wanachama wa DECI, jana waliendelea kufurika katika ofisi za kampuni hiyo, zilizoko Mabibo, ambapo walikuwa wakiitwa kwa namba na kupangwa kwenye foleni ndefu kwa ajili ya kuvuna mbegu walizopanda.
Huku wakiwa chini ya ulinzi wa askari polisi wenye silaha, na walinzi wa kampuni binafsi, viongozi wa kampuni hiyo walikuwa wakitangaza kuwa, kutokana na jana kuwa siku ya mapumziko, walipewa ruhusa na serikali ya kufanya kazi mpaka saa sita mchana.
“Leo ni sikukuu, kwa vile serikali inatupenda, imetupa muda wa kufanya kazi leo mpaka saa sita, tunyooshe namba juu, tumalize, wakiisha hawa tuonane Jumanne hapa, Bwana asifiwe,” alisema kiongozi huyo, ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
Alisema kuwa Jumanne, watakutana hapo kwa ajili ya wateja waliotakiwa kuvuna Aprili 7 na 9, mwaka huu, kutokana na kutokutolewa huduma kwa sababu ya mkutano wa maaskofu na wanaupatu, uliofanyika katika Ukumbi wa PTA Sabasaba.
Mamia ya wanaupatu hao, walisikika wakisema kuwa wanakerwa na tangazo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), linaloendelea kutolewa kwenye vyombo vya habari kuwa, haiitambui DECI, wakati inatoa huduma zake kwa mujibu wa sheria.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, April 11, 2009

No comments:
Post a Comment