Header Ads

MAHAKAMA:MAHALU ANA KESI YA KUJIBU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imesema kuwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin, wana kesi ya kujibu.

Uamuzi uliotolewa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani nchini, Sivangilwa Mwangesi, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili kutolewa uamuzi wa ama washitakiwa wana kesi ya kujibu au la.

Akitoa uamuzi huo, Naibu Msajili Mwangesi alisema washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka sita.

Alitaja mashitaka hayo kuwa ni kula njama kwa nia ya kutenda kosa, shitaka la pili, tatu na la nne ni la kutumia hati zenye maelezo yasiyo sahihi kwa lengo la kumdanganya mwajiri wao, ambaye ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shitaka la tano ni la wizi na shitaka la sita ni kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni mbili.

Alisema mahakama imejiridhisha kwamba watuhumiwa hao wana kesi ya kujibu baada ya upande wa mashitaka kuleta mashahidi saba na vielelezo tisa.

“Mahakama hii baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi saba na vielelezo tisa, imeshawishika kuona washitakiwa wana kesi ya kujibu na kuwahoji mawakili wa utetezi kwamba wateja wao watatoa ushahidi wao kwa njia gani,” alisema Mwangesi.

Wakili wa utetezi, Bob Makani na Alex Mgongolwa, walidai kuwa wateja wao watajitetea kwa njia ya kiapo na kwamba mshitakiwa wa pili, Grace ataleta mashahidi watatu wakati Profesa Mahalu ataleta mashahidi kadiri kesi itakavyoanza kusikilizwa.
Aidha, Mwangesi alisema washitakiwa hao wataanza kujitetea mfululizo kuanzia Mei 4 mwaka huu na kutaka mashahidi wafike bila kukosa.

Mapema Januari mwaka juzi, washitakiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya sh bilioni mbili, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Ijumaa, April 19, 2009

No comments:

Powered by Blogger.