Header Ads

KESI YA WATOTO WA VIGOGO BOT YAANZA KUUNGURUMA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE kesi ya kughushi vyeti vya kidato cha nne inayowakabili wafanyakazi nane wa Kitengo cha kuhesabu fedha chakavu katika Benki Kuu ya Tanzania(BoT), jana ilianza kuunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.

Washtakiwa hao ni Justine Mungai, Christine Ntemi,Siamini Kombakono, Janeth Magehenge,Beather Masawe, Jacquline Juma, Philimina Mutagurwa na Amina Mwinchumu ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Majura Magafu, Jerome Msemwa,Mpare Mpoki.

Katika kuonyesha upande wa serikali umejipanga vyema katika kesi hiyo, jana kabla ya shahidi wa kwanza kuanza kutoa ushahidi, Mwendesha Mashtaka Kiongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Edger Luoga mbele ya hakimu mkazi Neema Chusi, aliwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao kwa nyakati tofauti walighushi vyeti vya kidato cha nne vinavyoonesha vilitolewa na Baraza la Taifa la Mitihani(NECTA).

Luoga alidai baada ya kughushi vyeti hivyo mwaka 20001,waliviwasilisha kwa mwajili wao ambaye ni BOT na wakapata ajira katika kitengo cha kuhesabu fedha chakavu.Na ilipofika 2005 Takukuru walipata taarifa toka wasiri wao zilizoeleza ndani ya benki hiyo kuna watumishi walipata ajira kwa rushwa na kwamba walighushi vyeti.

Alidai Takukuru walifanya upelelezi wao na kupeleka vyeti vya washtakiwa hao NECTA na baraza hilo la mitihani liliidhitishia taasisi hiyo kuwa vyeti hivyo ni vya kughushi na mshitakiwa kwanza,pili,nne na sita wakati wakihojiwa na Jeshi la polisi walikiri kuhusika kutenda makosa hayo.

Lakini baada ya Luoga kumaliza kuwasomea maelezo hayo ya awali, washtakiwa wote walikana maelezo hayo na walikubali majina yao na kwamba ni kweli wao ni waajiriwa wa BoT.Upande wa mashtaka ukaiambia mahakama kuwa katika kesi hiyo itakuwa na mashahidi saba wakiwemo mashahidi toka Takukuru, BoT na NECTA na itasikilizwa mfululizo.

Mwendesha Mashtaka Kiongozi Luoga alimuongoza shahidi wa kwanza Thadei Nzalalila ambaye ni mchunguzi toka Takukuru, kutoa ushahidi wake.Ifuatayo ni mahojiano kati ya Luoga na Nzalalila.
Swali:Timu yenu ilikuwa na wajumbe wangapi ambao mlikuwa mnachunguza tuhuma hizi ambazo zinawakabili washtakiwa waliopo mahakamani?
Jibu:Tulikuwa na Richard Mkungu, Faraja Nyagawa, Fredrick Mbasili, Abinel Mganga na wengine ambao nimewasahau.
Swali:Ukiwa na timu ya uchunguzi ya Takukuru, mlianzia wapi kufanya uchunguzi wenu?
Jibu:Tulianzia uchunguzi BoT kwa kukusanya nyaraka mbalimbali.
Swali:Ni nyaka zipi hizo mlizikusanya BoT?
Jibu:Vyeti vilivyotimiwa kuomba na orodha ya majina ya wafanyakazi wanaofanyakazi katika idara ya kuhesabu fedha chakavu katika benki hiyo.
Swali:Nini kilifuata kilifuata baada ya nyie kuwasilisha maombi katika benki hiyo kutaka mpatiwe nyaraka hizo?
Jibu:Uongozi wa BoT ulitupatia ushirikiano kwa kutupatia nyaraka hizo tulizokuwa tukiziitaji.
Swali:Baada ya timu yenu kupatiwa nyaraka hizo mlikwenda wapi?
Jibu:Timu yetu ili kutaka kujiridhisha na tuhuma hizo, kwa heshima na taadhima ilikwenda NECTA.
Swali:Mlivyofika NECTA mlikutana na nini?
Jibu:Maofisa mbalimbali wa NECTA.
Swali:Baada ya kukutana na maofisa hao wa NECTA, waliileleza nini timu yenu ya uchunguzi kuhusu hivyo vyeti mlivyoenda kuvifanyia uchunguzi?
Jibu:Walitudhibitishia kuwa vyeti vile ni vya kughushi na kwamba havijawahi kutolewa na baraza la mitihani la taifa.
Swali:Ieleze mahakama timu yenu ilipeleka vyeti vingapi Necta?
Jibu:Takribani vyeti 17.
Swali:Kutokana na idadi majina mangapi ya vyeti vilibainika ni vya kughushi?
Jibu:Vyeti vya nane tu ambavyo vina majina ya washtakiwa waliosimama leo(jana) kizimbani.
Swali:Ulieleza mahakama hii kwamba mlipata taarifa toka kwa wasiri wenu kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi BoT waliajiriwa kwa rushwa, katika uchunguzi wenu mlibaini tuhuma hiyo ya rushwa?
Jibu:Hatukani rushwa ila tulibaini vyeti walivyotumia washatakiwa kupata ajira BoT vilikuwa ni vya kughushi.
Swali:Zaidi ya kuangaika na hivyo vyeti , wewe ukiwa ni mchunguzi mlifanya nini zaidi?
Jibu:Nilichukua maelezo ya onyo kwa mshtakiwa wa sita, Jacline Juma.
Swali:Ni utaratibu gani uliutumia kuandaa maelezo ya onyo kwa Jacqline?
Jibu:Nilimweleza maelezo atakayoyatoa ayatoe kwa ridhaa yake na kwamba yatatumika mahakamani kama ushahidi na maelezo hayo ya onyo niliyaandaa kwa mtindo wa maswali na majibu ambapo sehumu ya jibu mshitakiwa mwenyewe alikuwa akijibu kwa maandishi na kuweka saini yake na akakubali nami nikachukua maelezo yake.
Swali:Wewe una renki gani Takukuru?
Jibu:Afisa Mchunguzi, cheo changu ni sawa na Assistant Supertent of Police(ASP).
Swali:Baada ya kumaliza kumchukua maelezo ulifanya nini?
Jibu:Niliyafunga yale maelezo kama taratibu zinavyonitaka.
Swali:Je ungependa hayo maelezo ya onyo yapokelewe na mahakama hii tukufu kama ushahidi?
Jibu:Ndiyo.

Lakini ghafla aliinuka wakili Majura Magafu akitaka mahakama hiyo isipokee maelezo hayo shahidi huyo wakati akichukua maelezo ya onyo kwa mshitakiwa wa sita, akumweleza cheo chake,shhaidi huyo hakuwa na mamlaka ya kuchukua maelezo ya onyo kwasababu mashtaka yanayowakabili washtakiwa hayahusiani na rushwa na kwamba shahidi huyo ni mwanaume hivyo hakupaswa kuchukua maelezo ya mshtakiwa mwanamke na kwamba sababu hiyo alidai upande wa utetezi unaona hatua hiyo ni ya kitisho dhidi ya mshitakiwa wa sita.

Akijibu hoja za Magafu, Mwendesha Mashtaka Kiongozi wa Mahakama ya Kisutu, Edger Luhoga, alidai hoja ya kwamba shahidi hakuja cheo chake wakati anachukua maelezo ya onyo si ya kweli kwani shahidi alimweleza mshitakiwa kuwa yeye ni Mchunguzi wa Takukuru na kulingana na sheria zilizopo taasisi hivyo inafanyakazi za upelelezi kama polisi.

Luoga alidai kuhusu hoja ya kwamba mashtaka yanayowakabili washtakiwa hayahusiani na rushwa, alikiri kwamba mashtaka hayo hayahusiani na rushwa lakini kwasababu upelelezi wa shauri hilo ulianzwa na Takukuru na sheria Mwenendo wa Makosa ya Jinai, inampa madaraka DPP kuteua afisa yoyote toka polisi au Takukuru ambayo ilianza kuchunguza tuhuma za kesi husika.

“Na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, haisemi kuwa mtuhumiwa wa kike lazima achukuliwe maelezo ya onyo na mpepelezi wa kike na hoja ya mshitakiwa alipata vitisho kwasababu alihojiwa na mwanamme haina msingi wowote na tunaiomba mahakama itupilie mbalimbali pingamizi na wakili wa utetezi” alidai Luhoga.

Hakimu Chusi alisema malumbano hayo ya kisheria aliairisha kesi hii hadi leo ambapo atatoa uamuzi kuhusu mapingamizi hayo na kwamba kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kama ilivyopangwa.

Baada ya hakimu kuairisha kesi hiyo, washtakiwa wote wakiwa bado kizimbani walitoa vitenge na mitandio waliyokuwa wameiifadhi kwenye pochi zao na kujifunika nyuso zao na kichwani,ili kukwepa sura zao zisianekane kwa wapiga picha ambao walikuwa wakitaka kuwapiga picha, huku baadhi ya ndugu za washtakiwa ambao walifika kufuatilia kesi hiyo kutoka viti vya nyuma kuwapelekea kanga na vitenge ili wajitande mwili mzima.

Washtakiwa hao wote kwa pamoja walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Septemba 19 mwaka jana , wakikabiliwa na shitaka la kughushi vyeti vya kidato cha nne na kumdanganya mwajili wao BoT kwa kuwasilisha vyeti hivyo na kisha kupatiwa ajira.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, April 8,2009

No comments:

Powered by Blogger.