Header Ads

MSHITAKIWA KESI YA ZOMBE AWAGEUKA WENZAKE

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA wa 12 katika kesi ya mauji ya wafanyabaishara watatu na dereva taksi mmoja, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake tisa, Koplo Rajabu Bakari (46), amewageuka wenzake na kusema kuwa alishuhudia mauji ya marehemu hao yakifanyika msituni.

Washtakiwa wenzake katika ushahidi wao ambao tayari wamekwishautoa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Masati, kwa kauli moja walieleza kuwa mauji ya marehemu hao yalifanyika Sinza na ukuta wa Posta.

Koplo Rajabu ambaye jana alianza kutoa ushahidi wake saa nne asubuhi na kumaliza saa 9:58 jioni, alikuwa akiongozwa na wakili wake, Denis Msafiri ambaye aliileza mahakama kuwa mshitakiwa yeyote ambaye amewahi kuiambia mahakama hiyo kuwa mauji yalifanyika Sinza ameidanganya mahakama.

Rajabu alidai kuwa, mnamo Januari 14, mwaka 2006, yalifanyika mauji hayo katika eneo la msitu na kuongeza kuwa akiwa na marehemu Rashid Lema na Koplo Saad walikuwa ni miongoni mwa askari walioongozana na Mkuu wa Upelelezi wa Kinondoni, mshitakiwa wa pili, ASP-Christopher Bageni kwenye gari aina ya Pajero mali ya Jeshi la Polisi.

Aliendelea kusema kuwa, kwa pamoja walitoka eneo la barabara ya Sam Nujoma na kuelekea msituni uliopo barabara ya Morogoro huku gari moja aina ya defender ambalo lilikuwa limewabeba marehemu ambao walikuwa hai, likiwafuata na baada ya kufika huko, Bageni na Saad walishuka kwenye gari na kuwaacha kwenye gari hilo wakiwa wamekaa.

“Baada ya kutuacha kwenye gari nikasikia mlio wa risasi nikatoka ndani ya gari na kuelekea kwenye defender lilipobaki kule msituni ili nijue kulikoni, nikaona mtu mmoja akitolewa kwenye difenda na kushushwa chini na Saad nikamshuudia akimshindilia na risasi.

“Baada ya kuona hilo nikaangalia chini na kukuta miili mingine mitatu ikiwa imelala chini kimya inavuja damu kisha Bageni akatuambia mimi na Saad twende tukapande kwenye lile Pajero tulikuja nalo na kisha kurudi kituo cha polisi Urafiki,” alidai Bakari na kufanya umati wa watu kushikwa na butwaa.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya mawakili Denis Msafiri na Rajabu Bakari:
Swali:Januari 14, 2006 unakumbuka uliingia kazini saa ngapi siku hiyo?
Jibu:Niliingia asubuhi na nilikuwa zamu.
Swali:Ulikuwa zamu na askari gani?
Jibu:Marehemu Rashid Lema na Saad ambaye hadi sasa hajakamatwa.
Swali:Unakumbuka mlipangwa kufanya doria maeneo gani na ilitakiwa muanze na mmalize muda gani?
Jibu:Kinondoni, Mwananyamala na Mikocheni.Tulitakiwa tuanze saa 12 asubuhi hadi 12 ya asubuhi ya siku inayofuata ya Januari 15, 2006.
Swali:Ulikabidhiwa silaha?
Jibu:Tulipewa silaha ila Lema na Saad walipewa SMG mimi nilipewa Bastola.
Swali:Mbali na hizo silaha mlizopewa na mlikuwa na usafiri wa aina gani?
Jibu:Tulikuwa na gari aina ya Pajero na ilikuwa ikiendeshwa na Konstebo Frank.
Swali:Mlikuwa na redio Call?
Jibu:Asubuhi unapokuwa doria hatupewi redio call ila jioni unapokuwa kwenye doria ndiyo tunapewa. Na tunapewa baada ya kutoa taarifa za matukio tulikutuna nayo mchana.
Swali:Katika hiyo doria yenu, nani alikuwa kiongozi wenu?
Jibu:Mimi.
Swali:Mlivyorudi jioni pale Oyesterbay Kituoni kutoa taarifa za doria ya mchana, taarifa hizo mlitoa kwa nani?
Jibu: Mkuu wa Upelelezi wa Kituo, ASP-Bageni.
Swali:Katika hiyo zamu yenu, nani alikwenda kwa huyo mshitakiwa wa pili kutoa taarifa hizo?
Jibu:Mimi.
Swali:Hiyo taarifa ulitoa kwa njia gani?
Jibu:Mdomo na wakati nikienda ofisini kwa Bageni nilikutana naye anashuka ngazi akaniambia twende nae tulipoegesha gari akaniambia tuingie kwenye gari na tukiwa njiani akaniambia tunaanzia barabara ya Sam Nujoma.
Swali:Alikwambia Sam Nujoma kuna nini?
Jibu:Aliniambia kuna tukio la ujambazi watu wameibiwa.
Swali:Mlivyofika hapo Sam Nujoma mlikuta nini?
Jibu:Tulikuta lori tani tatu mali ya kampuni ya BIDCO likiwa katika barabara hiyo na ndani yake ilikuwa na watu wanne, majina yao siku yafahamu ila mmoja alisema yeye ni dereva mwingine ni kuli (mbeba mizigo), na tulifika eneo hilo jua rasmi likiwa limeisha na giza lilikuwa halijaanza kuingia.
Swali:Wewe ulinzungumza na hao watu?
Jibu:Hapana ila Bageni ndiye alikuwa akiwahoji.
Swali:Ulisikia mahojiano yao?
Jibu:Nilisikia wakisema wao ni wafanyakazi wa BIDCO na waliporwa fedha zao siku hiyo na kabla ya kuporwa walitishiwa bastora na walisema waliporwa sh milioni tano.
Swali:Baada ya Bageni kuambiwa hayo nini kilifuata?
Jibu:Bageni alisogea pembeni kidogo akaanza kuongea nasimu yake ya kiganjani na siyo redio call ambayo alikuwa ameshika mkononi.
Swali:Baada ya kumaliza kuongea na simu nini kilifuata?
Jibu:Gari aina ya Pick Up la Kituo cha Polisi Chuo Kikuu lilikuja pale Samnujoma tulipokuwa tumesimama na ndani yake ilikuwa imebeba watu wanne ukiacha polisi ambapo watu hao walikuwa wamekalishwa chini na askari wamesima.
Swali:Unaweza kufahamu idadi ya askari walikuwemo kwenye hiyo Pick Up?
Jibu: Sajent James, PC Noel ambaye alikuwa mshitakiwa mwenzetu ila mahakama hii ilimuachilia huru.
Swali:Hao watu wanne waliokuwa wamekalishwa chini ulikuwa una wafahamu?
Jibu:Hapana.
Swali:Hiyo Pick Up iliambatana na na gari jingine?
Jibu:Ndiyo iliambana na gari jingine aina ya Saloon yenye rangi ya Daki blue.
Swali:Kulikuwa na gari jingine?
Jibu:Baada ya muda kidogo ilikuja gari jingine aina ya Saloon ,nyeupe.
Swali:Baada ya hao watu wanne kuja na hayo magari manne kusimama hapo Samnujoma, nini kilifuata?
Jibu:Nilimtambua mshitakiwa wa tatu, Makele ambaye alikuwa mkuu wa Upelelezi Kituo cha Urafiki, ,Koplo Abeneth na mwanamke ambaye sikumtambua kwa sura.
Swali:Hao waliokuwepo kwenye hiyo Saloon nyeupe walishuka kwenye gari?
Jibu:Ndiyo maana niliwatambua, walishuka kwenye gari.
Swali:Hiyo saloon ya daki blue ilikuwa ikiendeshwa na askari?
Jibu:Ndiyo.
Swali:Wale watu wanne walikuwa kwenye Pick Up ya polisi walishushwa kwenye gari?
Jibu:Hapana.
Swali:Ulipata kufahamu wale walikuwa wanakosa gani?
Jibu:Nilipata taarifa kuwa walikuwa wamekamatwa kwenye tukio la ujambazi na walikamatwa wakiwa na bastora na briefcase ye yenye milioni tano.
Swali:Baada ya maelezio hayo nini kiliendelea?
Jibu:Bageni alienda tena pempeni kuzungumza na simu na wakati huo mimi na Frank tulienda pembeni kidogo tulipokuwa tumeegesha gari ili tusubiri afande amalize kuongea na simu.
Swali:Wale watu wa BIDCO mliwashirikisha kuwatambua wale watu wanne?
Jibu:Bageni aliwashirikisha na dereva wa BIDCO aliwatambua na kusema wale ndiyo waliowafanyia uhalifu.
Swali:Baada ya Bageni kumaliza kuzungumza na simu alitoa maagizo gani?
Jibu:Niliona Defenda ya Osytebay imekuja pale na tayari giza lilikuwa limeishaingia kidogo na waliokuwa kwenye hiyo hiyo gari ni mshitakiwa Abeneth, Koplo John na Koplo Abubakar na gari hilo lilikuwa na namba za usajili TZR 6559.
Swali:Nini kilifuata?
Jibu:Bageni aliamuru wale watu wanne washushwe kenye Pick Up waingizwe hilo kwenye Defenda.
Swali:Hiyo amri ilitekelezwa?
Jibu:Ilitekelezwa wale watu wakaingizwa kwenye hilo gari na baadhi ya askari wa Chuo Kikuu wakapanda kwenye hiyo gari.
Swali:Baada ya watu wale kuamishiwa humo kulitolewa maelekezo gani tena?
Jibu:Dereva wa Chuo Kikuu PC Noel aliambiwa aende kituo cha Urafiki na yule dereva wa defenda aliingia kwenye gari na kuelekea njia ya ubungo.
Swali:Nyie mlielekea wapi?
Jibu:Bageni alikuwa akiongea na simu kwa mara ya tatu pale na baada ya bapo alituambia tusukume gari lililotuleta pale ,tukalisukuma likawaka tukaingia kwenye gari na akamtaka dereva tuelekea Ubungo na kweli tulielekea huko.
Swali:Wakati mkielekea Ubungo yale magari mengine yaliyotangulia kuondoka mlikuwa mkiyaona?
Jibu:Hapana kwani yaliondoka dakika kumi zilikuwa zimeishapita.
Swali:Mlipofika ubungo mataa mlielekea wapi?
Jibu:Dereva aliambiwa aelekee Kimara tukaingia kwenye kisima kimoja cha mafuta afande Bageni akatoa fedha mfukoni akalipa tukawekewa mafuta, tukaendelea na safari hadi Kituo cha polisi Mbezi Lous.
Swali:Mlipofika katika kituo hicho cha polis?
Jibu:Dereva wetu aligeuza gari akaliangaliza usawa wa kurudi mjini, Bageni akaingia ndani ya kituo kile, mimi na Lema tukabaki kwenye gari.
Swali:Alivyorudi ikawaje?
Jibu:Alirudi na askari mmoja aliyekuwa amevalia sare ya Jeshi la Polisi, ambaye alimpata pale kituoni na kisha askari huyo alipanda kwenye lile gari letu.
Swali:Yale mageri manne mliyokuwa nayo pale Samnujoma mlipofika hapo Mbezi Louis, uliyaona?
Jibu:Siku yaona.
Swali:Baada ya Bageni kurudi kwenye gari mlielekea wapi?
Jibu:Akamwamuru dereva tuelekee mbele kama tunaenda Morogoro, yaani kule msituni tulipoendaga na mahakama mwaka jana na na kabla hatujafika katika msitu huo kuna kituo cha mabasi.
Swali:Hukumuuliza Bageni mnakwenda wapi?
Jibu:Nashukuru mungu niliuliza dereva akaniambia tunaenda Mbezi Makabe, nikamuuliza swali la pili tunaenda kukamata, dereva akanijibu hajui, nikanyamaza kimya.
Swali:Unasema Bageni alionhea na simu , je alirudi kwenye gari?
Jibu:Hakurudi ila sekunde chache niliona defenda ng’ambo ya pili ya barabara ikiwa imepaki na sikuelewa ilikuwa imetokea kituo gani wala namba zake.
Swali:Baada ya Defenda hiyo kuja nini kiliendelea?
Jibu:Bageni alimuuliza yuke askari aliyevalia sare tunaelekea wapi,akamjibu mbele kule tulikokwendaga na mahakama siku hili na defenda ikawa inatufuata.
Swali:Uliweza kumuuliza Bageni mnakwenda wapi?
Jibu:Ni kosa kubwa kumuuliza afande ,aswali, tuliendelea na safari hadi tukamaliza nyumba zote zilizokuwa zinaonekana kisha tukaingia porini.
Swali:Mlivyonigia porini mlifanya nini?
Jibu:Yule askari aliyevaa sare alimwambia Bageni eneo lenyewe ndilo hili ila lina Chui sana.
Swali:Baada ya askari huyo kusema maneno hayo mlifanya nini?
Jibu:Tulienda mbele kidogo na gari letu na dereva akasimamisha gari.
Swali:Ilikuwa muda wa saa ngapi?
Jibu:Sikumbuki ila giza tayari lilikuwa limeishaingia.
Swali:Baada ya dereva wenu Frank kusimamisha gari nini kilifuata hapo msituni?
Jibu:Aligeuza gari na lile defender likageuzwa baada ya hapo Bageni,Lema na Saad walishuka kwenye gari.
Swali:Wewe je?
Jibu:Mimi na dereva na yule askari tuliyemchukua Mbezi hatukushuka kwenye gari.
Swali:Wakati wameshuka ile redia call ilikuwa wapi?
Jibu:Nilibaki nayo mimi nikaifungua nikasikia tukio la ujambazi la Kijitonyama.
Swali:Kule porini wakati Bageni , Saad na marehemu Lema walivyoteremka walisema wanaenda kufanya nini?
Jibu:Hawakusema.
Swali:Kutoka Pajero yenu ilipokuwa imesimama na ile defenda ni umbali gani kwa kukadilia?
Jibu:Kama mita 15-20.
Swali:Ulivyokuwa kule msituni hukuweza kutambua ni watu gani waliokuwa wamepakizwa kwenye ile defenda?
Jibu:Sikuweza kutambua.
Swali:Wakati unasikiliza redio call kule porini ulisikia nini?
Jibu:Nilisikia mlio wa bunduki ambapo mlio huo ulisika eneo lililokuwepo ile defenda na baada ya kusikia hivyo nilishuka kwenye gari nikajue kulikoni, ndipo nilikuta mtu mtu mmoja anashuka kwenye ile defenda na Saad akamtwangwa risasi na pia chini nikaona tayari kuna watu watatu wameishapigwa risasi.Hivyo yule nileyemuona akipigwa risasi ndiye alikuwa akimaliziwa.
Swali:Ulipita muda gani wewe kusikia mlio huo?
Jibu:Dakika moja haijapita.
Swali:Baada ya zoezi hilo la kupigwa risasi wale watu kukamilika nini kiliendelea?
Jibu:Miili ya watu wale ilipandishwa kwenye defenda na nilishuhudia kwa macho yangu ikipakizwa,mimi, Bageni ,Lema na Saad turiduni kwenye Pajero letu na yule askari aliyevalia sare alionekana kuchanganyikiwa na kile kitendo , tukamshusha njiani badala ya Kituo cha polisi Mbezi Lous.
Swali:Baada ya kumshusha mliekea wapi?
Jibu:Urafiki polisi, Bageni akaingia kituoni pale na sisi tulibaki kwenye gari na tulikaa kwa muda mrefu na alirudi akatuambia tuondoke turudi ofisini Oystebay, tukamshusha na sisi askari wa dogo tukaendelea na doria.
Swali: Miili ya marehemu ilipelekwa wapi?
Jibu:Bageni alimuru ipelekwe Muhimbili na kweli ilipelekwa.
Swali:Siku ya pili yake yaani Januari 15, 2006, mlifanya nini?
Jibu:Mimi na Rashid tulirudisha zile silaha ofisini na Saad akafungua jarada.
Swali:Shahidi 30,31 na 36 walisema kuwa tukio la kupigwa risasi Bunju, wewe unalifahamu?
Jibu:Ni kweli nalifahamu, tarehe sikumbuki ya tukio hilo ila tulilifanyabaada ya Januari 16.
Swali:Nani alienda kupiga risasi bunju?
Jibu:Siku hiyo nilifika ofisini na kukuta Lema na Saad wameishaingia kwenye gari , nikaambiwa niongozane nao nikafyatue risasi kwani afande Bageni anataka maganda haraka sana.
Swali:Baada ya kupokea hayo maelekezo mlikwenda Bunju?
Jibu: Tulielekea huko na kabla ya kuondoka nilishauri kwamba ni kwanini tusiende pale FFU Ukonda kwenye uwanja wa Range , ila nikalazimishwa zoezi la kutafuta maganda hayo likafanyike bunju.Kweli tulikwenda bunju tukapiga risasi tukarudi na maganda na nikamkabidhi yale maganda Bageni, akaniambia asante sana.
Swali:Ulivyokuwa msituni ukona maganda na na mkiwa njiani kutoka bunju hukuuliza maganda hayo ni kwanini yanatakiwa?
Jibu:Sikufahamu ni kwanini yanatakiwa na wala sikuona maganda kule msituni.
Swali:Unaikumba Tume ya Jaji Mussa Kipenka?
Jibu:Ndiyo kwani nilienda kuhojiwa na leo nasema ukweli maelezo niliyotoa kwenye tume hiyo ni tofauti kabisa naniliyotoa polisi kwani maelezo niliyotoa kwa Tume ya Kipenka tulipewa maelekezo tutoe maelezo ya uongo.
Swali:Nani aliwapa maelezo ya nini mkaongee kwenye tume hiyo?
Jibu:Zombe na maelekezo hayo ni kwamba tunakaseme kuwa mauji yalitokea Sinza ukuta wa posta na siyo msituni na binafsi sifahamu kama siku hiyo kulitokea tukio la ujambazi eneo la sinza ukuta wa posta.
Swali:Je kulikuwa na sababu yoyote ya nyie kutakiwa mtoe maelezo ya uongo kwenye Tume hiyo?
Jibu:Tuliambiwa maelezo yale ya uongo ndiyo msimamo wa jeshi la polisi hivyo atakaye saliti maelezo yale msalaba wote atabebeshwa yeye.

Swali:Siku Bageni anatoa ushahidi wake Februali mwaka huu, alidai kuwa alifahamu tukio hilo kupitia redia call na kwamba, wewe unasemaje katika hilo?
Jibu:Mtukufu Jaji, afande bageni ni muongo sana kwani yeye ndiye aliyetupeleka mimi na wenzake kule msituni mauji yalipofanyika.
Swali:Kumbuka kama uliwahi kumweleza Bageni kwamba mapambano ya risasi na marehemu hao yalitokea Sinza ukuta wa Posta?
Jibu:Nasema hivi sijui na wala sijawahi kumweleza hilo.
Jaji Massati aliairisha kesi hiyo hadi leo ambapo mshitakiwa wa 13, Festus Gwasabi ataanza kutoa ushahidi wake.
Mbali ya Zombe na Lema, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka wilayani Ulanga, Morogoro, na dereva teksi mmoja, ni pamoja na SP Christopher Bageni, SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasabi..

Zombe na wenzake,wanadaiwa kufanya mauaji hayo Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, ambapo waliwaua, Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,April 29,2009

1 comment:

Anonymous said...

Do you have any video of that? I'd care to find out more details.

Feel free to visit my web-site - cheap earphones in bulk

Powered by Blogger.