Header Ads

JWTZ LITALETA AMANI DARFUR?


Na Happiness Katabazi

MACHI 31 mwaka huu, msuluhishi mgogoro wa Jimbo la Darfur, Sudan, Dk. Salim Ahmed Salim, alikuwa kwenye kambi ya mafunzo ya ulinzi wa Amani, Msata, wilayani Bagamoyo, Pwani. Alikuwa akiwafunda wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanazania (JWTZ) wanaotarajiwa kwenda Darfur.


Kufika kwa Dk. Salim, siku hiyo na kuwafunda wanajeshi hao kambini hapo, kulitokana na mwaliko alioupata kutoka uongozi wa JWTZ uliosema wamefikia uamuzi wa kumwalika ili awafunde wanajeshi hao kwakuwa yeye ni anaufahamu kwa kina mgogoro wa Darfur.

Nilikuwa mwandishi mwanamke pekee niliyeambata na waandishi wa habari wanaume kutoka vyombo mbalimbali vya habari na wale JWTZ katika hafla ya kuwaaga wajeshi hao iliyofanyika Msata. Tulipofika kwenye kambi hiyo ambayo ipo umbali mrefu kutoka barabara kuu, tulikuta wanajeshi wote waliokuwa wakiagwa siku hiyo.

Walivalia kombati, safari buti za JWTZ, huku mikono yao ya kulia wakiwa wamevalia vitambaa na kichwani wakiwa wamevaa kofia za chuma kwa ajili ya kuzuia risasi, vitu vyote hivyo vilikuwa na nembo ya UN. Hivyo, mavazi yaliwafanya waonekane ni tofauti na watu wengine waliofika kambini hapo.

Wajeshi hao wameonekana kuiva kimafunzo na wapo tayari kwenda kupepesha bendera ya Tanzania, Darfur kutokana na furaha waliyo nayo. Baadhi yao waliniuma sikio na kusema ujio ule pale kambini umechangamsha kambi ile kwani muda mwingi uishi peke yao na makamanda.

Akizungumza na wanajeshi 875 kwenye uwanja wa mazoezi unaotumiwa na wanajeshi hao ambao wameishapata mafunzo mahsusi kwa ajili ya kwenda kulinda amani Darfur, Dk. Salim amewataka maofisa na askari wa Jeshi hilo, wanaokwenda kulinda amani katika jimbo hilo, watimize majukumu yao bila ubaguzi.

“Wanajeshi mkiwa Darfur nawaombeni sana mkafanikishe jukumu la ulinzi wa amani na kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wananchi walioathirika na vita, naamini mkizingatia haya ninayowaeleza pamoja na mafunzo mliyoyapata, mtafanikiwa. Darfur si sehemu zote zina machafuko, hivyo jukumu lenu si kwenda kupigana tu bali pia kulinda amani.

‘‘Na ninataka mtambue kule mnakokwenda kuna magenge mbalimbali ya kiharifu, hivyo nasisitiza mzingatie mafunzo mliyoyapata,” anasema Dk. Salim.

Amewataka wakiwa Darfur cha kwanza wazingatie usalama wao vile vile watimize jukumu la ulinzi wa amani kwa kufikisha misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa vita washirikiane na wananchi wakule bila kuwagawa kwenye makundi.

Kwa upande wao, maofisa na wanajeshi hao waliosilikiza kwa makini, walimuakikishia Dk. Salim na Luteni Jenerali Shimbo, kutimiza majukumu yaliyowapeleka Darfur, na si vinginevyo.

Licha ya kuzungumza na wanajeshi hao, pia Dk. Salim alipata fursa ya kujibu maswali mbalimbali aliyoulizwa na waandishi wa habari katika kambi hiyo inayotumika kwaajili ya kutoa mafunzo kwa walinzi wa amani(peace keeping).

Alipoulizwa yeye binafsi kwamba kutolewa kwa hati ya kukamatwa na kufikishwa katika mahakama ya kimataifa ya The Hegue iliyopo Ufaransa kwa Rais wa Sudan, Hassan al-Bashir, kunaweza kuathiri kazi inayofanywa na vikosi vya walinzi walinzi wa amani, Dk. Salim alisema kushitakiwa kwake kutaathiri kwa kiasi fulani kwa mchakato wa amani ila hakuwezi kuathiri zoezi la upelekwaji wa vikosi walinzi wa amani.

“Hivyo msimamo wa Afrika tunasema amri hiyo ya kukamatwa kwa Bashir, kwa bahati mbaya imekuja muda mbaya kwani kutaathiri mchakato mzima wa amani jimboni Darfur,” anasema Dk. Salim ambaye amewahikushika nyadhifa za juu katika Serikalini.

Akijibu swali la mwandishi mmoja aliyetaka kufahamu kama serikali ya Sudan iliomba msaada wa JWTZ; anasema hakuna jeshi lolote duniani linaweza kwenda Sudan bila Sudan kuiruhusu. JWTZ imeruhusiwa hivyo lina kwenda kwa jukumu la ulinzi wa amani na sikupigana na makundi ya watu yanayopinga serikali ya Sudan.

Akijibu swali la ni kwa nini vita inaendelea Darfur na Umoja wa Mataifa (UN) umechelewa kupeleka vikosi; Dk. Salim alisema watu waelewe kuwa vita ya wenyewe kwa wenyewe inachukua muda mrefu na historia inaonyesha kuwa inadumu kwa muda mrefu lakini, anasema uchelewaji huo umetokana na uzembe wa jumuiya hiyo ya kimataifa.

“Kimsingi vikosi vilipaswa vipelekwe tangu Januari 2008 lakini hadi Machi mwaka huu, havijapelekwa...natambua kuwa vinaitajika vifaa vya kupelekwa huko. Na hilo ni uzembe kwa Jumuiya ya Umoja wa Mataifa kwwani wanachosema si wanachotenda,” anasema na kufanya wanajeshi waliomzunguka kutabasamu.

Alipoulizwa ni kwa nini Tanzania inapeleka wanajeshi Sudan wakati baadhi ya nchi za Maziwa Makuu zina vita na hatupeleki wa wanajeshi, Dk. Salim anajibu:

“JWTZ imeombwa kupeleka wanajeshi na kwamba Darfur kuna vita, kuteteleka kwa Sudan kutaathiri nchi tisa zinazopakana na nchi hiyo.
Huwezi kuachia watu wafe, wateseke Darfur na hasa ukizingatia Tanzania ina historia yake katika uamuzi wake wakupeleka wanajeshi wake katika nchi zenye vita na wakifika nchi husika utimiza majukumu ipasavyo na kufanikiwa kurejesha amani katika nchi nyingi ambazo amani iliteteleka.”

Naye Mnadhimu Mkuu wa Jeshi hilo, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, anasema wanajeshi wanao kwenda Darfur ni 875 kati yao wanawake 20 miongoni mwao ni Ofisa mwenye cheo cha kaptaini, Celina Rafael na 75 ni waandisi wa medani.

Luteni Jenerali Shimbo anasema kikosi hicho kinaongozwa na Luteni Kanali Alli Mzee Katinde. Na wakiwa Darfur, wataishi kwenye maeneo mawili ya Muhajaria na Khor Abeche na kuongeza kuwa wanajeshi wote wapowana afya njema.

Shimbo anasema wanajeshi hao wamepata mafunzo ya ulinzi wa amani kwa miaka miwili kambi hapo na kutaja moja aina moja ya mafunzo waliyoyapata kuwa ni ‘mafunzo ya kina’.

“Hivi sasa vijana wetu tayari na tunategemea vifaa vianze kuondoka nchini kwenda Darfur, April, mwaka huu, kisha kundi la waandisi wa medani 75 litafuata kwa ajili ya kwenda kujenga makazi katika maeneo watakayofikia wanajeshi wetu kisha kundi jingine litafuata,” anasema Shimbo kwakujiamini.

Anasema JWTZ ulifikia uamuzi wa kumwalika Dk. Salim kwaajili ya kuwafunda wanajeshi hao kwasababu anaufahamu vyema mgogoro wa Sudan.

Anamalizia kwa kuwaasa wanajeshi wazidishe nidhamu wakifika Darfur, kwani endapo wataenda kufanya kinyume na majukumu yaliyowapeleka huko watakuwa wanalipaka matope jeshi hilo na taifa kwa ujumla.

Mungu Ibariki Tanzania Mungu Ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, April 9 mwaka 2009

1 comment:

Peter Joseph said...

DEAR HAPPINESS K.,
WABONAKI WAITU. KWANZA NASIFU SANA
KWA UJASIRI ULIO NAO. NIMEKUWA NASOMA MAKALA ZAKO, ZINATIA MOYO SANA; UKIZINGATIA KUWA KUNA VITISHO
VINGI AFRICA KWA WAANDISHI. MAKALA YAKO KUH. MZEE DITTO ILIKUWA NZURI.
NDIO ILIKUWA YA KWANZA KUSOMA, NA PIA KUKUFAHAMU. KEEP IT UP, KARIBU
SANA USA. LETS KEEP IN TOUCH, BYE.
MAY GOD BLESS YOU AND ALL YOUR FAMILY OVER THERE,AMEN.

Peter@stl-mo.usa.

NB-My email is::
pjoseph20002000@yahoo.com

Powered by Blogger.