Header Ads

MAHAKAMA YAMNG"ANG"ANIA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imekataa kufuta kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Miradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Walirwande Lema, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutolea uamuzi wa ama kuifuta au la.

Uamuzi huo ulitokana na ombi la wakili wa Liyumba, Majura Magafu ambaye Machi 2, mwaka huu, aliwasilisha mahakamani hapo ombi la kutaka mahakama hiyo itumie kifungu cha 225(1-4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai 2002, kinachotamka kuwa, ndani ya siku 60, upelelezi kesi husika uwe umekamilika, vinginevyo ifutwe.

Lema alisema baada ya kupitia hoja za mawakili wa pande zote mbili, amebaini kuwa licha ya siku 60 kupita na upalelezi wa kesi hiyo kutokamilika, haoni kama haki za msingi za washitakiwa zimevunjwa.

“Kwa sababu hiyo, natupilia mbali ombi la wakili wa utetezi la kutaka niifute kesi hii na ninatoa amri ya kuuongezea muda upande wa mashitaka ili waweze kukamilisha ushahidi, na tayari ulishaleta ombi la kuongezewa muda,” alisema Lema na kuahirisha kesi hiyo kwa nusu saa.

Mbali ya kusikiliza ombi hilo na kulitupilia mbali, mahakama hiyo pia ilisikiliza ombi lingine la upande wa utetezi la kutaka washitakiwa waachiliwe huru kwa madai kuwa hati ya mashitaka ina kasoro.

Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface ambaye alikuwa akisaidiana na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Frederick Manyanda na Wabuhanga, Beni Likoni, Prosper Mwangamila na Tabu Mzee, alidai kuwa waombaji walileta ombi lao la kutaka mahakama hiyo itupilie mbali hati ya mashitaka pamoja na kibali cha DPP cha kufungua kesi hiyo kwa madai kuwa ina dosari za kisheria.

Aliendelea kudai kuwa, kifungu cha 135 walichokitumia mawakili wa utetezi, kingeweza kutumika endapo tu wangeainisha ni kifungu gani kidogo ndani ya kifungu sentensi katika kifungu hicho, lakini wao wametumia kifungu hicho kavu.

“Kutumia kifungu kisichohusika na kutochagua kifungu kwa ukamilifu, kisheria hakuna suluhu, hivyo upande wa mashitaka unaiomba mahakama hii itambue kuwa ombi la utetezi ni mfu na yanatakiwa yatupiliwe mbali haraka iwezekanavyo kwa sababu wametumia vifungu visivyo sahihi,” alidai Boniface.

Aidha, Wakili Magafu aliyekuwa akisaidiana na Profesa Gamalieli Mgongo Fimbo, Hurbet Nyange na Hudson Ndyusepo, aliinuka na kuanza kujibu hoja hizo na kudai kuwa pingamizi la Boniface halina msingi na lina lengo la kuchelewesha kesi hiyo na kwamba amezitoa ili kupima upepo wa mahakama unavyovuma.

Magafu alidai kuwa, nao upande wa mashitaka umeshindwa kuonyesha ni kifungu gani wameshindwa kukitumia kuwasilisha maombi yao na kuongeza nao upande wa mashitaka umeonyesha haujui kifungu hicho na kusisitiza kuwa, maombi hayo yameletwa kwa njia sahihi na kuiomba mahakama itupilie mbali pingamizi la upande wa mashitaka.

Baada ya kusikiliza malumbano hayo makali ya kisheria, yaliyodumu kwa saa moja na nusu, Lema aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 31, ambapo itakuja kwa ajili ya kutolea uamuzi maombi hayo.

Machi 30, mwaka huu, Lema alianza kuendesha kesi hii baada ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo ambaye ndiye alikuwa nayo tangu ilipofunguliwa Januari 27, mwaka huu,
kujiondoa baada ya jamii kupitia vyombo vya habari kulalamikia dhamana ya Liyumba.

Februari 17, mwaka huu, hakimu Msongo alimwachia kwa dhamana iliyozua utata Liyumba.

Moja ya masharti ambayo hayakutimizwa na Liyumba, ni kuwasilisha mahakamani hati zenye thamani ya sh bilioni 55, wadhamini wawili wa serikali wakiwa na barua kutoka kwa waajiri wao na kukabidhi hati za kusafiria mahakamani hapo.

Lakini siku hiyo, Liyumba aliwasilisha hati yenye thamani ya sh milioni 882, hati ya kusafiria ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, huku wadhamini wawili wakiwa hawana barua zilizosainiwa na mwajiri wao kama masharti yalivyotolewa na mahakama.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, April 24, 2009

No comments:

Powered by Blogger.