Header Ads

WASHTAKIWA KESI YA NBC UBUNGO WANA KESI YA KUJIBU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imesema washtakiwa 11 wanaokabiliwa na kesi ya wizi wa kutumia silaha na kupora sh milioni 1.6 mali ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Tawi la Ubungo, wana kesi ya kujibu.

Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Pelagia Khaday, alisema hayo jana wakati akitoa uamuzi wake baada ya pande zote mbili katika kesi hiyo kuwasilisha hoja za washtakiwa iwapo wana kesi ya kujibu au la.

Khaday alisema licha ya ushahidi katika kesi hiyo kutolewa kwa vipande vipande, mahakama hiyo imeona ni vema ikawapatia nafasi washtakiwa hao kujitetea.

“Kwani baadhi ya mashahidi waliwatambua baadhi ya washtakiwa katika gwaride la utambulisho kwamba siku ya tukio walikuwepo na baadhi ya vielelezo vimeonyesha kuwa vinawahusu washtakiwa hivyo nimeona ni vema washtakiwa nao wakapewa nafasi ya kujitetea,” alisema Hakimu Khaday.

Wakati akisema hayo ghafla ndege wawili walifika kwenye jarada la kesi hiyo alilokuwa akilisoma na kufanya hakimu huyo kutaharuki hali iliyosababisha wananchi waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo kushtuka lakini hakimu huyo alisema yupo salama na kwamba hilo ni jambo la kawaida.

Kutokana na uamuzi huo, alisema washtakiwa hao wataanza kujitetea Mei 21.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Februari 2, mwaka 2006 saa tatu asubuhi katika NBC tawi la Ubungo, waliiba sh milioni 168,577.84 mali ya benki hiyo.

Wakati huohuo, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Victoria Nongwa amemhukumu kifungo cha maisha jela, muosha magari wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Robert Daudi(29) baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka tisa.

Nongwa alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na pande zote ameridhika kuwa mshtakiwa huyo alifanya kitendo hicho.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo Wakili wa Serikali, Ntuli Mwakahesya, aliomba mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa, kwani vitendo vya namna hivyo vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku hali inayosababisha kuwaharibu kisaikolojia watoto waliotendewa vitendo hivyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, April 24, 2009

No comments:

Powered by Blogger.