Header Ads

SOKOINE, HIVI NDIVYO TUNAVYOKUENZI

Na Happiness Katabazi

MIAKA 25 iliyopita, Watanzania walifikwa na msiba mkubwa, kwa kumpoteza mmoja wa viongozi aliyeipigania nchi yake bila woga.

Kiongozi huyo si mwingine bali ni aliyekuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Edward Moringe Sokoine, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari jioni ya Aprili 12, 1984 katika eneo la Wami, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.

Sokoine alifariki dunia wakati nikiwa na umri wa miaka mitano, lakini nakumbuka nilikuwa nikilisikia jina lake kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kabla na baada ya kifo. Hakika, nyingi zilikuwa zimebeba ujumbe wa kumtukuza kutokana na mchango wake, nilimsikia Radio Tanzania na kumsoma kupitia vitabu mbalimbali.

Nikiri kuwa sikubahatika kumtia machoni kiongozi huyu, hadi Mwenyezi Mungu alipomtwaa. Ila nimetokea kuwa muumini mzuri tu wa mtindo wake alioutumia kutenda kazi katika ofisi za umma.

Kwa mujibu wa vitabu na watu waliowahi kufanya kazi naye, wanamuelezea kuwa ni kiongozi aliyejawa na uzalendo kwa nchi yake, hakupenda makuu, aliyewashughulikia wote waliohujumu uchumi wa taifa hili, hakuwa mwoga, alimkemea na kumchukulia hatua yeyote aliyekwenda kinyume na taratibu zilizowekwa.

Hakuwa mchumia tumbo kama walivyo viongozi wengi wetu wa sasa. Hakuingia madarakani kwa kubebwa na vyombo vya habari wala kupenda sifa na kuwagawa wanachama wa CCM kama ilivyo sasa. Alipenda umoja.

Lakini leo tukiwa tunakumbuka kifo chako Sokoine, mambo maovu ambayo wewe na Baba wa Taifa, Julius Nyerere, kila kukicha mliyapiga vita kwa vitendo, leo maovu hayo ndiyo yamekuwa kigezo cha kupata uongozi na kupata umaarufu ndani ya jamii.

Mlipinga rushwa kwa ngazi zote, lakini leo hii hospitalini, polisi, kwenye ajira na kwenye michakato ya uchaguzi, ziwe chaguzi za ndani ya chama chako, Chama Cha Mapinduzi (CCM), au chaguzi za kiserikali, ni rushwa tu ndiyo imetamalaki. Hutolewa na kupokewa kwa wazi.

Si kwenye sekta hizo tu, bali hata katika vyombo vya habari rushwa nayo imo kwani, wanahabari ni miongoni mwa wala rushwa wazuri tu.

Tunapewa na baadhi ya viongozi manyang’au ili tusiweze kuripoti machafu yao kwenye jamii. Manyang’au wamekuwa wakitupatia fedha tuwachafua mahasimu wao kisiasa, ili wao ndio waonekane wasafi mbele ya jamii.

Na kazi hiyo tukiishaikamilisha husherehekea na kutamba kuwa hakuna aliye msafi.

Sisi waandishi wa habari za mahakamani hasa pale, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baadhi yetu tunakuenzi kwa kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya washtakiwa wenye fedha, wenye umaarufu, na wenye asili ya Kiasia, wanaofikishwa hapo kwa makosa mbalimbali.

Lengo lao ni kutaka tusiripoti kesi zinazowakabili kwa sababu tukiwaandika kwenye vyombo vya habari, watadhalilika mbele ya jamii na shughuli zao za kitapeli zitakwama. Hivyo, tunaamua kuchukua fedha zao na kisha hatuandiki kesi zinazowakabili.

Hakika sisi ni majasiri kuliko mafisadi kwani, kila siku tunashinda mahakamani hapo na kuona watu mbalimbali wakihukumiwa kwenda jela lakini wala hatuogopi kuwa kupokea rushwa ni kosa la jinai, linaloweza kumpeleka mtu jela.

Hili hufanyika mara kwa mara pale Kisutu, mchana kweupe! Baadhi ya askari polisi wanalifumbia macho, kwani nao ni miongoni mwa wanaofaidika na vipato hivyo haramu vinavyotolewa ndani ya jengo la mahakama, chombo kinachopaswa kuwa kimbilio la haki za wananchi.

Hivyo ndivyo tunavyokuenzi kwenye suala la rushwa kwa sisi wanahabari, na mhimili huu wa nne (usio rasmi), sasa umeanza kuwa na nguvu.

Ulipigana kufa na kupona na wahujumu uchumi lakini leo hii, baadhi ya wafanyabiashara wachafu wamejipenyeza kwenye CCM yako.

Wanatoa misaada ya fedha chafu na serikali yetu inawapa nafuu ya kodi na kupitisha mizigo yao inayoingia nchini bila kukaguliwa na mamlaka husika, kwa sababu ya kile kinachoelezwa kuwa wafanyabiashara hao wana rekodi nzuri.

Nafuu hiyo haiwatoshi, wafanyabiashara wengine sasa wamejitumbukiza kwenye CCM na kugombea nyadhifa mbalimbali.

Dhamira yao si kukisaidia chama bali ni kukitumia chama kutimiza haja zao, mathalani kupata upendeleo katika zabuni za serikali na kinga ya kidiplomasia (Diplomatic Immunity), ili wanapopitisha mizigo yao haramu pale uwanja wa ndege wasikaguliwe wala kutiliwa shaka na wana usalama.

Ulisisitiza kwa vitendo maendeleo ya kilimo nchini, leo wakulima wetu hakuna anayewajali. Fedha nyingi hutengwa katika kugharamia shughuli za kisiasa.

Wanasiasa wanajilipa malupulupu makubwa na ndiyo maana hivi sasa Watanzania wengi, hata ambao hawana sifa za uongozi, wanakimbilia kuhonga fedha nyingi ili wapate uongozi.

Viongozi wetu wa leo wamegeuka kuwa manyapara, kazi yao ni kutoa amri bila kuonyesha njia.

Majukwaani wanasema kilimo ni uti wa mgongo, lakini hakuna kiongozi ambaye ameonyesha mfano kwa vitendo, hata kwa wananchi wanaomzunguka, kwamba na yeye hushika jembe na kulima.

Wamekuwa ni mahiri na wajanja wa kucheza na maneno na hotuba. Kabla ya kuzitoa, hutuma mashushushu wao sehemu husika, kupeleleza wananchi wa eneo hilo wanakabiliwa na tatizo gani kisha hurudi ofisini na kuandaa hotuba ya matumaini kuhusu kero hizo.

Kiongozi huyo anapotembelea eneo hilo huzungumzia kero au matatizo hayo na kuahidi kuyatafutia ufumbuzi. Kumbe ni danganya toto!

Kwa upande wa wafugaji, Serikali haijali masilahi yao bali inajali masilahi ya wawekezaji wakubwa.

Baadhi ya viongozi wanaotoka maeneo ya ufugaji hufurukuta kutetea haki za wafugaji, hata hivyo wanalifanya hilo huku wakijua kwamba serikali ya CCM haina sera nzuri ya ufugaji.

Hiki ni kiini macho kwa taifa kuwa na sera ya mifugo bila kuwa na sera ya kuendeleza wafugaji.

Hakuna kikundi cha Watanzania kilichodharaulika na kunyimwa haki za kibinadamu kama wafugaji.

Kwanza, walinyang’anywa ardhi yao ya kufugia na nyumba zao kuchomwa moto katika Wilaya ya Hanang’. Huko serikali ilianzisha mashamba makubwa ya kilimo cha ngano.

Wafugaji wale hawakupata fidia wala ardhi mbadala na sasa wamesambaa kila mahala nchini, Mvomero, Ihefu na kwingineko hali ni hiyo hiyo.

Kama vile hiyo haitoshi, mahakama za nchi hazikuwasaidia wafugaji hao walipo kwenda kudai haki zao mahakamani.

Hii inaonekana kwamba sera na sheria za nchi kwa ujumla wake, haziwalindi wafugaji.
Kule Mkomazi, wafugaji waliokuwa wakiongozwa na Lakei Faru Parutu, walifukuzwa ndani ya hifadhi bila kufidiwa fedha, au ardhi mbadala. Leo hii wanatangatanga bila kujua wapi walishie mifugo yao. Hivyo ndivyo tunavyokuenzi.

Kwa bahati mbaya uliaga dunia wakati nchi yetu haijaingia kwenye mfumo wa vyama vingi, mfumo wa vyama vingi ulianza rasmi 1992.

Sasa tuna zaidi ya vyama vya upinzani 15, lakini ni vyama vichache mno vinavyoonyesha kuwa na upinzani wa ukweli.

Ndani ya vyama hivyo kuna mamluki wa kisiasa, wachumia tumbo na walafi wa madaraka.
Pindi wanapokosa fursa hizo ndani ya vyama vyao, hurudi CCM au huanzisha vyama vyao binafsi. Sasa, siasa na uongozi imekuwa ni biashara.

Tanzania uliyoiacha mwaka 1984, si hii ya leo kwani, imepiga hatua za kimaendeleo katika sekta mbalimbali japo maendeleo hayo hayawiani na wakati tulionao. Wananchi wengi wanapata elimu za msingi katika shule nyingi za serikali, lakini elimu hiyo haina ubora wa kutosha.

Watanzania hivi sasa wameanza kujua haki zao na kuzidai, wameanza kuwa majasiri na kuwakosoa viongozi na serikali wazi wazi pindi inapofanya kinyume. Uhuru wa kutoa maoni hata katika Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete unazidi kuongezeka.

Hata hivyo, baadhi yetu tumekuwa tukiutumia uhuru huo vibaya, kwa kuwapaka matope wenzao na kutundika picha za utupu kwenye mitandao, vitendo vinavyochochea mmomonyoko wa maadili kwa kizazi hiki na kijacho.

Tunapoadhimisha miaka 25 ya kifo cha Sokoine, viongozi wetu na wananchi kwa ujumla tujitazame upya. Maadili yetu je, ni sawa na ya viongozi wa awamu ya kwanza ya kina Nyerere, Sokoine, Karume na wengine?

Sokoine, hivi ndivyo tunavyokuenzi kinafiki. Machafu uliyoyapiga vita, leo tunayakumbatia. Serikali, chama chako, na vyuo vikuu havijishughulishi kuandaa hata mijadala ya kukumbuka mchango wako.

Tunashuhudia serikali ikilipia matangazo ya sherehe za muungano kwa takriban wiki tatu sasa, miaka kadhaa ya Kikwete tangu aingie madarakani, maadhimisho mbalimbali lakini haijadiriki kutoa matangazo ya kuonyesha kuwa Aprili 12 mwaka huu, taifa linakumbuka kifo chako.

Hukuwa fisadi, ulikuwa mchapakazi na mpenda haki, hivi unafikiri nani atakukumbuka?
Pengo kati ya tajiri na maskini limeongezeka, hivi matajiri waliotajirika na kuneemeka baada ya enzi ya uongozi wako wewe na Mwalimu, watakukumbuka?

Tuache unafiki wa kuzungumza kuwa tunamuenzi Sokoine mdomoni wakati kivitendo hatumuenzi. Tutakuwa tunachuma dhambi bure, mwisho wa siku tuje kuwa kuni kwenye moto wa milele. Mungu aipumzishe roho yako mahala pema peponi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, April 15, 2009

No comments:

Powered by Blogger.