Header Ads

KESI YA TANESCO DHIDI YA DOWANS YAKWAMA

Na Hapiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara Dar es Salaam, jana ilishindwa kuanza kusikiliza kesi ya kutaka mitambo ya Kampuni ya Dowans Tanzania Ltd, isiuzwe, iliyofunguliwa na Shirika la Umeme (TANESCO) dhidi ya Dowans, kwa sababu ya kukosekana jaji wa kuisikiliza.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, Katarina Revocati, alisema kesi hiyo ambayo jana ilikuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa haitaweza kusikilizwa kwa sababu aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Catherine Oriyo amehamishwa katika mahakama hiyo hivi karibuni, baada ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Revocati alisema kwa sababu hiyo, uongozi wa Mahakama nchini utampanga jaji mwingine ambaye atasikiliza kesi hiyo na hivyo kuiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 24, mwaka huu.

“Kesi hii ambayo leo (jana) ilikuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa, haitaweza kusikilizwa, kwa sababu Jaji Mfawidhi, Orriyo, ambaye ndiye alikuwa akisikiliza kesi hii hivi karibuni ameteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, kwa sababu hiyo naahirisha kesi hii hadi tarehe hiyo,” alisema Naibu Msajili Revocati.

Katika kesi hiyo namba 19/2008, mlalamikaji ni Tanesco, inayotetewa na kampuni ya uwakili ya Rex Attoneys, dhidi ya Dowans Tanzania Ltd, ambayo inatetewa na Kampuni ya uwakili ya Amicus Attorneys.

Kwa mujibu wa hati ya madai, TANESCO inaiomba mahakama kutoa amri ya kuizuia Dowans asiuze mitambo yake hadi kesi ya msingi iliyopo mahakamani hapo itakapomalizika na endapo mahakama haitakubali kutoa amri hiyo, iamuru Dowans kuweka mahakamani asilimia kumi ya dola za Marekani 109,857,686.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima,April 18, 2009

No comments:

Powered by Blogger.