Header Ads

WAKILI WA WATUHUMIWA EPA ABANWA

Na Happiness Katabazi

WAKILI maarufu wa kujitegemea, Majura Magafu, ambaye anawatetea baadhi ya watuhumiwa wa kesi za wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT) na ile ya matumizi mabaya ya ofisi za umma, jana alijikuta akipatwa na wakati mgumu, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kumbana kwa maswali.

Majura alijikuta kwenye hali hiyo, baada ya sekunde chache kuwasilisha ombi lake mbele ya jopo la mahakimu wakazi, lililokuwa likiongozwa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Addy Lyamuya, kuiomba mahakakama hiyo kumruhusu leo aweze kuendelea na kesi ya mauaji, iliyotokea Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Wakili huyo leo atakuwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kuendesha kesi ya mauaji ya Ubungo mataa, ambapo ameteuliwa na mahakama hiyo ya juu kuwatetea baadhi ya washtakiwa.

Katika kesi hiyo, inayohusisha wizi wa sh milioni 207, inayowakabili Kada wa CCM, Rajabu Maranda na Imani Mwakosya, Ester Komu na Bosco Kimela, ambao wote ni maofisa wa BoT, jana shahidi wa tisa aliendelea kutoa ushahidi wake.

“Unaomba kesi hii iahirishwe kwa sababu unakwenda kwenye kesi ya mauaji Mahakama Kuu, hivi hapo ofisini kwako hakuna mawakili wengine ambao wanaweza kuja kuendelea na kesi za wateja wako zilizopo katika mahakama hii, hivi huoni kwenda kwako Mahakama Kuu mara kwa mara kunasababisha wateja wako kuchelewa kujua hatima zao kwenye kesi zinazowakabili katika mahakama hii?” Hakimu Lyamuya alimhoji Magafu.

Yafuatayo ni maswali kati ya Lyamuya na Magafu:

Lyamuya: Umeomba kesi hii iahirishwe kwa sababu wewe kuanzia kesho (leo) utakuwa Mahakama Kuu kwa kipindi cha mwezi mmoja, kutetea watuhumiwa wa kesi ya mauaji, je, ni kwanini ofisi yako isimtume wakili mwingine aje aendeshe kesi hii badala yako?
Magafu: Wakili aliyepo ni mgonjwa wa kisukari, hawezi kuja kusimama hapa mahakamani.

Lyamuya: Hapa mahakamani si lazima wakili asimame, je, hakuna wakili zaidi ya huyo mgonjwa?

Magafu: Yupo Maregesi, ila kwa mazingira ya kesi hizi za EPA hawezi kuja kuendesha kesi hizi, kwa sababu kwa namna moja ama nyingine naye anahusishwa kwenye tuhuma hizi za wizi wa EPA.

Lyamuya: Zaidi ya Maregesi, hakuna tena wakili mwingine katika ofisi yenu?
Magafu: Mwingine ni wakili Makubi, ila kwa sasa anauguliwa na mzazi wake na amekwenda likizo na sina uhakika ni lini atakuja ofisini.

Lyamuya: Hiyo summons ya wewe kuitwa kwenye hiyo kesi ya mauaji Mahakama Kuu, uliipata lini?

Magafu: Niliipata wiki mbili zilizopita.

Lyamuya: Ulivyoipata hiyo summons, kwanini hukutoa udhuru Mahakama Kuu kwamba una kesi zaidi ya tatu unazozitetea hapa Kisutu na zote zimeishaanza kusikilizwa?

Magafu: Sikufahamu kikao cha mauaji kingepangwa kwa muda mrefu wa mwezi mmoja, hivyo naomba mahakama hii iniruhusu nikaudhurie kwenye kikao cha Mahakama Kuu.

Lyamuya: Magafu unafahamu kwamba kesho (leo) katika mahakama hii kwenye kesi nyingine ya EPA, mbali na hii iliyopo mbele yetu sasa inayomkabili Maranda ambaye ni mteja wako, inakuja kwa ajili ya upande wako kuwasilisha hoja kuwa wateja wako wana kesi ya kujibu au la?

Magafu: Sijui. Ninavyofahamu, kesi hiyo inakuja kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya upande wangu kuwasilisha hoja ya kwamba wateja wangu wana kesi ya kujibu au la.

Lyamuya: Ndiyo nakwambia sasa kwa mujibu wa rekodi za mahakama zinaonyesha kesho (leo) kesi nyingine ya EPA inayomkabili mteja wako Maranda na wenzake inakuja kwa ajili ya kuwasilisha hoja kuwa kuna kesi ya kujibu.

Lyamuya: Wewe unatetea kesi nyingi za EPA, huoni kwenda kwako Mahakama Kuu, kutasababisha wateja wako kuchelewa kupata haki zao katika kesi zinazowakabili?

Magafu: Off recod, kama ni hivyo waheshimiwa naomba niwasiliane na wakili mwenzangu ambaye anauguliwa na mzazi wake aje aendelee na kesi moja ya EPA ambayo nilikuwa naiendesha mimi na mimi pia nitawasiliana na Mahakama Kuu ili iweze kuniondoa kwenye orodha ya mawakili watakaowatetea washtakiwa wa kesi ya mauaji ya Ubungo, ili niweze kuendelea na kesi za EPA.

Kitusi: Hakuna cha off record hapa kila kitu kinarekodiwa, unataka tuandike nini kwenye rekodi ya mahakama?

Magafu: Naomba irekodiwe kwamba nitawalisiliana na wakili mwezangu ambaye anauguliwa na mzazi wake ili aje kuendesha kesi moja, pia nitawasiliana na Mahakama Kuu ili iweze kuniondoa kwenye orodha ya mawakili wa kuwatetea watuhumiwa wa kesi ya mauaji iliyopo Mahakama Kuu.

Awali Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda aliyekuwa akisaidiana na Vitalis Timon aliwasilisha ombi la kutaka kesi hiyo iahirishwe kwa sababu wanataka kumuongeza mshitakiwa mwingine kwenye kesi hiyo na kwamba endapo mshitakiwa huyo angekuwa kwenye eneo la mahakama jana, wangemuunganisha.

Aidha, Manyanda aliieleza mahakama kwamba, kwakuwa kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa, upande wa mashtaka ulikuwa umemleta shahidi wao aitwaye Emmanuel Boaz, ambaye jopo hilo lilimtaka aingie mahakamani na akashindwa kutoa ushahidi wake, baada ya kutokea mabishano na maombi ya kuombwa kuahirishwa kwa shauri hilo.

Hata hivyo Lyamuya aliahirisha kesi hiyo hadi keshokutwa ambapo kesi hiyo hiyo itaendelea kusikilizwa. Mara ya mwisho, kesi hii iliahirishwa Septemba 9, mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, April 15, 2009

No comments:

Powered by Blogger.