ROGER MUZUNGU
Kilio chetu cha kurejeshwa tuzo za Kili kimesikika
*Tumefanikiwa kutwaa tuzo ya wimbo bora wa mwaka huu
Na Happiness Katabazi
“TIMU ya taifa, hatutaki zaidi, tunatosheka na afadhali.”
Si kila mwanamke anaye kwenda baa ni malaya, si kila mwanamke anayeingia baa anajiuza, wengine waenda baa ni kwa starehe zao binafsi, kwenye pochi zao wana fedha zao za matumizi. Fedha za kula, fedha za kunywa na usafiri wa kurudi majumbani eh, kwao.
“Eh nashindwa kuelewa juu ya nini binadamu twakuwa na imani potofu? Hasa kwa dada zetu twawafikiria vibaya. Mwanamke akienda kazini hawamsemi lakini akienda kuangalia FM Academia , tu wanachonga chonga na kumuona malaya why…kwanini”?
Hayo ni baadhi ya mashairi yanayopatikana katika kibao cha ‘Heshima kwa Wanawake’ toka Bendi ya FM Academia ‘wazee wa ngwasuma’ ambacho kimewapatia heshima ya kutwaa tuzo ya wimbo bora wa mwaka, katika mashindano ya muziki hapa nchini maarufu kama ‘Kill Awards Tanzania’.
Kufuatia hatua hiyo, gazeti hili liliamua kumtafuta mtunzi wa kibao hicho, Roger Muzungu, ambapo hakuna ubishi kuwa kadiri siku zinavyosonga mbele kinazidi kujipatia umaarufu na kubadili mtazamo wa jamii kwa mtoto wa kike.
Tangu enzi za mababu zetu ilijengeka dhana kwamba mtoto wa kike ni dhaifu na kwamba hawezi kufanya jambo lolote bila kupata msaada wa mwanamume.
“Nathubutu kusema dhana hii ilikuwa ikirutubisha mfumo dume lakini katika karne hii wanaharakati, wanawake wenyewe wamesimama kidete kuhakikisha dhana kama hizo, mfumo dume unatokomezwa na kwa kiasi fulani tunaanza kuona mafanikio ya vita hiyo kwani hivi sasa wanawake wengi wameteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali na wamekuwa wakiendesha familia zao bila kutegemea msaada wa mwanamume,” alisema Muzungu.
Kwa wale wanaofuatilia bendi za muziki wa dansi za hapa nyumbani, utakubaliana nami kuwa Muzungu ni miongoni mwa wanamuziki wanaojiheshimu, na mwenye subira, hali iliyomfanya hata kupata mafanikio kwenye fani hiyo ya muziki kutokana na vibao vyake kutamba.
Kwa wale msiomjua Muzungu, mwanamuziki huyo alianza kutumikia bendi ya Dimond Sound ‘Ikibinda Nkoi,’ waliokuwa na maskani yao ukumbi wa Silent Inn, wakati huo akiwa mwanamuziki na mwalimu wa wanenguaji wa bendi hiyo lakini kwa bahati mbaya kuna baadhi ya nyimbo alizitunga akiwa na bendi hiyo hazikuweza kurekodiwa hadi bendi hiyo iliposambaratika.
Roger Muzungu a.k.a ‘mutu ya zamani’, ambaye ni mwanamuzi wa FM Academia, anasema anajisikia ni mwenye furaha wimbo alioutunga kupata tuzo ya wimbo bora wa mwaka 2009.
Anasema amefurahi sana kwani imethibitisha ni jinsi gani Watanzania kwa ujumla wamekubali mashairi yaliyomo kwenye wimbo huo ambao anasema ulimchukua miaka miwili kukaa chini na kuutunga na kisha kuukabidhi kwenye bendi yake na kufanyiwa mazoezi na wanamuziki wenzake na kisha kurekodiwa na kuanza kusikika kwenye vituo mbalimbali vya utangazaji.
“Nawashukuru wapenzi wa bendi yetu ya FM Academia ambao tumekuwa nao bega kwa bega na wote walioupigia kula wimbo huo hadi kula zikatosha na hatimaye wimbo huu ukapata tuzo na tunawaahidi kuwa muda si mrefu tutatoa vibao vipya vikali hivyo mkae mkao wa kula,” anasema Roger Muzungu kwa kujiamini.
Anasema huo ni wimbo wake wa pili kuutunga akiwa na bendi hiyo, wimbo wa kwanza ulikuwa, ‘Heinken Ngwasuma’ uliopigwa kwa mtindo wa sebene.”
Muzungu anasema Juni mwaka huu, bendi yake inatarajia kukamilisha albamu na nyimbo zipo tayari na moja ya nyimbo hizo ni Heshima kwa Wanawake, Vuta nikuvute uliotungwa na Elombee, Jusmine wa Nyoshi El Saddat, Fadhira kwa Mama wa Katumbi Jesus, Matatizo ya Yangu wa Toscanie na Generique ambao umetungwa kwa kushirikisha wanamuziki wote wa bendi hiyo na utakuwa na maadhi ya sebene.
Anasema baadhi ya nyimbo nyingine ambazo zitaingia kwenye albamu hiyo, bado hazijapangiwa majina.
Kuhusu bendi yao kuondolewa kwenye mashindano ya Kill Awards mwaka jana kwa sababu bendi yao ni ya Wakongo, anasema walilamikia wazi wazi kipengele hicho na kwa sababu bendi hiyo haina Wakongo peke yao pia ina wanamuziki Watanzania.
“Tunashukuru kilio chetu kimesikika hatimaye katika mashindano ya mwaka huu, Kill Award iliondoa kipengele hicho hivyo kufanya bendi yetu kushiriki mwaka huu, na mungu akasaidia tukafanya vizuri” anasema Munzungu.
Anasema wimbo wake unapendwa hata na wanaume wamekuwa wakiunga mkono mashahiri yake na kwamba aliamua kutunga wimbo huo kwani jamii ilikuwa na mtazamo hasi kwa wanawake kwamba wakienda baa au kumbi za starehe wanaonekana ni wanawake wasi na maadili mema na ni malaya.
Kumbe hali sasa ni tofauti kwani wanawake hivi sasa wengine wamepata elimu, wanajibidiisha kwenye biashara za kuwaingizia vipato halali, hivyo baadhi ya wanawake siku hizi utawakuta wanakutana pamoja kwenye kumbi za starehe kubadilishana mawazo na kuagiza vinywaji kwa gharama zao bila ya kutegemea wanaume, hatua hii ni muhimu katika harakati za kusaka usawa kijinsi barani Afrika.
Muzungu anawahasa wanamuziki wenzake kuwa waache chuki zisizo na maendeleo bali wawe wabunifu katika fani ya muziki ili wanamuziki wote waweze kukuza muziki wa Tanzania.
Akizungumzia mchakato wa Kill Awards Tanzania, mwaka huu, Muzungu anasema yeye binafsi anaona haki imetendeka kwa sababu hata yeye alikuwa ana fikira kuwa bendi zenye wanamuziki kutoka Kongo, zingebaguliwa, lakini hilo halikutokea kwani mambo yamekwenda vizuri kama yalivyopangwa.
Aidha, anatoa changamoto kwa waandaaji wa Kill Awards kwamba wajitanue zaidi kwa kushirikisha bendi na nyimbo za wanamuziki kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki(EA), kwasababu kushirikisha nchi hizo kutaimarisha mahusiano mema kwa wanamuziki kutoka nchi hizo.
Pia kutaitangaza Kill Awards na pia kuwafanya wanamuzi na bendi kutoka nchi hizo kuongeza bidii katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Hata hivyo anazitaka zile bendi au wanamuziki ambao hawajabahatika kupata tuzo katika mashindayo yaliyopita wasikate tamaa, bali waongeze bidii na waendelee kushiriki, kwani ipo siku nao watapata tuzo, kwani tuzo haziwezi kutolewa kwa wanamuziki na bendi zote zilizoshiriki katika shindao hilo kwa wakati mmoja.
Muzungu ambaye hujivuma vilivyo awapo jukwaani, anamaliza kwa kutoa shukrani zake za dhati kwa wale wote waliofanikisha FM Academia waliotwaa Tuzo ya wimbo bora wa mwaka.
Hii ni mara ya pii kwa FM Academia ambayo imejizolea mashabiki ndani na nje ya nchi kutwaa tuzo za Kill Awards, mwaka juzi katika mashindano ya Kill Awards, bendi hiyo kupitia albamu yake ‘Dunia Kigeugeu’ ilipata tuzo ya albamu bora.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, April 18, 2009
No comments:
Post a Comment