Header Ads

BAWATA YAIBWAGA SERIKALI KORTINI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imesema uamuzi wa serikali kuingilia Baraza la Wanawake Tanzania (BAWATA) lisifanye shughuli zake, ulikuwa batili kwa sababu ulivunja katiba ya nchini.

Sambamba na hilo, mahakama hiyo imesema vifungu 2(2), 6, 9(a)(b)(iii), 12 na 13(2) vya Sheria ya Asasi za Kijamii ambavyo sasa vinasomeka kifungu cha 2(2),814,17 na 19(2) kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, vinavunja ibara ya 15(1), 18 na 20 ya katiba ya nchi, hivyo imeitaka serikali kuvifanyia marekebisho ndani ya mwaka mmoja kuanzia jana.

Walalamikaji katika kesi hiyo ya kikatiba namba 27/1997, ni BAWATA, Profesa Anna Tibaijuka, Sherbanu Kabisa, Rose Mushi, Mary Marealle na Salma Kauli ambao walikuwa wakitetewa na Profesa Issa Shivji dhidi ya Msajili wa Asasi za Kijamii, Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Ameir Mohamed na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo, Amir Manento (amestaafu), Jaji Laurian Kalegeya (Mahakama ya Rufani sasa) na Jaji Justus Mlay na kusomwa kwa niaba yao na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Saul Kinemela.

Jaji Manento alisema jopo hilo limefikia uamuzi huo baada ya kubaini uamuzi uliotolewa Septemba 17, mwaka 1996 na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani, F. Mushy haukufuata haki za msingi zilizobainishwa kwenye katiba.

“Katiba ya nchi ni sheria mama na endapo kuna sheria yoyote nchini inakinzana na katiba, sheria hiyo ni batili, hivyo uamuzi wa serikali wa kusimamisha shughuli za BAWATA ulikuwa batili.

“Kwa kuwa jopo hili limeutangaza uamuzi huo ni batili, na kwa kuwa BAWATA ilisajiliwa kwa misingi ya kufuata sheria, tunaiamuru serikali iwalipe walalamikaji sh milioni 20, ikiwa ni usumbufu na gharama za uendeshaji kesi, kwani kwa kipindi chote hicho asasi hiyo ilikuwa imesimama kufanya shughuli zake,” alisema Jaji Manento.

Hata hivyo, alisema upande wa serikali katika kesi hiyo umeshindwa kuthibitisha madai yake kwamba BAWATA ilikuwa ikiendeshwa kama chama cha siasa.

Kwa mujibu wa hati ya madai, inaonyesha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mushy, Septemba 17 mwaka 1996, aliamuru kusimamishwa kwa shughuli za baraza hilo kwa madai kuwa lilikuwa likiendeshwa kama chama cha siasa, katiba yake haikupitishwa na mkutano wa wanawake wote/mkutano mkuu wa wanawake uliopitisha azimio la kuiunda na kwamba badala ya kuandaa na kuongoza wanawake kijamii na kiuchumi, lilikuwa linajiingiza kwenye siasa.

Mushy aliagiza BAWATA itaendelea kufungiwa hadi itakapoitisha mkutano mkuu na kuchagua viongozi wake, katiba ya baraza kupitishwa na wanawake wote na mfumo wake uwe umebadilishwa kutoka ule unaofanana na chama cha siasa na kuwa wa uratibu wa vikundi vya wanawake kwa ajili ya maendeleo, na kwamba mfumo usifanane na ule wa ngazi za utawala.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Profesa Tibaijuka, alieleza tayari walishachaguliwa kwa mujibu wa katika na kwamba BAWATA si chama cha siasa.

BAWATA ilisajiliwa Mei 16, mwaka 1995 na kupewa hati Na. SO 8404 chini ya Sheria ya Asasi ya Jamii ya mwaka 2002. Wazo la kuunda asasi ya wanawake lilizaliwa mwaka 1991 na kujadiliwa pamoja na maofisa wa Umoja wa Wanawake (UWT), kwa barua ya Septemba 22, 1993. Aliyekuwa Mwenyekiti wa umoja huo, Sophia Kawawa, alimtaka Profesa Tibaijuka kuitisha mkutano kujadili ‘nafasi ya wanawake katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini’.

Mkutano wa siku tatu uliudhuliwa na washiriki wapatao 400 ulifanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia 24 hadi 27 Julai 1994.Mkutano uliazimia kuunda asasi ya kitaifa ya wanawake isiyofungamana na vyama vya siasa na kuunda kamati ya muda ya watu 10 iliyoundwa na Tibaijuka kuchaguliwa kuwa mwenyekiti katika kikao cha pili cha kamati hiyo.

Ilipofika Februali 18, 1995, Kamati ya Muda iliitisha kongamano, ukumbi wa British Council jijini,ambapo wanawake wengi walioudhuria mkutano wa kwanza Chuo Kikuu walialikwa na kuhudulia na kushiriki kikamilifu.Mwenyekiti wa kwanza wa UWT-Bibi Titi Mohamed alifungua kongamano lililoudhuria na wanawake 72 na ndilo lilipitisha Katiba ya BAWATA , likaomba usajili na hatimaye kusajiliwa kwa baraza hilo.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu iliunga mkono usajili wa BAWATA na katika barua yake ya Mei 9, 1995 pamoja na mambo mengine, ilisema:“Nimeipitia Katiba hiyo na nimeridhika kabisa kwamba malengo na matarajio ya BAWATA kama yalivyoonyeshwa kwenye Katiba hayapingani na Katiba ya Nchi wala Sheria zozote zilizoko hivi sasa hapa nchini, na kwa sababu hiyo, kwa nakala ya barua hii namshauri MSajili wa Vyama atakapojiridhisha na masharti mengine yote kuhusu usajili wa vyama, akisajili chombo hiki, BAWATA.’

Baada ya kusajiliwa , Kamati ya Muda ilianza kazi ya kuunda matawi kwa ngazi ya chini ya vijiji na wilaya na kufanya uchaguzi wa viongozi wa ngazi hioz.Hatimaye, uliitishwa Mkutano Mkuu, kwa mujibu wa ibara ya 14(3) na 22, kuchagua uongozi wa kitaifa.

Aidha ilipofika Septemba 1996 , mwaka mmoja na miezi minne tangu kusajiliwa kwa baraza hilo ilikuwa na wanachama 150,000 nchi nzima,katika wilaya 111 na matawi 2000,katika shughuli za kijamii,kiuchumi na elimu kwenye ngazi ya vijiji zenye shabaha ya kuinua ubora wa maisha ya kina mama na ikapata umaarufu katika muda mfupi ikizingatiwa kuwa kwa mika yote kulikuwa na ukiritimba wa chama kimoja cha wanawake nchini chini ya chama kimoja.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, April 3, 2009

No comments:

Powered by Blogger.