Header Ads

MSHITAKIWA MUHIMU KESI YA ZOMBE AFARIKI DUNIA

*Ni Koplo Rashid Lema aliyelazwa Ocean Road Dar
*Aacha ujumbe mzito kwa Zombe kabla ya kukata roho

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA wa 11 katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake tisa, Koplo Rashid Lema, amefariki dunia.


Lema ambaye amekuwa akielezwa kuwa ni shahidi muhimu katika kesi hiyo, amefariki dunia majira ya saa 10, alfajiri ya kuamkia jana, katika Taasisi ya Saratani, Ocean Road ya jijini Dar es Salaam, alikolazwa kwa zaidi ya wiki tatu sasa.

Mbali ya Zombe na Lema, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka wilayani Ulanga, Morogoro, na dereva teksi mmoja, ni pamoja na SP Christopher Bageni, SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasabi.Mkurugenzi wa Tiba wa Taasisi hiyo, Dk. Khamza Maunda, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, Lema alifariki dunia akiwa katika wodi namba nne, alikokuwa amelazwa.

Hata hivyo, alisema hawezi kutaja maradhi yaliyokuwa yakimsumbua kwa sababu miiko ya taaluma yake hairuhusu kufanya hivyo.

“Lema kama mgonjwa wetu, nathibitisha kuwa amefariki saa 10 alfajiri, usiku wa kuamkia leo (jana) na mwili wake umehifadhiwa hapa hospitalini, hivyo sisi taasisi yetu inangoja hatua zitakazochukuliwa na Jeshi la Magereza na askari wa jeshi hilo, waliokuwa wakimlinda Lema tangu alipolazwa kwenye taasisi hii,” alisema Dk. Maunda.

Baadhi ya wagonjwa waliolazwa wodi moja na Lema, waliliambia Tanzania Daima kuwa, kabla ya kufariki, alifanya vituko na kuacha ujumbe kwa Zombe na washitakiwa wenzake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mgonjwa mmoja ambaye ana kansa ya mguu, alisema, juzi majira ya saa tano usiku, Lema alianza kupiga kelele za kuwaita manesi, akiwataka waje wachukue sh 10,000 wakamnunulie muda wa maongezi (Vocha) ili aweke kwenye simu yake na kumpigia mkewe ili aje aagane naye.


Alisema wakati akitoa maagizo hayo, ambayo hata hivyo hakuweza kutimiziwa, Lema alikuwa akiomba dua kwa lugha ya Kiarabu.

Mgonjwa huyo alisema, kabla ya kufariki dunia, Lema alipiga kelele na kuchukua maji ya mmoja wa wagonjwa wenzake na kuanza kujimwagia kichwani.

“Wakati akifanya hayo, alikuwa akimwomba Mungu amsamehe kwa yote aliyoyafanya na washitakiwa wenzake nao wasamehewe, isipokuwa Abdallah Zombe,” alisema mgonjwa huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

“Tunakuthibitishieni kuwa, Lema amefariki muda huo, kwani hayo yote aliyokuwa akiyafanya sisi tulikuwa tukimshuhudia kwa macho yetu kwa kuwa tunalala naye wodi moja na mwili wake umetolewa wodini kupelekwa mochwari majira ya saa moja asubuhi, na hata mkewe alivyofika asubuhi, alilia sana,” alisema mgonjwa mwingine anayesumbuliwa na kansa ya tumbo.

Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi (ACP) Mtiga Omar, naye alithibitisha kupokea taarifa hizo kifo hicho.

Kwa mujibu wa utaratibu wa jeshi hilo, mhusika mkuu wa kifo hicho ni Mkuu wa Gereza la Keko, kwani ndipo alipokuwa akiishi kama mahabusu.
Msemaji huyo, alisema Mkuu wa Gereza la Keko, anawajibika kufika katika hospitali aliyofia mahabusu wake na kuthibitisha kwa maandishi kifo hicho na kisha anatakiwa kupeleka taarifa hiyo makao makuu ya jeshi hilo na pia anawajibika kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
“Akishatoa taarifa Polisi, pia anawajibika kutoa taarifa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambako ndiko kesi iliyokuwa ikimkabili marehemu na wenzake ipo, na kisha kuongozana na polisi kwa ajili ya kuchunguzwa mwili wa marehemu huku wakishirikiana na askari wa magereza, aliyekuwa akimlinda hadi alipofariki.
“Kisha mwili unakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi au kama marehemu hana ndugu, atazikwa na jiji,” alisema ACP Mtiga.
Tanzania Daima pia ilifika nyumbani kwa marehemu, Kota za Polisi Oysterbay na kushuhudia umati mkubwa wa watu waliofika kuomboleza kifo hicho.
Haruna Khalfani Lema, ambaye ni mjomba wa marehemu, alisema wanasubiri wakabidhiwe mwili wa ndugu yao na mamlaka husika ili waweze kuusafirisha kwenda Moshi kwa ajili ya mazishi.
Haruna alisema, marehemu ameacha wajane wawili na watoto watano.
Lema ambaye alikuwa akisumbuliwa na maradhi kiasi cha kushindwa kutoa utetezi wake mahakamani, alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Machi 3, mwaka huu, na kuhamishiwa Ocean Road Machi 19, hadi alipofariki.
Kabla ya kufikishwa Muhimbili, Lema alikuwa akitibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke ambako alipelekwa Machi 2 baada ya kuzidiwa gerezani.
Zombe na wenzake, walianza kutoa utetezi wao wa kesi hiyo inayovuta hisia za wengi Februari 3, mwaka huu.
Lema, akiwa miongoni mwa washtakiwa hao, alifika Mahakama Kuu na wenzake kuingia, lakini yeye alishindwa na kulazimika kukaa ndani ya mahabusu ya mahakama hiyo kwa sababu alikuwa hawezi kukaa kwenye kiti.
Siku hiyo, ndiyo ilikuwa ni mara yake ya mwisho kufika mahakamani hapo, akiwa amedhohofu kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimkabili kiasi cha kulazimika kutembea kwa msaada wa wenzake.
Februari 19, mwaka huu, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Massati ambaye anasikiliza kesi hiyo, alilazimika kuahirisha kuisikiliza baada ya Lema kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi wake kutokana na afya yake kuzidi kuwa mbaya.

Lakini kabla ya Jaji Massati kutoa uamuzi huo, wakili Denis Msafiri, anayewatetea (Lema, Rajabu Bakari) aliiomba mahakama aende gerezani kumuona Lema na kuona afya yake kama inamruhusu kufika mahakamani kutoa ushahidi.

Jaji Massati alipomuuliza ni kwa nini mshitakiwa wa 12, asiendelee kutoa ushahidi wake siku hiyo, wakili huyo alidai ni muhimu Lema atoe ushahidi wake kwanza ambao utatoka kwenye kinywa chake, ndipo mshtakiwa wa 12 afuate kutoa ushahidi, hoja ambayo ilikubaliwa na Jaji Massati na kuahirisha kesi hiyo hadi kikao kijacho.

Lema anaelezwa kuwa shahidi muhimu kwa sababu ndiye alibadilisha sura ya kesi hiyo, kwani baada ya kutoka mafichoni alikokuwa amejificha, alimweleza mlinzi wa amani aliyechukua maelezo yake kwamba, mauaji ya watu hao, yalifanyika kwenye msitu wa Pande.

Zombe na wenzake,wanadaiwa kufanya mauaji hayo Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, ambapo waliwaua, Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, April 4, 2009

No comments:

Powered by Blogger.