Header Ads

JK APANGUA WAKUU WA MIKOA 11

*Kandoro ahamishwa Dar na kwenda Mwanza
*Mabadiliko yawagusa ma-RC walio wabunge
*William Lukuvi amrithi Kandoro Dar es Salaam

Na Happiness Katabazi


SIKU chache baada ya kufanya mabadiliko makubwa ya wakuu wa wilaya nchini, Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko mengine madogo ya wakuu wa mikoa.

Katika mabadiliko hayo, rais ameendelea kuziacha sura zile zile za wakuu wa mikoa na badala yake akawahamisha kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kusainiwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Aggrey Mwanri inaonyesha kuwa mabadiliko hayo ambayo yalikuwa yakitarajiwa, yamehusisha wakuu wa mikoa 11 kati ya 21 wa Tanzania Bara pekee.

Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, ambayo yameelezwa kuwa na lengo la kusukuma utendaji serikalini, wakuu wote wa mikoa ambao ni wabunge wa majimbo na mmoja wa viti maalum, wameguswa, jambo ambalo linaweza kuibua maswali kuhusu utendaji na pengine ufanisi wao wa kazi.
Miongoni mwa mabadiliko makubwa ni uamuzi wa Rais Kikwete kumhamisha kutoka Dar es Salaam, Abbas Kandoro na kumpeleka mkoani Mwanza.
Kandoro anaondoka Dar es Salaam akiwa ameuongoza mkoa huo kwa miaka mitatu baada ya kuteuliwa mwaka 2006, kuchukua nafasi ya Luteni Yussuf Makamba aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika mabadiliko hayo, nafasi ya Kandoro sasa itachukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, William Lukuvi.
Kuondoka kwa Kandoro, kunakuja siku chache tu baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kufanya ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam kukagua mazingira na shughuli za usafi na kuibua maswali kuhusu masuala mbalimbali.
Aidha, kuhamishiwa Dar es Salaam kwa Lukuvi, kada wa CCM ambaye amepata kufanya kazi na Rais Kikwete zama wakiwa viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana enzi ikijulikana kama UVT miaka ya 1980, kunaweza kukawa kuridhishwa kwake na namna alivyoweza kuuongoza Mkoa wa Dodoma katika kipindi cha miaka takriban minne sasa.
Wakati Lukuvi ambaye ni Mbunge wa Isimani mkoani Iringa akihamishiwa Dar es Salaam, nafasi yake ya Dodoma imekwenda kwa Dk. James Msekela ambaye kama ilivyo kwa Lukuvi, ni Mbunge wa Tabora Kaskazini.
Wengine waliohamishwa kutoka vituo vyao ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Enos Mfuru ambaye anakwenda Mara kuchukua nafasi ya Issa Machibya anayehamia Morogoro.

Katika mabadiliko hayo madogo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Meja Jenerali Said Kalembo anahamia Tanga anakokwenda kuchukua nafasi ya Mohamed Abdulaziz.
Aziz ambaye naye ni Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini, amehamishiwa katika Mkoa wa Iringa akimrithi, Hajaat Amina Mrisho, anayekwenda mkoani Pwani.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Christine Ishengoma ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum amehamishiwa Mkoa wa Ruvuma.

Katika mlolongo huo huo wa mabadiliko, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Monica Mbega ambaye naye ni Mbunge wa Iringa Mjini, amehamishiwa mkoani Kilimanjaro akichukua nafasi ya Mohammed Babu anayekwenda Kagera.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi 16, 2009

No comments:

Powered by Blogger.