MEJA LUHWAGO AFARIKI DUNIA
Na Happiness Katabazi
KAIMU Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano na Mhariri Mkuu wa gazeti la Ulinzi linalotolewa kila mwezi, Meja William Luhwago (50), amefariki dunia.
KAIMU Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano na Mhariri Mkuu wa gazeti la Ulinzi linalotolewa kila mwezi, Meja William Luhwago (50), amefariki dunia.
Taarifa iliyotolewa jana na Idara ya Habari na Uhusiano ya Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa vyombo vya habari, ilieleza Meja Luhwago alifariki juzi usiku katika Hospitali ya Tumaini, Dar es Salaam baada ya kuugua ghafla.
Taarifa hiyo ilieleza Luhwago atakumbukwa kwa mchango wake wa uadilifu, uaminifu na uchapakazi alioutoa katika jeshi kwa muda wote wa utumishi wake. Marehemu ameacha mjane na watoto watano.
Wakati wa uhai wake, Meja Luhwago alishika nyadhifa mbalimbali, ikiwamo mwandishi wa habari mwandamizi Makao Makuu ya Jeshi, Mhariri Mkuu wa gazeti la Ulinzi, Mkuu wa Kitengo cha Uandishi na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma jeshini, wadhifa aliokuwa nao hadi alipofariki dunia.
Meja Luhwago alijiunga na JWTZ mwaka 1977, wakati wa utumishi wake jeshini alipandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali hadi kufikia cheo cha meja.
Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa msiba upo nyumbani kwa marehemu Upanga. Marehemu atazikwa kwa heshima zote za kijeshi katika Kijiji cha Bomalang’ombe, Kata ya Bomalang’ombe, wilayani Kilolo, Iringa.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, April 2 mwaka 2009
No comments:
Post a Comment