Header Ads

JEETU PATEL AOMBA AKATIBIWE INDIA

Na Happiness Katabazi

MSHTAKIWA wa kwanza katika kesi ya wizi wa sh bilioni 2.5 za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu Jeetu Patel, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, impe ruhusa ya siku 30 kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa moyo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 1154/2008 ni Devendra Patel na Amit Nandy, ambao wote pamoja na Jeetu Patel wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando, Joseph Tadayo na Martin Matunda.

Mbele ya jopo la mahakimu wakazi wa mahakama hiyo, linaloongozwa na Hakimu Rwaichi Meela anayesaidiana na Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, John Kayoza na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, Grace Mwakipesile, wakili Marando aliwasilisha ombi hilo kwa niaba ya mteja wake, Jeetu Patel, muda mfupi baada ya Meela kusema kuwa, wasingeweza kusikiliza maelezo ya awali jana, kwani ni wapya katika kesi hiyo na bado hawajapatiwa nakala ya kesi hiyo.

Awali, kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na hakimu mmoja, lakini sasa imefikia hatua ya kuanza kusikilizwa, na imepangiwa jopo la mahakimu wakazi watatu.
Marando aliiambia mahakama hiyo kuwa, Jeetu Patel anasumbuliwa na maradhi ya moyo na amekuwa akitibiwa katika Hospitali ya Hindu Mandal.

Alidai kuwa, hospitali hiyo imeandika taarifa mbili za uchunguzi wa ugonjwa unaomsumbua mteja wake, na kupendekeza akatibiwe nchini India kwani hospitali hiyo haina uwezo wa kumtibu.
Marando alidai kuwa, licha mteja wake kukabiliwa na kesi nne mahakamani hapo, anaomba aruhusiwe kwenda India kuanzia Aprili 20 hadi Mei 14, mwaka huu kwa ajili ya matibabu.

Kwa upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na wakili wa serikali, Vitulis Timon ambaye alikuwa akisaidiana na Fredrick Manyanda, Oswald Tibabyekoma na Stanslaus Boniface, ulidai kuwa hawana pingamizi na ombi hilo.

Hata hivyo, kiongozi wa jopo hilo la mahakimu wakazi, Meela alisema watatoa uamuzi wa ombi hilo leo kwani watakuwa wameshapitia nakala za kesi hizo kwenye majalada yao.
Novemba 16, mwaka jana, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa wote kwa pamoja bila ya halali yoyote, walitumia kampuni yao ya Nobel Azania Investment Ltd kuonyesha kuwa kampuni ya nje ya Bencon Investment, imewapatia idhini ya kurithi deni lake la sh bilioni 2.5.

Wakati huo huo, kesi nyingine ya EPA ya wizi wa sh bilioni 1.8 inayomkabili Bahati Mahenge, Manase Makale, Eda Makale na Davis Kamungu, itasikilizwa na jopo la mahakimu wakazi wawili wapya.

Kiongozi wa jopo hilo ni Sekela Mosha anayesaidiana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha ambaye alisema kuwa kesi hiyo itaanza kusikilizwa Mei 13-15, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi za umma na kusababisha hasara ya sh bilioni 220, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba na Meneja Mradi wa benki hiyo, Dogratius Kweka, jana ilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Walirwande Lema alisema, Aprili 23, mwaka huu, atatoa uamuzi kuhusu ombi la mawakili wa utetezi waliokuwa wakitaka washtakiwa hao wafutiwe kesi kwa kuwa siku 60 za upelelezi wa kesi hiyo, zimepita, lakini haujakamilika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, April 16, 2009

No comments:

Powered by Blogger.