Header Ads

HATMA YA LIYUMBA APRIL 23

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema uamuzi wa kufuta au kutoifuta kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Miradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka, utatolewa Aprili 23 mwaka huu.

Hayo yalisemwa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Waliwande Lema, baada ya kusikiliza maombi ya upande wa mashitaka na wa utetezi, ikiwamo kutaka mahakama hiyo itumie kifungu cha 225 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai 1985, kitachotamka kuwa ndani ya siku 60 upelelezi katika kesi husika uwe umekamilika.

Lema alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kutoa uamuzi wa kutaka kesi hiyo itajwe tena Aprili 15, mwaka huu na uamuzi wa ombi hilo la upande wa utetezi, atautoa Aprili 23 mwaka huu.

Awali Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface ambaye alikuwa akisaidiana na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Frederick Manyanda na Wabuhanga, aliieleza mahakama hiyo kuwa, shauri hilo jana lilikuja kwa ajili ya kusikiliza maombi matatu.

Aliyataja maombi hayo kuwa ni ya washtakiwa kutaka waachiliwe huru kwa sababu hati ya mashitaka ina kasoro, kusikiliza pingamizi la upande wa mashtaka ambalo linaiomba mahakama hiyo isiyakubali maombi ya washitakiwa na ombi la tatu la upande wa utetezi la kutaka kesi hiyo ifutwe kwa sababu siku 60 zimepita tangu ilipofunguliwa na upelelezi bado haujakamilika.

Wakili wa utetezi, Majura Magafu ambaye alikuwa akisaidiana na Profesa Gamalieli Mgongo Fimbo, Hurbet Nyange na Hudson Ndyusepo, alieleza maombi ya kutaka wateja wake waachiwe huru chini ya kifungu cha 225(4), (5) cha CPA.

Akijibu hoja za Magafu, Boniface alidai kuwa upande wa mashitaka wanakubaliana na kifungu 225 CPA na kwamba upelelezi bado haujakamilika ndani ya siku 60, ila aliomba mahakama iangalie kuwa siku 60 hazikuisha Machi 26 bali ziliisha Machi 28 mwaka huu, hivyo hadi kufikia jana, zilikuwa zimepita siku tano tu.

“Baada ya kusema hayo, turudi kwenye kifungu 225, chote kinaangukia chini ya sehemu ya saba ya sheria za ndani (utaratibu wa uendeshaji wa mashauri katika mahakama za chini)… ninachofahamu kesi hii ilipelekwa Mahakama Kuu Februari 6 na upande wa mashtaka walikuwa ni wadaiwa katika ombi lao la kutaka wapunguziwe masharti ya dhamana.

“Mheshimiwa hakimu, Februari 10, maombi yao yalisikilizwa na Jaji Projest Rugazia na alitoa uamuzi Februari 13, mwaka huu, hivyo kesi hiyo haikuwepo Mahakama ya Kisutu kuanzia Februari 6-13, na hatufahamu kesi hiyo ilikuja lini mahakamani hapo na kufanya kesi hiyo kutokuwepo mahakamani hapo kwa siku saba,” alidai Boniface.

Aliendelea kudai kuwa, ni kweli kwamba kifungu hicho kinaweka muda wa ukomo pale kesi zinapokuwa zinazagaazagaa mahakamani bila kusikilizwa, na kuongeza kuwa kwa bahati mbaya kesi hiyo ilikuwa kwenye mahakama tofauti.

Machi 30, mwaka huu, Lema alianza kuendesha kesi hii baada Hakimu Mkazi, Hadija Msongo ambaye ndiye alikuwa nayo tangu ilipofunguliwa Januari 27, mwaka huu, kujiondoa baada ya jamii kupitia vyombo vya habari kulalamikia dhamana ya Liyumba.

Februari 17, mwaka huu, hakimu Msongo alimwachia kwa dhamana iliyozua utata Liyumba.
Utata huo, ulitokana na kauli ya wakili wa serikali, Justas Mulokozi kuonyesha kushangazwa na uamuzi wa kumwachia mtuhumiwa huyo licha ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Moja ya masharti ambayo wakili huyo alidai hayakutimizwa na Liyumba, ni kuwasilisha mahakamani hati zenye thamani ya sh bilioni 55, wadhamini wawili wa serikali wakiwa na barua kutoka kwa waajiri wao na kukabidhi hati za kusafiria mahakamani hapo.

Lakini siku hiyo Liyumba aliwasilisha hati yenye thamani ya sh milioni 882, hati ya kusafiria ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, huku wadhamini wawili wakiwa hawana barua zilizosainiwa na mwajiri wao kama masharti yalivyotolewa na mahakama.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, April 3, 2009

No comments:

Powered by Blogger.