Header Ads

SHAHIDI ADAI SAINI YA MTENDAJI MKUU WA BRELA ILIGUSHIWA

Na Happiness Katabazi

MCHUNGUZI wa Maandishi, Maabara ya Upelelezi Kitengo cha Forensic Bureau ya Jeshi la Polisi nchini, C.8565 Station Sajent, Othuman (49), ambaye ni shahidi wa tano katika kesi ya wizi wa sh biloni 1.8 za EPA, inayomkabili Farijala Hussein na Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma, Rajab Maranda, jana aliieleza mahakama kuwa saini iliyowekwa kwenye hati ya usajili wa kampuni ya Kiloloma & Brothers si saini ya Afisa Mtendaji Mkuu wa (BRELA), Esteriano Mahingira.

Shahidi huyo, alieleza kwamba baada ya kufanyia uchunguzi wa kitaalam, saini ya Mahingira na saini iliyosainiwa kwenye hati ya usajili wa Kampuni ya Kiloloma & Brothers, ilibainika kuwa ilikuwa imeghushiwa.

“Baada ya kuletewa hati ya usajili wa Kiloloma & Brothers na saini ya Mahingira kwa sababu ndiyo zilizokuwa zikibishaniwa hasa, nilichukua vifaa maalum ambavyo ni mali ya Jeshi la Polisi ambavyo tunavitumia kutambua maandishi yaliyogushiwwa au la na baada ya uchunguzi wangu nimebaini saini iliyopo kwenye hati ya kampuni hiyo haifanani kabisa na saini ya Mahingira na kwenye ripoti yangu ya uchunguzi ambayo naikabidhi mahakamani ili itumike kama kielelezo, nimesema hilo,” alidai Othuman.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya wakili mwandamzi wa serikali, Fredrick Manyanda, ambaye alikuwa akisaidiana na wakili mwandamizi wa serikali, Stanslaus Manyanda, na shahidi huyo:

Wakilil: Wewe kama mpelelezi na mtambuzi wa Jeshi la Polisi, majukumu yako ni yapi?

Shahidi: Kuchunguza hati mbalimbali mfano, maandishi, saini, alama za mihuri, noti bandia.
Wakili: Ni njia gani mnatumia kubaini kuchunguza hati hizo?
Shahidi: Tunatumia vifaa maalum vya kuchunguza kikiwemo kifaa kiitwacho VSC5000 na elimu tuliyoipata katika nyanja hiyo.

Wakili: Baada ya kutumia vifaa hivyo kuchunguza mnafanyaje?
Shahidi: Naandika ripoti ya uchunguzi niliyofanya kwa mwombaji aliyeomba tumfanyie uchunguzi.
Wakili: Iambie mahakama, Januari 3 mwaka huu, uliambiwa nini kuhusu kesi hii inayoendelea hapa mahakamani?
Shahidi: Nilipokea vielelezo mbalimbali vilivyotoka Idara ya Upelelezi Makao Makuu.
Wakili: Ni vielelezo gani hivyo?
Shahidi: Karatasi za kawaida, mihuri na hati za usajili wa kampuni ya Kiloloma & Brothers.
Wakili: Baada ya kupokea ulifanya nini?
Shahidi: Nilichunguza.
Wakili: Baada ya kuchunguza ulifanya nini?
Shahidi: Niliandaa ripoti ya uchunguzi wetu.
Wakili: Hebu shahidi angalia hii kabrasha.
Shahidi: Hii ni taarifa ambayo imeambatanishwa na nyaraka nilizoletewa nifanyie uchunguzi na pia zina maoni niliyoyatoa kuhusu uchunguzi huo.
Wakili: Hebu tambua hizi nyaraka; inasemaje?
Shahidi: Ni nyaraka ya United Bank of Africa (UBA).
Wakili: Hiyo nyaraka ni ya nani?
Shahidi: Ya Kiloloma & Brothers.
Wakili: Imeandikwa jina la nani?
Shahidi: Rajabu Maranda.
Wakili: Ni namba ngapi na mali ya benki gani?
Shahidi: UBA namba 062352.
Wakili: Inayofuata ni hundi namba ngapi?
Shahidi: 062354 ya benki hiyo.
Wakili: Hizo hundi zilikuja ofisini kwako kufanya nini?
Shahidi: Kufanyiwa uchunguzi.
Wakili: Kwa mujibu wa taarifa yako ni nyaraka zipi za ukweli na zipi ni za uongo?
Shahidi: Hizo zilikuwa ni hundi mbili tofauti zinazobishaniwa, hundi za UBA namba 062352 ya septemba 13 mwaka 2005 na hundi namba 06354 ya Septemba 15 mwaka huo huo.
Wakili: Kuna nyaraka nyingine ndani ya hilo kabrasha?
Shahidi: Ndiyo ipo ni nakala kivuli ya hati ya usajili ya Kiloloma & Brothers na imepewa namba ya usajili 151025.
Wakili: Jalada B lina nini?
Shahidi: Karatasi tano zenye saini ya Rajabu Maranda.
Wakili: Ni nyaraka gani nyingine ipo ndani ya jalada hilo?
Shahidi: Ni hundi ya Benki ya Baroda yenye namba 010389.
Wakili: Imesainiwa na nani?
Shahidi: Rajabu Maranda.
Wakili: Nenda kwenye jalada jingine; lina vielelezo namba ngapi?
Shahidi: B hadi E6.
Wakili: Ina vielelezo gani vitaje kwa sauti tafadhari?
Shahidi: Karatasi sita zenye saini ya Esteriano Mahingira.
Wakili: E hadi E3 na E8 nini kimo ndani yake?
Shahidi: Karatasi sita zenye maandishi sita zenye saini ya Farijara Hussein.
Wakili: Kuna nini tena kwenye hiyo risiti ya New PB Bagamoyo Road Station?
Shahidi: Ina namba 0209 ya Julai 14 mwaka 2005.
Wakili: Ina nini tena ndani yake?
Shahidi: Adendum to leter of offer ya Desemba mosi mwaka 2005.
Wakili: Hati zote kwenye kundi hilo zimesainiwa na nani?
Shahidi: Farijala Shaban Hussein.
Wakili: Ni matokeo ya uchunguzi wako katika hayo makundi?
Shahidi: Nimechunguza maandishi ya vielelezo A5, ambapo zipo kwenye nyaraka zinazobishaniwa.
Wakili: Ukalinganisha na nini?
Shahidi: E3 hadi E8 hizi ni nyaraka ambazo hazibishaniwi.
Wakili: Ukagundua nini?
Shahidi: Nikagundua maandishi yanayobishaniwa na yasiyobishaniwa yanafanana.
Wakili: A na A1-A2 ni nini hizo?
Shahidi: Hizo ni hundi mbili na hazikubishaniwa na zina saini ya Maranda.
Wakili: Katika ripoti yako ulitoa maoni gain?
Shahidi: Niligundua saini zinazobishaniwa na zisizobishaniwa zinafanana.
Wakili: Ieleze mahakama katika uchunguzi wako wakati unachunguza saini ya hati ya usajili wa hati ya Kiloloma & Brothers.
Shahidi: Katika uchunguzi wangu nimebaini kwamba saini iliyopo kwenye hati hiyo ya usajili haifanani na saini ya Mahingira.

Naibu Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Cypriana William aliahirisha shauri hilo hadi Jumatatu ili jopo hilo na wakili wa utetezi Majura Magafu wapate fursa ya kupitia nyaraka hizo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Januari 31 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.