Header Ads

MALECELA,MALECELA UMENISIKITISHA SANA

Na Happiness Katabazi

WIKI iliyopita, jabali katika ulingo wa siasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), John Malecela, alizungumzia mambo mbalimbali yanayohusu chama hicho ikiwemo kukemea wanachama wanaolumbana hadharani bila kupitia vikao halali vya chama.


Pamoja na hilo, alizungumzia mambo mengi ikiwemo mgogoro ndani ya chama na kuwataka wanachama wanaotaka kukihama chama hicho wafanye hivyo haraka .

Pia aliwataka wanachama wanaotaka kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani, wasahau kwa sababu hawawezi kumshinda Rais Jakaya Kikwete.

Malecela hakuishia hapo, alikwenda mbali zaidi, tena bila haya, kwa kueleza kuwa kamwe chama hicho hakiwezi kuyumbishwa na matajiri kwani chama hicho ni cha wanyonge, wakulima na wafanyakazi. Kauli hii ya Malecela imenisikitisha sana.

Ili mtu uheshimike, ni lazima kwanza wewe binafsi ujiheshimu. Ujiheshimu katika nyendo zako, kauli zako unazotoa mbele ya jamii ziwe na ukweli ndani yake, busara na hata kufundisha jamii inayomzunguka.

Na kama mtu atayafanya hayo, basi atakuwa amempendeza Mungu na wanawadamu ambao aliwaumba kwa mfano wake. Usipotenda hayo hata ukiwa ni kiongozi mwenye madaraka makubwa katika taifa lolote au mzee unayeheshimika katika jamii, ukweli ni kwamba utadharaulika hata na watoto wadogo.

Nimelazimika kutumia maneno haya ninayoamini ni yenye hekima kwa sababu, moja ya kauli iliyotolewa na Malecela ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wachache wanaoheshimika nchini kutokana na mchango wao katika taifa hili, kuwa CCM ni chama cha wakulima, wafanyakazi na wanyonge.

Nimuulize mzee Malecela, anazungumzia CCM ya awamu ipi? ni ile ya Awamu ya Kwanza iliyokuwa ikiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, au ni CCM hii iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa na sasa Rais Jakaya Kikwete au hipi?

Mzee Malecela, ni CCM hii ambayo uchaguzi wa mwaka 2005 ambapo na wewe ulikuwa ni miongoni mwa wanachama 10 waliokuwa wakiparurana na kutengeneza mitandao yenu hadi kumwaga fedha kwa waandishi wa habari ili wawarembe kwenye vyombo vya habari muweze kuchaguliwa na Mkutano Mkuu! Mmoja kati yenu aweze kupeperusha bendera ya kuwa mgombe urais?

Mzee Macelela, CCM ya wakulima, wafanyakazi na wanyonge, ndiyo hii ambapo baadhi ya wanachama wake hawasemezani, wanazuliana fitna, hawapikiki chungu kimoja na hawapendani?

Malecela, ni CCM hii ambayo gazeti la Habari Leo hivi karibuni, liliandika habari kwamba kuna baadhi ya wabunge wamepanga njama ya kumuondoa kwenye nafasi ya uenyekiti, mwenyeketi wa sasa Rais Kikwete.

Ni CCM hii ambayo sote tunashuhudi kwamba ili upate madaraka ni lazima ushikwe mkono na vigogo au uwe na fedha za kuwamwagia wapiga kura?

Ebu mzee Malecela weka pembeni unafiki, ghiliba za kisiasa kama ulivyozoea na ueleze umma kwamba ni CCM gani hivi sasa ni ya wakulima, wanyonge na wafanyakazi, ama sivyo hutaamika tena kwani katika hili umezungumza uongo wakati ukweli unaujua.

Wazee wetu tunawaheshimu sana kwani mmetutangulia kuona na kujua mengi hivyo sisi vijana tunapenda kujifunza kutoka kwenu iwe mavazi, aina ya maisha mnayoishi na hata mtindo mnaoutumia kufanya kazi. Sasa ikifikia mahala mkashindwa kutambua hilo mjue nanyi mnachangia kulipeleka taifa kuzimu.

Amekufa Nyerere, lakini kwa kauli zake dhabiti na matendo yake bado tunamheshimu utafikiri bado yupo hai. Lakini yupo Simba wa Vita, Rashid Kawawa, ambaye naye amelitumikia taaifa hili kwa uadilifu mkubwa.

Alijiheshimu, ndiyo maana leo hii tunamheshimu. Hakuwa mchumia tumbo kama walivyo viongozi wengine. Hakutaka kuendelea kung’ang’ania ubunge ili aendelee kuhudhuria vikao vya bunge, akapate posho kama walivyo wabunge wengine ambao hawataki kabisa kupisha wanachama vijana nao wagombee katika majimbo wanayoyashikilia hadi sasa.

Leo hii baadhi ya Watanzania wameanza kumuita Kawawa kuwa ni ‘Baba Mdogo’ wa Taifa letu kwani Baba wa Taifa, Nyerere amefariki dunia.

Nawaunga mkono kwani ndiyo mzee asiye na makuu aliyebaki ambapo hivi sasa baadhi ya viongozi, wananchi, taasisi mbalimbali akiwemo, Rais Kikwete, wamekuwa wakienda kijijini kwake, Madale kumuomba ushauri wa masuala mbalimbali.

Hivyo, kauli ya Malecela kusema chama hakiyumbishwi na matajiri ni uongo mtupu, na kwamba chama hicho ni cha wafanyakazi, wanyonge na wakulima ni uongo mkubwa.Tumuulize Malecela hivi Rostam Aziz, Christopher Gachuma, Yusuf Manji na matajiri wengine ni wanyonge?

Mbaya zaidi , matajiri wengi ndani ya chama hicho, wana haki ya kuwa wanachama, utajiri wao wanautumia kwa ajili ya kukigawa chama kwa kutapanya fedha kwa wanachama wanaowaunga mkono ili wapate madaraka na mwisho wa siku waweze kuwanyoshea biashara zao na kupata tenda kilaini.

Napenda kumsihi mzee wangu Malecela atambue kwamba zile zama na mababu kupiga hadithi za uongo ili wajukuu zao wapate usingizi zimepitwa na wakati, kwani hivi sasa wajukuu tumeelevuka karibu kila nyanja na tumegundua baadhi ya wazee wetu, kwa ujinga, uoga au ubinafsi wao wamelifikisha taifa letu hapa lilipo.

Hivyo, bado tunahitaji mawaidha yenu, ila tunaomba mtuongoze katika mstari ulionyooka na si kutuweka kwenye makundi makundi ambayo yanafadhiliwa na manyang’au kwa maslahi yenu.

Mungu Ibariki Tanzania Mungu Ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, April mosi , 2009

2 comments:

Anonymous said...

Happiness asante kwa kumpa ukweli mzee huyo, hawa ni miongoni mwa watu waliotufikisha hapa tulipo.wamekuwa watawala na siyo viongozi kwa muda mrefu.Nchi hii tangu iondokewe na kiongozi wake sasa hivi watawala wamekuja juu kuifilisi,wako wapi kina Ngombale waliojivisha ngozi ya kondoo huku ni mbwa mwitu,je si Ngomale huyohuyo aliyewahi kuvuliwa uanachama wa CCM/TANU alipokuwa Tanga na aliporudi akajificha kwa kujifanya kama kwamba ukimkata damu itakayo toka ni kijani au njano,leo hii wanaanza kuumbuka tunayaona leo je wameanza lini?.Waandishi haitoshi kuandika tu magazeti wasaidieni wananchi kuelewa nchi inaelekea wapi hata kwa warsha, semina,hasa huko vijijini ambako wengi wao hawasome magazeti na siyo magazeti tu mzungu mmoja aliwahi kusema kwamba "ukitaka kumficha kitu mtu mweusi weka katika kitabu" kwa maana kuwa hatuna jadi ya kusoma.

Anonymous said...

Happiness hongera dada nimefurahishwa na articles zako kwa kweli nafurahi kuona kuwa kuna vijana watanzania wanatumia vipaji vyao vya uwana habari vizuri siyo tu kwa kufunika mambo yasiyokubalika na jamii. Nitaendela kusoma blog yako. Leo hii ni mara yangu kwanza nilikuwa nafuatilia article yako ya huyo Meja aliyefariki nikasema ngoja nisome na mengine kwa kweli endelea na kazi yako nzuri.. from-USA

Powered by Blogger.