Header Ads

REGINALD MENGI HAJAKOSEA

Na Happiness Katabazi

TUHUMA zinazoelekezwa sasa kwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Abrahamu Mengi, kwasababu tu hivi karibuni aliwataja wafanyabaiashara watano kuwa ni ‘Mafisadi Papa’, hazina msingi.

Kashfa hizo za rada,ununuzi wa ndege ya rais,EPA,mifuko ya Pesheni,Richmond zilizuka hapa nchini katika vipindi mbalimbali na wala siyo ngeni masikioni mwetu ila kwale wenye ugonjwa kusahau na wasiyofatilia masuala mbalimbali yanayohusu taifa letu, lazima wataona tuhuma hizo ni ngeni.

Sasa tuhuma zote hizo ziliripotiwa na vyombo vya habari na kuzungumzwa kwa mapana na viongozi wa upinzani. Na hao waliotuhumiwa hawajazikanusha mpaka leo hii.

Haijalishi kwamba vyombo vya upelelezi wa Makosa ya Jinai havikuona umuhimu wa kuwafikisha mahakamani wahusika.

Kinacho thibitika hapa hata hao wahusika wenyewe hawakujitahidi kukanusha tuhuma hizo. Jamii kwa ujumla tunachukulia kuwa kwa watuhumiwa kukaa kimya wamekiri kuhusika na tuhuma hizo.

Iweje leo Mengi anapowataja watu hawa, wanakuja juu na kulalamika kwamba wamekashfiwa?

Wapo wanaodai kwamba Mengi amewataja hao kwasababu hao ni wahindi,waislamu lakini wale walio sikiliza hotuba yake, alitaja majina na kashfa ,hakuzungumzia rangi ya mtu,dini ya mtu wala kabila la mtu.Yeye alisema hao ni mafisadi papa walihusika na ndiyo waliohusika na kashfa hizo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(Utawala Bora),Sophia Simba amejitokeza kidedea kutetea waliotuhumiwa na Mengi, kuwa ameshawahukumu kwa kuwaita mafisadi papa na kwamba ameingilia uhuru mahakama .

Kwa hakika Waziri Simba kakosea, amemcheka Mengi kwa kuchemsha basi yeye katokota kabisa.Mengi mfanyabishara mzalendo siyo Mahakama, alichotaja ni tuhuma na majina ya watuhumiwa na akasema ushahidi anao lakini yeye ajatoa hukumu.

Kwa hiyo mafisadi papa kama wanataka kulumbana na Mengi, mahakama zipo wazi hadi saa tisa na nusu siku zote za kazi. Tusichotaka ni Mawaziri ambao wamefadhiliwa na mafisadi papa kutuambia kile tusichotaka kusikia kuwa nchi yetu ni shamba la bibi .

Kama hawa mabwana wanaoitwa mafisadi papa wameamua kufanya biashara kwa kutumia ufisadi kwa kutuibia sisi, Je tusiseme kwa kuogopa kuambiwa tumewakashfu au tunawabagua?

Simba amechaguliwa tu hivi karibuni kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake(UWT-CCM) kwa kile kinachoamika ulikuwa uchaguzi mchafu unaonuka rushwa.Hakuna aliyehoji alipata wapi mapesa hayo ya kununua kula.

Imekuwa sasa ni utamaduni wa CCM kutumia mabilioni ya fedha katika chaguzi bila kuogopa kuhojiwa.Sasa Waziri Simba, amejidhiirisha kupitia utetezi wake kwa mafisadi Papa kwamba mabilioni yale yaliyotumika kwenye kampeni zake ,yaliyokuwa ni uwekezaji mzuri uliofanywa na mafisadi papa.

Hilo ndilo tunaloliona sisi kuwa ndio msingi mkuu wa Waziri Simba katika kutetea wale waliomweka madarakani.

Kadri siku zinavyokwenda na tunapokaribia uchaguzi Mkuu wa mwakani, kambi ya mafisadi papa itapanuka ,tutawahesabu kila mmoja kwa upande atakaouchagua kuusimamia.

Angalau kwa leo Watanzania wamejua kuwa Simba ambaye pia ni Mwenyekiti wa UWT,yuko kwenye kambi ya mafisadi papa.

Sisi tunajua miongoni walitajwa na Mengi ni Jayantkumar Chandubhai Patel maarufu kwa jina la ‘Jeetu Patel’ ambaye anakabiliwa na kesi nne za wizi wa fedha za EPA,zilifunguliwa pale katika Mahakama ya Hakimu Kisutu,lakini kesi hizo ni sehemu tu ya ufisadi papa na wala Mengi hakuingilia mwenendo wa kesi hizo ambazo zimepewa namba 1153,1154,1155,1157 za mwaka jana, na kesi zote hizo bado hazijaanza kusikilizwa.

Katika kesi namba 1153, Jeetu na wenzake wanatuhumiwa kuiba sh bilioni 3.3,kesi namba 1154 yeye na wenzake wanatuhumiwa kuiba sh bilioni 2.5, kesi namba 1155 yeye na wenzake wameiba sh bilioni 4.9, kesi namba 1157 yeye na wenzake wanatuhumiwa kuibia sh bilioni 3.9.

Kwa hiyo wale wanaomtisha Mengi kwamba kaingilia uhuru wa mahakama je wanajua wanalolisema au wameamua tu kupayuka?

Inavyoonekana ni kwamba katika hoja nzima hii ya Mengi, Mengi aliamua kujadili hoja ya ufisadi na katika kujadili hoja hiyo amepeleka mjadala mzima wa ufisadi hatua moja mbele kwa kutupatia msamiati mpya unaotenganisha mafisadi dagaa,wakawaida ,waliokubuhu ndiyo wamewaita mafisadi papa, na tunasubiri atutajie mafisadi nyangumi.

Hili ni jambo jema na la kheri kwa wanaharakati wa kweli wa vita dhidi ya ufisadi na ubadhilifu wa mali ya umma.Mengi amewawezesha Watanzania waliowanachama na wafadhili wa CCM kujitoa kwenye dimbwi la tuhuma kwamba chama hicho sasa ni chama cha kifisadi.

Inapotokea kwamba mfanyabiashara wenye mahusiano mazuri na CCM kama alivyo Mengi anajitoa kimasomaso kupambana hana kwa hana na ufisadi, anawapa fursa wafanyabiashara ambao ni wana CCM wasiopenda ufisadi kupanda kwenye jukwaa la Wanaharakati wakiwa vifua mbele.

Hii ina maana kwamba ufisadi hauna chama, dini, kabila,mfanyabiashara,rangi hata jinsia. Lakini wapo wale wanaogeuza jambo hili jema alilolifanya Mengi kuwa ni jambo binafsi kwahiyo wamegeuza hoja yake kuwa ni jambo binafsi na hivyo wanadiriki kumsonga, kumdhihaki.

Yafaa Watanzania tutoke hapo tujifunze kujadili hoja badala ya kujadili watu binafsi badala ya kutukana na kukashfiana.Tukifanya hivyo tutapoteza lengo la Demokrasia na heshima ya nchi yetu.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili ,Mei 3,2009

No comments:

Powered by Blogger.