Header Ads

DOWANS YABWAGWA MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara, Dar es Salaam, jana ililifukuza ombi la Kampuni ya Dowans Tanzania Ltd, lililokuwa likiitaka mahakama hiyo ifute maombi ya Shirika la Umeme (TANESCO) la kutaka mitambo hiyo isiuzwe kwa sababu yalikuwa na dosari za kisheria.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Robert Makaramba, ambapo alisema amefikia uamuzi wa kutupa maombi hayo kwa sababu Dowans imeshindwa kuishawishi mahakama ni vipi Tanesco ilitumia vifungu vya sheria visivyo sahihi kuwasilisha ombi lake katika mahakama hiyo.

“Kwa kuwa Dowans imeshindwa kuishawishi mahakama hii ikubaliane na ombi lake, mahakama inalitupa ombi la Dowans na badala yake, inakubaliana na ombi la Tanesco la kutaka mitambo hiyo isiuzwe hadi nitakapotoa uamuzi wa kesi hii, Julai 2, mwaka huu,” alisema Jaji Makaramba.

Jaji Makaramba alisema kuhusu hoja ya Dowans kuwa, mamlaka hiyo haikuwa na uwezo wa kutolea maamuzi ya maombi yaliyowasilishwa na Tanesco, ni dhaifu kwa sababu tayari mahakama hiyo katika kesi hiyo hiyo, ilishawahi kutoa amri ya kuzuia kwa muda mitambo ya kampuni hiyo isiuzwe.

Mei 4, mwaka huu, Kampuni ya Dowans kupitia wakili wake, Abduel Kitururu, iliwasilisha ombi lake mahakamani hapo la kutaka mahakama hiyo itupilie mbali ombi la Tanesco la kuzuia kuuzwa kwa mitambo yake ya kufufua umeme, kwa sababu maombi hayo hayana msingi, kwamba Tanesco inayotetewa na wakili Alex Nguruma imewasilisha mahakamani maombi yake kwa kutumia kifungu kisichokubalika katika kuwasilisha maombi yao.

Katika maombi yake, Tanesco inaiomba mahakama kuzuia Kampuni ya Dowans kuuza mitambo yake kwa namna yoyote hadi shauri lililowasilishwa na Dowans kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa iliyoko Paris, Ufaransa litakapotolewa uamuzi.

Hata hivyo, Tanesco katika kesi hiyo, inaiomba mahakama iiamuru Dowans iweke mahakamani asilimia kumi ya dola za Kimarekani 109,857,686 kama dhamana kufuatia gharama zitakazotumika katika kesi iliyopo Paris.

Katika hoja zake zilizowasilishwa mahakamni hapo kupinga maombi hayo, Wakili Kitururu amedai Tanesco imeleta maombi hayo kwa kutumia kifungu 95 cha sheria ya mwenendo wa kesi za madai (Civil Procedure Code) na kifungu cha 23 (2) cha Sheria inayojulikana kama International Chamber of Commerce Rules.

Kupitia hoja hizo, kifungu hicho hakiwezi kuipa mamlaka mahakama ya Tanzania kushughulikia maombi kama yaliyowasilishwa na Tanesco hapa nchini, bali kipengele hicho cha sheria kinaweza kutumiwa na upande husika katika shauri hilo katika mahakama ya kimataifa kutafuta amri ya zuio kabla kesi ya msingi haijamalizika kusikilizwa.

Inadaiwa kuwa, Juni 23, 2006 Tanesco iliingia makubaliano ya usambazaji wa umeme wa dharura na Kampuni ya Richmond, ambayo ilielekeza majukumu yake kwa Dowans Holding SA.

Baadaye, Dowans Holdings ilielekeza majukumu yake kwa kampuni yake dada ya Dowans Tanzania Limited. Baada ya mapitio ya makubaliamo hayo na mapungufu yaliyojitokeza Juni 30, mwaka jana, Tanesco iliiandikia Dowans ikieleza kuwa, uhamishaji huo wa majukumu ya kiutendaji hayakuwa halali.

Novemba 2, mwaka jana, Dowans ilifungua kesi katika mahakama hiyo ya kimataifa ikidai kiasi cha dola za Kimarekani 109,857,686 kama gharama za huduma za umeme ambazo zilikuwa hazijalipwa.

Aidha, Desemba 11, mwaka jana, Tanesco iliwasilisha maombi ya kuomba iongezewe muda wa kuwasilisha utetezi wake katika mahakama hiyo, lakini kabla kesi hiyo haijafikia mwisho, Dowans ilitangaza kuiuza mitambo yake.

Kitendo hicho kilikuwa na lengo la kuvuruga namna ya ukazaji wa hukumu itakayotolewa na mahakama hiyo ya kimataifa juu ya gharama za kuendesha kesi hiyo kwa upande wa Tanesco.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis, Mei 14,2009

No comments:

Powered by Blogger.