Header Ads

LIYUMBA AITIKISA SERIKALI

Na Happiness Katabazi

‘FILAMU’ ya kumkamata na kukumuachilia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, jana iliendelea tena baada ya mshitakiwa huyo kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka mapya.

Liyumba alifikishwa mahakamani hapo jana, majira ya saa 8:00 mchana, chini ya ulinzi wa polisi akiwa amepakizwa kwenye gari aina ya Yundai, yenye namba za usajili T 450 ARU ambalo lilikuwa likiongozwa na Defender lenye namba za usajili T 220 AMV na Land Cruiser yenye namba T 120 AZD.

Baada ya kushushwa, mshitakiwa huyo alipitishiwa mlango wa nyuma na kisha kuingizwa kwenye chumba cha Mwendesha Mashitaka Mkuu Kanda ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Kenyela alikokaa kwa dakika takriban 20.

Baadaye, alitolewa na kuingizwa katika mahakama ya wazi kwa ajili ya kusomewa mashitaka mapya.

Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila, akisaidiana na John Wabuhanga na Justus Mlokozi mbele ya Hakimu Mkazi, Nyigumalila Mwaseba, alidai kuwa Liyumba amefungulia kesi mpya ya jinai yenye mashitaka mawili na imepewa namba 105/2009.

Katika shitaka la kwanza, Liyumba anakabiliwa na kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo anadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006, akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Mwangamila alidai kuwa, shitaka la pili ni kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 kwa uamuzi wake wa kuidhinisha ujenzi wa minara hiyo pacha.

Hata hivyo, mashitaka hayo katika hati mpya yanafanana na yale waliyoshitakiwa katika hati ya mashitaka iliyofutwa na kilichobadilika ni yeye kushitakiwa kwa makosa mawili wakati hati ya mashitaka ya awali ilikuwa na mashitaka matatu.

Hata hivyo, Liyumba alikana mashitaka yote, lakini upande wa mashitaka uliiomba mahakama itoe dhamana kwa mujibu wa kifungu Na. 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho 2002.

Kifungu hicho kinasema ili mshitakiwa apate dhamana, lazima awasilishe mahakamani nusu ya fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya nusu ya mali ya mtuhumiwa anayodaiwa kuiba.

Hata hivyo, kiongozi wa jopo la mawakili linalomtetea Liyumba, Majura Magafu, aliibua hoja mpya ya kisheria akidai kuwa kifungu hicho hakipaswi kutumika katika kesi hiyo.

Akiwasilisha hoja hiyo, Magafu aliiambia mahakama kuwa, mashitaka yanayomkabili mteja wake ni ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia hasara serikali na kuongeza kuwa, kifungu hicho kinasema masharti hayo yatatumika kwa mshitakiwa anayetuhumiwa kuiba au mali inayoonekana ya mamlaka husika yenye zaidi ya thamani ya sh milioni 10.

“Shitaka la kusababisha hasara halimaanishi mteja wangu alichukua sh bilioni 221 za BoT au mali yenye thamani hiyo.

“Kwa kuwa upande wa mashitaka umetaka tuwakumbushe historia ya kifungu hicho kilianzia wapi, nalazimika kuwakumbusha;

“Ni hivi, kifungu hicho kiliingizwa kwenye Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, baada ya miaka ya 1980 baada ya serikali ya awamu ya kwanza kutangaza vita dhidi ya wahujumu uchumi na serikali ilisema, kama mtu anatuhumiwa kuiba zaidi ya milioni 10, na miaka michache baadaye ndiyo kifungu hicho kiliingizwa kwenye Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kuanza kutumika.

“Hakimu, ni rai yetu kwamba hiki kifungu cha 148(5)(e) cha CPA kisitumike kabisa kwenye kesi hii kwani mteja wangu hakuiba fedha wala mali…na hiki kifungu ni mtego wa panya, na katika uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Daud Pete dhidi ya DPP ya mwaka 1991, mahakama ilikataa sheria za nchi kutumika kama mtego wa panya,” alidai Magafu.

Aidha Magafu alidai wanasikitishwa na upande wa mashitaka kutaka kutumia kifungu hicho kwa ajili ya dhamana, kwani ni hatari kwa watumishi wa umma ambao wamestaafu baada ya kulitumikia taifa kwa uaminifu. Lakini kwa sababu ya chuki tu, wanaamua kutumia kifungu hicho ili kuwatesa.

Hakimu Mwaseba aliamua kuahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya kutoa uamuzi kuhusu utata wa masharti hayo ya dhamana.

Baada ya kuahirishwa, Liyumba alichukuliwa na maofisa usalama na kuingizwa kwenye gari lililomleta na kisha kupelekwa mahabusu.

Juzi, Hakimu Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba 27/2009 iliyokuwa ikimkabili Liyumba na Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, aliwaachilia huru baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa imekosewa, lakini muda mfupi baadaye walikamatwa tena mahakamani hapo.

Wakati huo huo, vyanzo vya kuaminika toka Makao Makuu ya Takukuru na Jeshi la Polisi, vimelihakikishia gazeti hili kuwa, Kweka ambaye awali alishitakiwa na Liyumba kwenye kesi ya jinai namba 27/2009, iliyofutwa na mahakama hiyo, anaendelea kuhojiwa na maofisa wa Takukuru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 29, 2009

No comments:

Powered by Blogger.