Header Ads

ZOMBE:DPP ANANITEKETEZA

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA namba moja katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wanne wa madini, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe, jana aliieleza Mahakama Kuu kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Elieza Feleshi, ana lengo la kumteketeza katika kesi hiyo.

Zombe alitoa kauli hiyo huku akionyesha hali ya masikitiko mara baada ya kupanda kizimbani kutaka kutoa utetezi wake kwa mara ya pili.

Alitoa kauli hiyo baada ya wakili wake, Jerome Msemwa kumwomba Jaji Salum Massati amruhusu mteja wake ajitetee kwa mara nyingine, hoja iliyoibua mvutano wa kisheria mahakamani hapo.

Baada ya kutokea hali hiyo, Jaji Massati alimwamuru Zombe kuteremka kizimbani baada ya wakili Majura Magafu kuhoji kama sheria inaruhusu kwa mtuhumiwa kurudia kutoa ushahidi wake pasipo kuathiri mwenendo wa kesi.

“Hili suala lisichukuliwe kiurahisirahisi, isifikie pahala pa ku-recal (kuwaita upya) mashahidi wote wa kesi hii,” Magafu alitoa angalizo.

Kabla Zombe hajateremka kizimbani baada ya mvutano huo, alimwomba jaji ruhusa walau aseme jambo na aliporuhusiwa kufanya hivyo, alidai: “DPP anataka kuniteketeza kabisa. Hii ni mahakama tukufu inayotoa haki ila alichonifanyia DPP anataka kuniteketeza kabisa.”

Wakili wa serikali katika kesi hiyo ya jinai, alitoa shinikizo Zombe kutojitetea kwa nyaraka zilizokwishakubalika kutotumika mahakamani hapo na kwamba kwa upande wao hawakuwa wamejiandaa katika suala hilo.

Hata hivyo, wakili Msemwa alieleza kuwa mashitaka dhidi ya mteja wake huyo ni ya kutengenezwa na DPP na kuiomba mahakama isimnyime haki ya kujitetea.

Msemwa alipingana na Magafu juu ya kuwapo uwezekano wa kuathiri mwenendo wa kesi hiyo iwapo Zombe angejitetea kwa madai kuwa hali hiyo haiwezi kutokea.

Kutokana na mabishano hayo baina ya mawakili katika kesi hiyo, Jaji Massati alifunga suala hilo na kuahidi kulitolea uamuzi leo, iwapo Zombe atajitetea kwa mara nyingine au la.

Katika hatua nyingine, shahidi wa Zombe, ambaye ni mkuu wa gereza la Ukonga, ACP Samweli Nyakitina, alishindwa kuzikubali ama kuzikataa sahihi na mihuri ya ofisi yake kwa barua za mahabusu na wafungwa zilizokwenda nje ya gereza hilo.

Aliikataa pia barua ya pili iliyoandikwa na Zombe kwenda kwa Waziri wa Katiba na Sheria iliyohusu suala la kubambikiwa kesi na DPP kwa madai kuwa haikuwa na mhuri na haamini sahihi iliyowekwa katika barua hiyo.

Wakili Msemwa alipomuuliza mkuu huyo wa gereza iwapo katika kumbukumbu zake alishawahi kukutana na kusaini barua hiyo, alijibu kuwa kutokana na idadi kubwa ya wateja wa gereza hilo, inayokadiriwa kufikia zaidi ya 2,000, hawezi kukumbuka iwapo alishasaini barua kama hiyo mwaka 2006.

Shahidi huyo alidai kuwa, baada ya kufanyika kwa upekuzi wa wafungwa na mahabusu katika gereza hilo, walikuta simu nne alizokuja nazo kama vithibitisho na sh 153,000, vyote hivyo vikitoka kwa mahabusu 30, waliokwenda mahakamani siku hiyo na wafungwa 1,000 waliokwenda kazini.

Mara baada ya Wakili wa Serikali, Mugaya Mutaki kumaliza kumhoji shahidi huyo, aliwataka mawakili wengine wamhoji, lakini hakuna aliyemhoji, jambo lililoibua miguno miongoni mwao na watu waliofika kushuhudia kesi hiyo hadi Jaji Massati alipohairisha kesi hiyo.

Awali, mshitakiwa wa 13, Koplo Festus Gwasabi, akitoa ushahidi wake, alidai kuwa hapakuwepo mapambano ya silaha wakati walipowakamata majambazi katika eneo la Sinza Palestina, na kwamba alishangaa kusikia vyombo vya habari vikiripoti kuwa tukio hilo lilikuwa la kujibizana kwa risasi.

Alidai kuwa, siku ya tukio, akiwa pamoja na wenzake na gari aina ya Toyota Stout, waliwapeleka wenzao katika eneo la Salender Bridge na wakati wakirudi Survey, walipata taarifa kutoka kwa Sajenti James kuwa kulikuwa na tukio la ujambazi katika Barabara ya Sam Nujoma.

Aliieleza mahakama kuwa, baada ya kufika katika tukio hilo walikuta lori la Kampuni ya BIDCO likiwa limepaki katikati ya barabara na kuwakuta watu wanne waliowaeleza kuwa wamevamiwa na kuwachukulia kiasi cha sh milioni tano.

Baada ya tukio hilo, alidai kuwa Januari 15, waliitwa kwa Zombe kupongezwa kwa kufanikisha ukamataji wa majambazi hao kwani ni sifa kwa jeshi hilo, lakini alishangaa kuhusishwa katika tukio hilo.

Alikataa kuwa alishiriki katika mauaji ya wafanyabiashara haoa na kwamba hakukimbia hata baada ya kusikia mauaji hayo na yeye kutajwa kuhusika. Kesi hiyo itaendelea tena leo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 5,2009

No comments:

Powered by Blogger.