Header Ads

KESI YA MAHALU YAKWAMA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, jana ilishindwa kuanza kusikiliza utetezi wa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Meneja Utawala na Fedha, Grace Martin kwa sababu washitakiwa hao wamewasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam, ifanye mapitio ya mwenendo mzima wa kesi hiyo.

Hakimu Sivangilwa Mwangesi alisema ameamua kuahirisha kesi hiyo na kusimamisha usikilizwaji wake hadi hapo ombi la washitakiwa lililopelekwa Mahakama Kuu litakapoamuliwa.

Kabla ya kuahirisha kesi hiyo jana asubuhi, wakili wa utetezi Mabere Marando, anayesaidiana na Alex Mgongolwa, Bob Makani na Cuthbert Tenga, aliiambia mahakama hiyo kuwa Aprili 30, mwaka huu, waliwapa maombi upande wa mashitaka ya kutaka wapatiwe nyaraka halisi za mawasiliano yaliyokuwa yakifanywa na washitakiwa wakati wapo kwenye nyadhifa zao katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Italia na serikali ili wateja wake waweze kuzitumia wakati wa kutoa ushahidi wao.

Baada ya Marando kumaliza kutoa hoja hizo, wakili Tenga aliinuka na kuiambia mahakama hiyo kuwa, Aprili 29, mwaka huu, walifungua kesi ya jinai ya kutaka mahakama hiyo ipitie mwenendo wa kesi hiyo ambapo hata hivyo, Mahakama Kuu imesema haiwezi kuipangia jaji au kutoa hati ya washitakiwa kuitwa mahakamani hadi wapeleke mwenendo wa kesi hiyo.

Hivyo, anaomba mahakama hiyo iwapatie mwenendo wa kesi hiyo ili waweze kuupeleka.
Mahalu na Grace wanaiomba kesi hiyo ipitiwe na Mahakama Kuu kwa madai kuwa Mahakama ya Kisutu imekuwa ikiendesha kesi hiyo bila ridhaa ya DPP kama sheria inavyotaka.

Katika ombi la pili, wanaomba mahakama hiyo ipitie uamuzi wa Mahakama ya Kisutu ya kupokea mkataba kivuli wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, kinyume na utoaji wa nyaraka halisi mahakamani kwa madai kwamba ilifikia uamuzi wa kupokea mkataba kivuli kwa sababu ilikuwa ikifungwa mikono na sheria za Italia.

“Hakimu alitumia sheria za Italia ambapo sheria yenyewe ya Italia haikutajwa kwenye uamuzi wake uliosema Mahakama ya Kisutu inafungwa mikono na sheria za Italia,” alidai Tenga.

Ombi la tatu wanalotaka mahakama hiyo ipitie ni uamuzi wa hakimu Mwangesi wa kusikiliza ushahidi kwa njia ya video. Tenga alidai kwa mujibu wa kifungu cha 40A ya Sheria ya Ushahidi inakataza mahakama kupokea ushahidi wa shahidi asiyepo mahakamani.

“Tunapinga ushahidi wa shahidi huyo kuchukuliwa ushahidi wake kwa njia ya video kwani kufanya hivyo mahakama hiyo ilipokea ushahidi nje ya mipaka iliyoainishwa kisheria kuhusu mahakama hiyo ya mkoa, kwani Italia si sehemu ya mipaka ya Mahakama ya Kisutu, hivyo hatukuridhishwa na hilo na ndiyo maana tumepeleka ombi la kutaka kupitiwa kwa mwenendo mzima wa kesi ya hii,” alidai Tenga.

Aidha, ombi jingine la kutaka lipitiwe ni Aprili mwaka huu, kesi hiyo iliposikilizwa kwa njia ya video, Mwangesi alifunga ushahidi bila ya kutoa nafasi kwa pande zote katika kufunga ushaidi wa upande wa mashitaka.

Januari 2007, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washitakiwa hao walimdanganya mwajiri wao ambaye ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 3.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 5,2009

No comments:

Powered by Blogger.