Header Ads

LIYUMBA MWIBA MKALI

.Sasa apumua .aweza kutoka sero Juni Jumatatu

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, jana imelegezea masharti ya dhamana kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, ambaye anakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.


Hatua hiyo inatoa uwezekano mkubwa kwa mshitakiwa huyo, aliyesota mahabusu kwa siku 114, kuwa nje kwa dhamana Jumatatu ijayo - Juni Mosi mwaka huu, endapo atakamilisha masharti mapya ya dhamana.

Uamuzi wa kulegeza masharti ya dhamana mpya, ulitolewa jana na Hakimu Nyigumalile Mwaseba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambaye kabla ya kusoma uamuzi huo, alikumbusha kuwa katika shauri hilo dhamana ilikuwa haibishaniwi bali kilichokuwa kikibishaniwa ni masharti ya dhamana.

Kwa uamuzi huo, Liyumba sasa atatakiwa atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh milioni 300, wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh milioni 50 kila mmoja, kutotoka nje ya Dar es Salaam hadi kwa kibali maalum na kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani.

Masharti hayo ni tofauti na awali, ambapo alitakiwa awe na wadhamini wawili wa kuaminika, ambao wangesaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya nusu ya kiasi cha sh bilioni sh 221, anachotuhumiwa kuisababishia serikali hasara.

Sharti lingine la awali lilikuwa kuacha hati za kusafiria mahakamani, kuripoti katika ofisi za Takukuru kila siku ya Ijumaa na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibali cha mahakama.

Juzi, mawakili wa serikali, wakiongozwa na Justus Mulokozi, John Wabuhanga na Prosper Mwangamila, waliiomba mahakama itoe dhamana kwa mujibu wa kifungu Na. 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho 2002.
Kifungu hicho kinasema ili mshitakiwa apate dhamana, lazima awasilishe mahakamani nusu ya fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya nusu ya mali ya mtuhumiwa anayodaiwa kuiba.

Akitoa uamuzi ambao umemfanya Liyumba apumue, Hakimu Mwaseba alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kulazimika kukubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kwamba, ni kweli kifungu hicho kamwe hakipaswi kutumika katika mashitaka mapya yanayomkabili mshitakiwa huyo.

Alisema, hakuna ubishi kwamba mashitaka yanayomkabili Liyumba ni yale ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia hasara serikali ya sh bilioni 221, hivyo mashitaka hayo ni tofauti kabisa na yanayoainishwa kwenye kifungu hicho.

Akisoma kwa makini uamuzi huo, Mwaseba ambaye ni mmoja wa mahakimu vijana wa mahakama hiyo, alisema ameamua kutupa ombi la upande wa mashitaka la kutaka kifungu hicho kitumike kumpa dhamana Liyumba.

“Nakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kuwa kifungu hicho kamwe hakipaswi kutumika katika mashitaka yanayomkabili mshitakiwa na kwa sababu hiyo natupilia mbali ombi la upande wa mashitaka lililotaka mahakama hii itumie kifungu hicho katika kumpatia dhamana mshitakiwa na endapo upande wa mashitaka haujaridhika na uamuzi wake, unaweza kukata rufaa,” alisema Mwaseba na kusababisha mawakili wa serikali kujiinamia.

Baada ya kumaliza kutoa uamuzi huo, wakili Magafu aliomba mahakama kuahirisha kwa muda kesi hiyo hadi saa saba mchana jana ili mteja wake aweze kukamilisha masharti hayo.

Lakini wakili wa serikali, Mulokozi alipinga hoja hiyo kwa madai kuwa, wana shughuli nyingine na kupendekeza iahirishwe hadi tarehe nyingine.

Hata hivyo, Mwaseba alikubaliana na Mulokozi na kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu ijayo ambapo itakuja kwa ajili ya kukamilisha masharti ya dhamana na kama yatakamilika, Liyumba atakuwa nje kwa dhamana.

Baada ya hakimu kuondoka katika chumba cha mahakama, ndugu na jamaa wa Liyumba waliruka kwa furaha, huku wengine wakienda kizimbani kumbusu mshitakiwa huyo pamoja na kuwapongeza mawakili wake kwa kupambana katika kesi hiyo hadi kufikia hatua hiyo.

Wakati hayo yakifanyika, mawakili wa serikali walionekana kupooza na kuamua kubeba makabrasha yao na kuanza kuondoka.

Juzi, Liyumba alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka upya ambapo wakili wa serikali, Mwangamila, alidai kuwa kesi hiyo ya jinai imepewa namba 105/2009 na ina mashitaka mawili tofauti na awali ambapo ilikuwa na mashitaka matatu.

Kwa mujibu wa Mwangamila, katika shitaka la kwanza, Liyumba anakabiliwa na kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo anadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006, akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Mwangamila alidai kuwa, shitaka la pili ni kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 kwa uamuzi wake wa kuidhinisha ujenzi wa minara hiyo pacha.

Liyumba alisomewa mashitaka mapya baada ya Hakimu Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba 27/2009 iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa huyo na Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, kuwaachia huru baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa ina makosa kisheria.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, Liyumba na Kweka walikamatwa tena na Liyumba kusomewa mashitaka mapya, huku Kweka akiendelea kuhojiwa na Takukuru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Mei 30,2009

No comments:

Powered by Blogger.