Header Ads

MRAMBA APUNGUZIWA SHITAKA

*Ni lile linalohusu mapendekezo ya TRA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7, inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, umebadilisha hati ya mashitaka baada ya kufutwa kwa shitaka moja.
Shitaka lililofutwa, linamhusu Mramba peke yake, hivyo anabaki na mashitaka 11 badala ya 12.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Daniel Yona, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na Katibu Mkuu mstaafu Wizara ya Fedha na Uchumi, Grey Mgonja.

Ombi hilo la kubadilishwa hati ya mashitaka liliwasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana na wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, akisaidiana na Fredrick Manyanda na wanasheria toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Tabu Mzee, Beni Linkoni na Joseph Holle.

Wakati Boniface akiwasilisha ombi hilo mbele ya jopo la mahakimu wakazi watatu, linaloundwa na John Utamwa, Saul Kinemela na Fatma Masengi, hakuweka wazi sababu za upande wa mashitaka kufikia uamuzi huo.

Shitaka hilo la tano, awali lilikuwa likisomeka kuwa, Oktoba 10, 2003, mshitakiwa huyo (Mramba), akiwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka yake vibaya kwa kudharau mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ambayo yalikataza Kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation, isipewe msamaha wa kodi.

Baada ya ombi hilo kuridhiwa na jopo hilo la mahakimu, upande wa mashitaka uliiomba mahakama iwaruhusu kuwasomea upya maelezo ya awali washitakiwa, ombi ambalo lilizua malumbano makali ya kisheria kati ya upande wa mashitaka na wakili wa upande wa utetezi, Profesa Leonard Shaidi.

Profesa Shahidi ambaye alikuwa akisaidiana na Hurbet Nyange na Joseph Tadayo, walipinga ombi hilo wakidai kuwa hawapo radhi wateja wao wasomewe maelezo ya awali bila upande wa mashitaka kuwapatia nyaraka walizopanga kuzitumia kwenye kesi hiyo.

“Waheshimiwa mahakimu, kabla ya upande wa mashitaka kuwasomea wateja wetu maelezo ya awali, tunaomba watupatie nyaraka walizopanga kuzitumia kwenye kesi hii kwa sababu sheria inataka hivyo, kwa hiyo tunaomba mahakama iwaamuru kufanya hivyo,” alidai Profesa Shaidi.

Akijibu pingamizi hilo, Boniface alidai si lazima kisheria upande wa mashitaka utoe nyaraka hizo kwa upande wa utetezi.

Malumbano hayo ambayo yalidumu kwa takribani robo saa, yalisababisha kiongozi wa jopo hilo la mahakimu wakazi, Utamwa, kuahirisha kesi hiyo hadi Alhamisi wiki hii ambapo mahakama itatoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo.

Aprili 17, mwaka huu, Mramba ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, kupitia wakili wake, Nyange mbele ya Hakimu Mkazi, Henzron Mwankenja, alikiri kutoa vibali vya msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo na kwamba alifanya hivyo baada ya kuagizwa na Ikulu.

Awali, akisoma maelezo ya awali dhidi ya washitakiwa hao, mwanasheria wa Takukuru, Joseph Holle alidai kuwa washitakiwa hao wakiwa na nyadhifa hizo serikalini, walikuwa na jukumu la kuwa waaminifu na makini katika majukumu waliyokabidhiwa kisheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 19, 2009

No comments:

Powered by Blogger.