Header Ads

MAHAKAMA 'YAMTOSA' ZOMBE

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ililifukuza ombi la mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya Wafanyabiashara wanne wa madini, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe, la kutaka aruhusiwe kujitetea kwa mara ya pili.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati ambapo juzi alipokea ombi la Zombe la kutaka aruhusiwe kutoa ushahidi kwa mara ya pili na akaaidi kuwa jana angetoa uamuzi kuhusiana na ombi hilo.

Jaji Massati akitoa uamuzi wake alisema amefikia uamuzi wa kufukuza ombi hilo la Zombe lilowasilishwa kupitia wakili wake Jerome Msemwa, alisema kifungu Na.147(4) cha Sheria ya Ushahidi ya mwaka 2002 ina ipa mamlaka mahakama hiyo kumruhusu mshitakiwa ajitete kwa mara ya pili .

“Licha kifungu hicho pia akiilazimishi mahakama kuruhusu au kutomruhusu mshitakiwa mshitakiwa kutoa ushahidi kwa mara ya pili lakini uhuru huo wa mahakama unaweza kutumika katika mazingira maalum ili kukidhi maswala yaliyojitokeza ambayo hayakutalajiwa na kama kumruhusu huko au kutomruhusu hakutaathiri haki za washtakiwa wengine katika kesi husika.

“Hakuna shaka Zombe alishaleta barua zilizoandikwa toka gereza Ukonga kwenda kwa aliyekuwa DPP-Geofrey Shaidi lakini wakati alipokuwa akitoa ushahidi wake, hakufanya jaribio lolote la kuzitoa barua hizo kama vielelezo na upande wa mashtaka ulipomuhoji kwa undani kuhusu barua hizo , kulionekana mapungufu ya wazi katika barua alizotaka kuzitoa na zile zilizopokelewa na aliyekuwa DPP-Shahidi” alisema Jaji Massati.

Jaji Massati washtakiwa wote wakati wakijitetea walishazikana hizo barua zinazodaiwa na Zombe kwamba waliziandika gerezani na kuzipeleka kwa DPP bila kufuata taratibu,kwa hiyo hakuna sababu za msingi zilizotolewana wakili wa Zombe kwamba ni kwanini alishindwa kuzitoa barua hizo wakati akijitetea.

“Kama Zombe akiruhusiwa kujitetea kwa ya pili basi washtakiwa wengine watakuwa na haki ya kuomba nao waruhusiwe kujitetea kwa mara ya pili na endapo hilo litatokea ni wazi kabisa hali hiyo itasababisha kuvurugika kwa mwenendo mzima wa kesi hii na kwasababu hiyo natupilia mbali ombi Zombe lakutaka aruhusiwe kujitetea tena” alisema Jaji Massati.

Baada ya kutoa uamuzi huo Jerome Msemwa Msemwa aliinuka na kusema Zombe hatakuwa na shahidi mwingine hivyo kwa upande wake wanafunga ushahidi na wakili Denis Msafiri nao waliambia mahakama hiyo kuwa hawatakuwa na mashahidi.

Isipokuwa wakili wa mshitakiwa wa pili, Diougras Ishengoma alidai kuwa wao wanashahidi mmoja ila kwajana alishindwa kufika mahakamani hapo kwakuwa amepata dhalula ila akaiomba mahakama kuwa shahidi huyo atafika leo kujitetea na wakili Myovela alisema wanashahidi mmoja naye atafika leo.

Ndipo Jaji Massati akasema kutoka na taarifa hiyo mshitakiwa 1,3,5,7,9,10 na 12 wamefunga ushahidi isipokuwa mshitakiwa pili(ASP)-Christopher Bageni na 13,Koplo Festus Gwabisabi, bado hawajafunga ushahidi wao kwasababu mashahidi wao watafika leo kutoa ushahidi.

Mbali ya Zombe washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka wilayani Ulanga, Morogoro, na dereva teksi mmoja, ni pamoja na SP Christopher Bageni, SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwabisabi.

Zombe na wenzake,wanadaiwa kufanya mauaji hayo Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, ambapo waliwaua, Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Mei 6,2009

No comments:

Powered by Blogger.