Header Ads

WAKILI AHAHA KUMWOKOA ZOMBE

*Watumia zaidi ya saa sita kutoa hoja mahakamani
*Waomba washitakiwa waachiwe ushahidi ni dhaifu

Na Happiness Katabazi

MAWAKILI wa utetezi katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (ACP), Abdallah Zombe na wenzake, jana walikuwa na kibarua kibarua kizito cha kuhakikisha wanawanasua wateja wao katika kesi hiyo.

Walikuwa wakiwasilisha majumuisho ya ushahidi katika kesi hiyo baada ya washitakiwa kumaliza kutoa ushahidi wao na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuufunga.

Mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Massati, mawakili hao kwa nyakati tofauti walianza kuwasilisha hoja zao saa 4:20 asubuhi na kumaliza kazi hiyo saa 11:19 jioni.
Waliiomba mahakama hiyo kuwaachia huru wateja wao kwa kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo umejaa mkanganyiko mkubwa na pia ni wa kuungaunga.

Pia walisema mashahidi katika kesi hiyo wameshindwa kuthibitisha kama washitakiwa hao walihusika kufanya tukio hilo la mauaji, Januari 14, mwaka 2006.

“Tunaomba wateja wetu waachiliwe huru kwa kuwa hati ya mashitaka inasema mauaji yalifanyika msitu wa Pande, lakini kuna baadhi ya mashahidi walieleza yalifanyika Sinza Ukuta wa Posta. Kwa sababu hiyo, upande wa mashitaka umeshindwa kupeleleza kesi hii kwa umakini na matokeo yake ikaamua kutumia mtego wa panya wa kukamata hata wasiohusika,” alidai wakili Majura Magafu.

Wakili Jarome Msemwa ambaye anamwakilisha Zombe, alidai kitendo cha mteja wake kutoa taarifa za mauaji ya watu hao kwenye vyombo vya habari, si kosa, kwani alifanya hivyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa askari wake wa chini.

“Hivyo, Zombe alikuwa akiripoti tukio hilo tu, hakuwa mpelelezi na wala hakuwa na mamlaka ya kuwakamata wale marehemu na ndiyo maana alipofika ndugu wa marehemu pale ofisini kwake, aliamuru apelekwe kituo cha polisi Oysterbay kwa sababu askari wa kituo hicho ndio walikuwa wakishughulika na marehemu,” alidai Msemwa.

Kuhusu hoja ya mteja wake kufika Kituo cha Urafiki Januari 15, Msemwa alidai alifanya hivyo baada ya kuitwa na SSP Mantage na kuelezwa tukio zima, na kwamba kama Zombe alikuwa na nia mbaya angechukua sh milioni tano zilizopatikana katika tukio hilo.

Alidai kuhusu maelezo ya aliyekuwa mshitakiwa wa 11, marehemu Rashid Lema, kuwa walipokuwa barabara ya Sam Nujoma alimsikia Bageni akizungumza na simu akiitikia ndiyo afande, wakili huyo alieleza ushahidi huo ni wa kusikia na kamwe hauthibitishi kwamba siku hiyo alikuwa akizungumza na Zombe.

Pia alidai kuhusu Zombe kutoa mkono wa pongezi kwa askari hao, ni kitendo cha kawaida kama ofisa anaridhika na taarifa za askari wake na kuongeza kuwa Zombe hakufanya hivyo kwa ridhaa yake bali kwa mujibu wa utartibu wa Jeshi la Polisi.

“Unaposema mtu kaua ni lazima uonyeshe ushahidi na si vinginevyo, sasa hakuna hata shahidi aliyeweza kuithibitishia mahakama hii kama Zombe aliua watu hao…kilichofanyika Zombe aingizwe kwenye kesi hii ni hatua yake ya kutoa mkono wa pongezi kwa askari na kwenda Urafiki tu,” alidai.

Wakili Msemwa alidai kuhusu baadhi ya washitakiwa kuwa na vikaratasi vilivyoandikwa maelekezo na mteja wake ili wakatoe maelezo ya uongo mbele ya Tume ya Jaji Musa Kipenka, alidai hakuna mshitakiwa aliyeweza kuthibitisha suala hilo kwa vielelezo.

Alieeleza kuwa kesi hiyo imepikwa na magezeti, hali iliyoifanya jamii kumuona mteja wake kuwa ni muuaji na kwamba ni lazima atahukumiwa kunyongwa.

“Lakini hata Yesu alisulubiwa na kudhihakiwa kwamba si mwana wa Mungu, lakini baada ya mateso makali ndipo watesi wake waliamini Yesu ni mwana wa Mungu, hivyo mfano huo naufananisha na mteja wangu ambaye anasulubiwa bila hatia,” alidai Msemwa. Kwa upande wake, wakili wa mshitakiwa wa pili (Christopher Bageni), Ishengoma, alidai kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa, mteja wake hana hatia, kwani kesi hiyo imejengeka katika ushahidi wa mazingira na hakuna ubishi kwamba marehemu walikamatwa Sinza A.

Wakili huyo alidai kuwa, ushahidi uliotolewa na mshitakiwa wa 12, Rajabu Bakari, kwamba siku ya tukio Bageni alipata taarifa za tukio hilo kupitia ‘radio call’, ni uongo na kueleza kuwa anachokifanya mshitakiwa huyo ni kujinasua katika kesi hiyo.

“Rajabu ni muongo na anachokifanya ni kutaka kujinasua aonekane hakushiriki kwenye tukio hilo, kwa kifupi naomba mahakama hii imuone mteja wangu kuwa hana hatia, kwani hata ushahidi uliotolewa ni wa kusikia na wala hauonyeshi kama Bageni alikuwepo kwenye tukio,” alidai.

Aidha, Wakili Magafu ambaye anawawakilisha washitakiwa wa 3, 5, 7, 9 na 10, alidai katika kesi hiyo kuna mkanganyiko mkubwa uliosababishwa na upande wa mashitaka kwa sababu ulikosa umakini na kwamba wapelelezi wa kesi hiyo hawakufanya kazi yao kwa uadilifu.

Magafu akizungumza huku akipaza sauti, alidai ushahidi unaonyesha wazi kuwa marehemu walikamatwa eneo la Sinza, ila mkanganyiko umekuja na umefanya upande wa utetezi ujiulize maswali kuwa mauaji yalifanyika sehemu gani, kwani mashahidi wa upande wa mashitaka walidai kulikuwa na mapambano ya risasi eneo la Sinza, Ukuta wa Posta.

Magafu alidai mkanganyiko wa pili, ni wapi waliuawa marehemu hao, kwani upande wa mashitaka kwenye hati ya mashitaka unaeleza waliuawa msitu wa Pande, lakini mashahidi wanaeleza mapambano ya risasi yalifanyika Sinza.

“Ni mkanganyiko ulioletwa na upande wa mashitaka na swali linabaki, hawa watu waliwaulia wapi? Na mahakama haitakiwi kubebeshwa mzigo wa kujibu swali hilo.

Wanaotakiwa kuthibitisha ni wapi waliuliwa ni upande wa mashitaka na hadi sasa wameshindwa kuonyesha hilo,” alidai Magafu na kuomba mahakama kuwaachia huru wateja wake.

Kwa upande wao mawakili wa mshitakiwa wa 13 na 12, Myovela na Denis Msafiri nao pia waliomba wateja wao waachiliwe huru, kwani hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa walitenda kosa.

Baada ya mawakili wa utetezi kumaliza kuwasilisha hoja zao, Jaji Massati aliwataka mawakili wa upande wa mashitaka nao kuwasilisha hoja zao, lakini walimuomba jaji kuahirisha kesi hiyo hadi leo.

Hata hivyo, Jaji Massati alisema kwa mujibu wa ratiba ya kikao cha kesi hiyo, inaonyesha kuwa imemalizika jana, hivyo kuiahirisha mpaka itakapopangwa tena.

Mbali ya Zombe na Bageni, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasabi.

Wahsitakiwa hao wanadaiwa Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, waliwaua Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 8,2009

No comments:

Powered by Blogger.