Header Ads

LIYUMBA AIZIDI AKIRI SERIKALI MAHAKAMANI

*Yeye, Kweka wafutiwa mashitaka, dola yawakamata
*Furaha ya ndugu zao yadumu kwa dakika tano tu
*Waandaliwa mashitaka mapya, kutinga kortini leo

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilimwachilia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Mradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka, baada ya kubaini hati ya mashitaka imekosewa.

Lakini wakati Liyumba na mwanzeke wakifurahia uamuzi huo, walikamatwa tena na makachero wa polisi waliofurika mahakamani hapo, muda mfupi baada ya kuachiwa na kupelekwa katika kituo cha polisi Salender Bridge walikowekwa mahabusu.

Uamuzi wa kesi hiyo iliyovuta hisia za wengi kila ilipotajwa mahakamani, ulitolewa jana saa 4:47 asubuhi na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, baada ya kuahirisha kutoa uamuzi huo kwa mara tatu mfululizo.

Alisema amefikia uamuzi wa kuwaachia washitakiwa baada ya kukubaliana na maombi ya mawakili wa utetezi kuwa, hati ya mashitaka katika kesi hiyo, ina dosari za kisheria.

Februari 25, mwaka huu, wakili wa utetezi, Majura Magafu, ambaye alikuwa akisaidiana na Hudson Ndusyepo na Profesa Gamalieli Mgongo Fimbo, waliwasilisha maombi mahakamani hapo wakitaka wateja wao waachiliwe na kufutiwa mashitaka kwa madai kuwa kibali cha Mkurugenzi wa Mahitaka (DPP), kilichotumika kufungua kesi hiyo, kina makosa.

Pia walidai kuwa, shitaka katika kesi ya msingi, namba 27/2008, linalodai kuwa washitakiwa hao waliisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, halionyeshi ni aina gani ya kosa lililotendwa na watuhumiwa hao.

Alisema shitaka hilo limeandaliwa kinyume na kifungu cha 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Lema akisoma uamuzi huo, alisema kisheria hati ya mashitaka ndiyo inayojenga msingi wa kesi yoyote iliyopo mbele ya mahakama, hivyo inapobaini kuwa ina dosari za kisheria, inalazimika kuifuta na kisha kuwaachilia huru washitakiwa.

“Baada ya kupitia kwa kina hoja za pande zote mbili, mahakama hii inakubaliana na maombi ya utetezi kuwa, hati hiyo ina dosari na kwamba kosa la tatu halionyeshi ni kosa gani limetendwa na washitakiwa, hivyo nawaachia washitakiwa chini ya kifungu Na. 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai 2002.

“Nimewaachilia huru washitakiwa chini ya kifungu hicho baada ya mahakama kubaini kuwa hati ya mashitaka iliyofikishwa mahakamani na upande wa mashitaka ni ‘hopeless’,” alisema Lema na kusababisha makachero waliokuwa wameketi viti vya nyuma, kuanza kusogea karibu na kizimba waliposimama washitakiwa ili kuwakamata tena.

Tangu saa moja asubuhi, makachero hao kutoka Idara ya Usalama wa Taifa, Takukuru na Polisi, walikuwa wamezingira mahakama hiyo, huku makachero wa polisi toka Kitengo cha Kupambana na Ujambazi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ambao waliliambia gazeti hili kuwa walikuwa na taarifa za washitakiwa kuachiwa huru, wakiwa wamebeba silaha aina ya SMG, tayari kwa ajili ya kuwakamata washitakiwa hao.

Mara baada ya Lema kumaliza kutoa uamuzi wake, maofisa usalama walimwamuru Liyumba na Kweka washuke kizimbani na kuwataka waketi kwenye viti vinavyotumiwa na mawakili wakati wakiendesha kesi mahakamani hapo.

Washitakiwa hao ambao walionekana kuwa na furaha, walitii amri hiyo, kisha Mwendesha Mashitaka Mkuu Kanda ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Charles Kenyella, aliutangazia umati wa watu uliofurika kufuatilia kesi hiyo, kutoka nje ili maofisa usalama hao na mawakili wa utetezi, wabaki na washitakiwa.

Baada ya umati huo kutoka, ndipo maofisa hao wakiwamo wa Jeshi la Magereza, waliwakabidhi rasmi watuhumiwa hao mikononi mwa polisi.

Ilipofika majira ya saa 5:28 asubuhi, polisi waliwapakiza watuhumiwa hao kwenye gari la polisi aina ya Defender lenye namba za usajili T 337 AKV, huku maofisa usalama wengine wakipanda kwenye gari aina Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 319 ATD na kuwapeleka katika Kituo cha Polisi cha Salender Bridge, chini ya ulinzi mkali, na kuwaacha ndugu na jamaa wa washitakiwa hao, wakipigwa na butwaa.

Licha ya wanausalama kufurika mahakamani hapo, pia ndugu na jamaa wa washitakiwa hao walifurika kwa wingi kusikiliza hukumu hiyo, huku eneo lote la mahakama linalotumika kuegeshea magari, likiwa limefurika magari.

Baadhi ya ndugu wa washitakiwa hao, walishindwa kuficha hisia, kwani walikuwa wakibubujikwa na machozi, huku wengine sura zao zikiwa zimejawa na simanzi.

Dalili za Liyumba kuachiwa na kukamatwa tena, zilionekana tangu uamuzi wa kesi hiyo ulipokuwa ukiahirishwa kutokana na idadi kubwa ya watu wa usalama na polisi waliokuwa wakifurika kwenye kesi hiyo.

Awali, Aprili 23, mwaka huu, Lema alitupilia mbali ombi la utetezi lililowasilishwa mahakamani hapo na wakili Magafu, lililokuwa likiomba mahakama hiyo itumie kifungu 225(1-4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai 2002, kinachotamka kuwa, ndani ya siku 60, upelelezi katika kesi husika uwe umekamilika, vinginevyo ifutwe.

Lema katika uamuzi wake alisema, hatafuta kesi hiyo kwa sababu amebaini kuwa licha ya siku 60 kupita na upalelezi wa kesi hiyo kutokamilika, haoni kama haki za msingi za washitakiwa zimevunjwa, na alitoa amri ya kuongeza muda kwa upande wa mashitaka ili uweze kukamilisha ushahidi wake.

Machi 30, mwaka huu, Hakimu Mkazi Lema ndipo alipoanza kuendesha kesi hiyo baada ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo aliyeanza nayo awali, kujiondoa rasmi Januari 26, mwaka huu kwa madai kuwa jamii kupitia vyombo vya habari, imekuwa ikilalamikia dhamana ya Liyumba.

Februari 17, mwaka huu, hakimu Msongo alimwachia kwa dhamana Liyumba na kuibua utata kutokana na kutotimiza masharti.

Moja ya masharti ambayo hayakutimizwa na Liyumba, ni kuwasilisha mahakamani hati zenye thamani ya sh bilioni 55, wadhamini wawili wa serikali wakiwa na barua kutoka kwa waajiri wao na kukabidhi hati za kusafiria mahakamani hapo.

Siku hiyo, Liyumba aliwasilisha hati yenye thamani ya sh milioni 882, hati ya kusafiria ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, huku wadhamini wawili wakiwa hawana barua zilizosainiwa na mwajiri wao kama masharti yalivyotolewa na mahakama.

Na wakati hakimu Msongo akitoa dhamana hiyo, alipingana na masharti ya dhamana aliyoyaweka mwenyewe wakati washitakiwa walipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, na pia alipingana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambayo ilisikiliza maombi ya Liyumba ya kutaka wapunguziwe dhamana.

Lakini siku mbili baadaye, Msongo alitoa hati ya kukamatwa Liyumba na wadhamini wake baada ya kubainika hati 10 zilizotumika kumdhamini zilikuwa na makosa, na pia barua za wadhamini wake hazikuwa zimesainiwa na mwajiri wao na kwamba Liyumba alikuwa amewasilisha hati ya kusafiria iliyokwisha muda wake.

Liyumba na mwenzake walipanda kizimbani mara ya kwanza Januari 26 mwaka huu, wakikabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia hasara serikali.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili Mwandamizi wa Serikali, John Wabuhanga ambaye alikuwa akisaidiana na Fredrick Manyanda kuwa, washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka yaliyoisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Wakili Wabuhanga alidai kuwa, washitakiwa hao wanadaiwa kutumia vibaya fedha za umma kwa kuidhinisha ujenzi wa Minara Pacha ya BoT maarufu kama ‘Twin Tower’ na kwamba wanakabiliwa na mashitaka matatu.

Shitaka la kwanza linamkabili mshitakiwa wa kwanza, Liyumba, ambalo ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma. Kwamba kati ya mwaka 2001-2006, akiwa mwajiri wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha bila baraka za uongozi wa juu wa benki hiyo.

Shitaka la pili, linamkabili mshitakiwa wa kwanza peke yake, ambalo ni kuidhinisha malipo ya ujenzi huo bila kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Wabuhanga alidai kuwa, shitaka la tatu ni kuisababishia serikali hasara, ambalo liliwahusu washitakiwa wote ambapo wanadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006, wakiwa watumishi wa umma, kwa makusudi au kwa kushindwa kuwa makini na kazi yao, waliisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Msongo alisema ili mshitakiwa apate dhamana, ni lazima kila mmoja awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao watasaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya nusu ya kiasi wanachotuhumiwa kuisababishia serikali hasara.

Sharti jingine ni washitakiwa kuacha hati za kusafiria mahakamani na kila Ijumaa watahitajika kuripoti ofisi za Takukuru na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibali cha korti.

Nusu ya kiwango wanachodaiwa kuisababishia serikali ni sh bilioni 110, hivyo kila mmoja wao atapaswa kusaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya sh bilioni 50.

Wakati huo huo, vyanzo vya kuaminika toka Jeshi la Polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, vimeliambia Tanzania Daima kuwa, Liyumba atafikishwa mahakamani hapo leo na kusomewa mashitaka mapya kwa kuwa tayari hati ya mashitaka imeishaandaaliwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Mei 28, 2009

No comments:

Powered by Blogger.