Header Ads

'HADITHI' ZA RICHMOND ZAENDELEA MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya kashfa ya Kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond, inayomkabili Naeema Adam Gile katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa mara nyingine tena jana uliendeleza ‘hadithi’ zake kwa madai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.


Mbele ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, Wakili wa Serikali Michael Lwena, alidai kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya kutajwa na kwamba bado upelelezi haujakamilika hivyo kuiomba mahakama hiyo iiahirishe.

Hakimu Lema aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 30, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa tena.

Gile ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa, alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Januari 14, mwaka huu, na tangu wakati huo hadi jana, kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa kwa kile kinachodaiwa na upande wa mashitaka wakati kesi hiyo ikitajwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Januari 14, mwaka huu, ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka matano ambayo aliyatenda kwa nyakati tofauti.

Wakili Boniface alidai kuwa, Machi 13, 2006, Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa na dhamira ya kutenda kosa, alighushi hati ya nguvu ya kisheria (power of attorney) inayoonyesha imetolewa na Hamed Gile, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, kwamba amemruhusu kufanya shughuli za kampuni hiyo hapa nchini.

Alidai kwamba, shitaka la pili ni kutoa taarifa za uongo, kuwa Machi 20 mwaka 2006, katika eneo la Ubungo, Umeme Park, Barabara ya Morogoro, mshitakiwa alitoa hati hiyo ya nguvu ya kisheria inayomuidhinisha yeye kwamba ameruhusiwa kufanya kazi ya kampuni hiyo ya Marekani hapa nchini.

Aliendelea kudai kuwa, shitaka la tatu linalomkabili mtuhumiwa huyo ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma na kwamba Julai 20, 2004 eneo la Ubungo, Umeme Park, alitoa taarifa ya uongo kwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme (TANESCO), kwamba Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100 kwa Tanzania ili wajumbe wa bodi hiyo waweze kumpendekeza kupewa tenda ya kutoa huduma hiyo.

Katika shitaka la nne, Boniface alidai Juni, 2006 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango hicho ili apewe tenda hiyo.

Wakili Boniface alidai shitaka la tano ni kwamba Julai, 2006, ambapo mshitakiwa akifahamu na kwa ulaghai, alitoa hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, mwaka huo iliyokuwa ikimuonyesha kuwa ameruhusiwa na Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond, Hemed Gile, kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.

Gile amefikishwa mahakamani ikiwa ni takriban mwaka mmoja sasa baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuachia ngazi baada ya Tume Teule ya Bunge kubaini kuwa alihusika katika mchakato wa utoaji zabuni kwa Richmond.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Oktoba Mosi, 2009

No comments:

Powered by Blogger.