JAJI WARIOBA:TUSIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA
*Akiri taifa sasa linapoteza mwelekeo
*Aonya utitiri wa kesi za ufisadi mahakani
*Asema makundi ndani ya CCM yanaligawa taifa
*Asema kauli ya JK kuhusu kesi kubwa imemshtua
Na Happiness Katabazi
“TUWE na tahadhari kesi nyingi zinafunguliwa kwa msukumo wa kisiasa…lakini hata hivyo sitaingia kwa undani kuhusu kesi hizo zinazohusisha vigogo wa serikali kwani ziko mahakamani.
“Ila hatua ya kuwapeleka vigogo mahakamani inatia moyo kwamba vita ya ubadhirifu wa mali ya umma imewanyoa hata vigogo waliokuwa watumishi wa serikali.”
Hayo ni maneno yaliyotamkwa Jumanne ya wiki hii na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba(69), katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake Masaka, Dar es Salaam, ambapo katika mkutano huo alipata fursa ya kuzungumzia masuala yanayohusu mustakabali wa taifa na miaka 10 ya kifo cha Baba wa Taifa, Julius Nyerere.
Jaji Warioba alitoa tahadhari hiyo baada ya kuulizwa maswali mbalimbali na waandishi wa habari.
Moja ya swali aliloulizwa, ni nini mtazamo wake kuhusu wingi wa kesi za matumuzi mabaya ya madaraka kwa viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu.
Kwa kauli yake, Jaji Warioba alisema hataki kuingia kiundani kwa sababu kesi hizo ziko mahakamani.
Anasema hatua ya kuwafikisha baadhi ya vigogo mahakamani inatia matumaini kwa vile viongozi wanapopewa dhamana ya kusimamia masuala ya kijamii hujisahau.
‘Nimefikia hatua ya kutahadhari kuhusu kesi hizo kwani bado naona zoezi hilo linafanana na Oparesheni Mitumba iliyofanyika mwaka 1979 ambapo kamati ziliundwa na kukamata watu kisha kufikishwa mahakamani bila kufuata taratibu mahsusi za kisheria na mwisho wa siku serikali ilishindwa ikalazimika kuwalipa fidia watuhumiwa, kezi hizi zilikuwa maarufu sana,” anasea Jaji Warioba.
“Pia mwaka 1983 kulikuwa na operesheni ya kuwakamata wahujumu uchumi nayo ilikuwa na msukumo wa kisiasa tu, watu wengi walikamatwa na kufikishwa mahakamani, vilevile serikali ikajikuta inashindwa kesi na mwisho wa siku huingia hasara ya kuwalipa fidia,” anasema Jaji Warioba.
Anasema kwa mifano hiyo, serikali inapaswa kuwa makini zaidi hasa katika suala zima la ushahidi.
“Kutumia tume katika kuandaa kesi ni kazi bure, sina hakika kama tume hizi zinafanyakazi ipasavyo kwani tume nyingi zinafanyakazi kisiasa zaidi…nimesoma hukumu ya kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoa wa Dar es Salaam, ACP-Abdallah Zombe, na wenzake, iliyotolewa na Jaji Salum Massati , ni kweli watu wale wanne waliuawa hakuna ubishi lakini tume iliandaa ushahidi kwa kupewa siku kadhaa na aliyeiunda tume hiyo.”
“Nimeshangazwa na upelelezi wa tume hiyo kushindwa kumpata aliyeua watu wale kwani watuhumiwa wa ujambazi kwenye benki wanapoiba, polisi inawakamata haraka sana, lakini aliyeua watu wanne wameshindwa kumpata…haiingii akilini! Sasa sijui kesi ya Zombe ilipelekwa haraka kwa ajili ya kisiasa? Alisema Jaji Warioba kwa masikitiko.
Akitoa mfano wa kesi za wizi wa Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), anasema tume iliundwa kuchunguza wizi huo na kusisitiza kuwa si vyema kumuingiza Rais wa nchi kwenye maandalizi ya awali ya kesi kama kuunda tume na kutolea mfano kesi za EPA ambapo Rais alishauriwa kutoa amri ya watuhumiwa kurudisha fedha.
“Sasa sijui watuhumiwa hao walirudisha fedha hizi kwa misingi gani na ifike mahala tujiulize washtakiwa hao wakishinda kesi mtawarudishia nini na wakati fedha walizozirejesha zilishapelekwa kwenye matumizi mengine ya serikali kwenye sekta ya kilimo?” anasema Jaji Warioba.
Anasema alishtushwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa hivi karibuni, wakati akizungumza na taifa kupitia vyombo vya habari vya redio na televisheni kwamba kuna kesi tatu kubwa zipo mbioni kufikishwa mahakamani!
“Huu mtindo wa kumshauri Rais aseme hayo, mwisho wa siku washtakiwa wakishinda kesi, wale maofisa wa serikali waliokuwa wakimshauri Rais watamruka na watasema ni Rais ndiye aliyeagiza kesi hizo ziende mahakamani na si vyombo husika,” anasema Jaji Warioba.
Anasema ana wasiwasi kama Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu Hesabu za Serikali kama zipo huru zaidi kutokana na kuzidiwa na maagizo mazito kutoka ngazi za juu.
Anasema kisheria ofisi hizo zinatakiwa kuwa huru na misingi ya kuzianzisha ilikuwa ni hiyo kuwa zifanye kazi kitaalum na siyo maagizo ya wanasiasa tu.
Akizungumzia hali ya mshikamano uliopo hivi sasa ndani ya taifa, Jaji Warioba anasema kuna dalili ya umoja wetu kuanza kusambaratishwa.
Anasema siku za nyuma Tanzania ilikuwa nchi yenye mshikamano na wananchi wote walikuwa wakiitana ndugu lakini hivi sasa wameanza kugawanyika katika vikundi.
“Miaka ya nyuma maskini walikuwa na sauti katika kuendesha nchi hii lakini leo matajiri ndiyo wenye sauti katika kuendesha nchi na leo hii uongozi wa nchi upo karibu mno na matajiri kuliko wananchi maskini,” anasema.
Anaendelea kusisitiza kuwa hata ndani ya serikali tayari kuna matabaka kati ya watumishi wa umma kwani kuna wafanyakazi wa umma wanaopata mishahara mikubwa na wengine midogo.
Anasema awamu zilizopita ziliweza kudhibiti hali hiyo tofauti na sasa.
Jaji Warioba anasema, zamani siri za serikali zilikuwa hazivuji lakini leo zimekuwa zikivuja kwa sababu ya kuwepo makundi kati ya waliyonacho na wasionacho.
“Hakuna kitu kilichonishangaza kama wakazi wa Ngorongoro kuandamana hadi Ikulu Septemba mwaka huu tena mchana kweupe, hebu tazameni kule Ngorongoro kuna safu ya uongozi tena kuanzia mjumbe wa nyumba kumi kumi hadi mkoa, lakini wananchi hao waliamua kufuata utaratibu wao wa kwenda Ikulu kutaka kuonana na Rais wa nchi tena bila hata kuomba kibali cha kupewa ahadi ya kuonana na rais, hali hii ni hatari,” anasema Jaji Warioba.
“Sasa katika hili lililofanywa na wakazi wa Ngorongoro tunaona wazi imani ya wananchi kwa viongozi wao haipo tena na hii inaendelea kutugawa kwenye matabaka kadri siku zinavyozidi kusonga mbele,” anasema Jaji Warioba.
Kuhusu tatizo la ukabila na udini ambalo limeanza kuligawa taifa, mwanasiasa huyo mkongwe anasema awali ukabila ulikuwa ukitumika kwenye utani wa makabila mbalimbali, lakini umeanza kuwagawa wananchi kikanda na kikabila na siyo kitaifa.
Anasema tatizo hilo lipo, linapaswa kushughulikiwa haraka.
Anasema anagusia suala hilo si kwa sababu ya Waraka wa Kanisa Katoliki na Mwongozo wa waumini wa Dini ya Kiislamu uliotolewa hivi karibuni.
“Suala la udini nililiona mapema tangu mjadala wa OIC, lilikuwa chimbuko la wabunge wa kundi la G55 mwaka 1993 wakati Zanzibar ilipotaka kujiunga na jumuiya hiyo, mjadala wake ulijikita kitaifa siyo misingi ya kidini kama ilivyo sasa na ndipo wabunge kama Njelu Kasaka, Jenerali Ulimwengu walisimama kidete kwa maslahi ya taifa,” anasema Jaji Warioba.
Anasema katika kikao cha Bunge kilichopita alihudhuria ambapo alishuhudia mijadala ya OIC, uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi na Waraka wa Kanisa Katoliki, vikijadiliwa kwa misingi ya kidini waziwazi bila woga.
“Nilishuhudia mbunge Mkristo anachangia mjadala wa hoja kuhusu Mahakama ya Kadhi anaupinga na mbunge Muislamu anachangia hoja ya kupinga Waraka wa Katoliki, sasa nilijiuliza hawa wametoka wapi?” anasema Jaji Warioba.
“Kwanza naomba nikiri wazi kwamba sijaona tatizo la Kanisa Katoliki kwa kuwa mwaka 1994, 1999 na 2004 kanisa hilo lilitoa waraka uliokuwa ukiwaelekeza waumini wao mambo waliyokuwa wakizungumza ni yaleyale isipokuwa waraka wa sasa wa mwaka 2008 umeweka msisitizo... sasa imezuka hoja eti nchi inaweza kuwa kama Lebanoni inatokewa wapi?” alihoji.
“Ndugu waandishi ukisoma Waraka wa Katoliki utaona unalaani rushwa na unasisitiza maadili, mambo ambayo viongozi wa dini wamekuwa wakiyahubiri kwenye nyumba za ibada mara kwa mara; sasa maneno hayo yamewekwa kwenye maandishi imekuwa kelele. Kama ni hivyo basi itafika mahali hata viongozi wa dini watakapotaka kuhubiri vita ya rushwa tutawakataza!”anashangaa Jaji Warioba.
Akizungumzia miaka 10 ya kifo cha hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Jaji Warioba anasema alikuwa ni mcha Mungu na alipenda haki kwa kila mtu.
“Kila kila siku alfajiri alikuwa akienda kusali pale kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro, baada ya hapo anakwenda ofisini. Na jambo kubwa maishani mwake hakuwahi kuchanganya dini na uongozi wa nchi,” anasema Jaji Warioba.
“Ni sisi tumekuja tukaanza kuchanganya dini na siasa. Siku hizi imekuwa kawaida siku za sikukuu kama Kristmas na Pasaka zinaandaliwa tafrija na viongozi wa siasa na mfungo wa Ramadhani zinaandaliwa futari kwa ajili ya malengo ya kisiasa siyo dini...tena wakati mwingine kiongozi wa kisiasa anayeandaa futari siyo Mwislamu,” anasema Jaji Warioba.
“Tukae tukijua tunajiangamiza na tusitafute mchawi kwani umoja na mshikamano ndiyo utakaodumisha umoja wa taifa hili lakini hali ilivyo hivi sasa napata wasiwasi,” anasema.
Kuhusu suala la maadili kwa viongozi, anasema lazima tukubali umoja na maadili vimeporomoka na kwamba hajui nini kifanyike haraka ili kuepuka matatizo.
Kuhusu swali ni kwa nini viongozi wa sasa wamekuwa wakipishana kauli, Jaji Warioba anasema hapendi kutumia neno ufisadi ila anasema ni vyema jamii ipambane na maovu.
Anasema mkutano wa NEC ya CCM uliomalizika hivi karibuni mkoani Dodoma, viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa kauli zinazopishana katika matukio muhimu ya kitaifa.
Anasema wapo wanaeleza umma kuhusu Spika wa Bunge, Samuel Sitta kuwa alipata wakati mgumu baada ya kubanwa lakini wapo ambao wanamuunga mkono katika vita dhidi ya ufisadi.
“Katika hali hiyo ya viongozi kupishana kauli tena hadharani mimi nasema ‘There is credibility gape’, hatujui tuamini lipi na tumwamini kiongozi gani. Kuna viongozi wanataka kupiga vita ya ufisadi na kuna wengine wanawaambia wapunguze spidi ya kupambana na mafisadi. Ningependa kuona viongozi wengi wanajiunga na kundi la kupinga ufisadi,” anasema.
Anasema hivi sasa wananchi kupitia njia mbalimbali za mawasiliano wamefanikiwa kufahamu tuhumu nyingi za ufisadi kama kampuni ya Dip Green, Meremeta, Kagoda na nyingine ambazo jamii inahitaji kupata majibu yake.
Kwa upande wa makundi katika vyama vya siasa, Jaji Warioba anasema, yeye kama mwana CCM anaona kuna mgawanyiko na kama hautadhibitiwa haraka unaweza kuligawa taifa.
“Tena kibaya, mgawanyiko huo wa makundi tayari umevikumba vyombo vya habari nchini kwani baadhi ya waandishi wameonyesha kuunga mkono makundi hayo kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, napenda kuwatahadharisha kuwa hali hiyo ni mbaya; ni vyema wakazingatia taaluma yao,” anasema Jaji Warioba.
Katika miaka 10 ya kifo cha Mwalimu Nyerere kama alivyosema hapo juu, Jaji Warioba anasema Tanzania bado ni nchi yenye amani na utulivu na jitihada za kuleta maendeleo zinaendelea hadi leo.
Anasema tangu Mwalimu Nyerere, mwasisi wa taifa hili, alipofariki nchi imepiga hatua kimaendeleo kwani wananchi wengi wamekuwa na kasumba ya kuangalia mapungufu kuliko mafanikio.
Anasema kama Nyerere angekuwa hai angesema nchi imepiga hatua kielimu, kiafya na miundombinu na jitihada zimefanywa na serikali licha ya vuguvugu la mtikisiko wa uchumi uliozivuruga nchi na kusema hali siyo mbaya sana.
Kuhusu hali ya kisiasa hivi sasa tofauti na uongozi wa Nyerere, anasema uhuru wa kutoa maoni umepanuka na kusema enzi za chama kimoja kulikuwa na sera zake.
Anasema demokrasia imekua licha ya malumbano ndani ya vyama vingi.
Kuhusu kufanya kazi na Mwalimu Nyerere, Jaji Warioba anasema watu wengi walikuwa wakisema Mwalimu haambiliki jambo ambalo halikuwa na ukweli wowote.
“Nyerere alikuwa anachukia kama binadamu wengine; alikuwa anapenda kukosolewa na kupokea ushauri wa wataalamu na wasaidizi wake na hakupenda kuwagawa wananchi kwenye makundi,” anasema Jaji Warioba.
Lakini Jaji Warioba anaonekana kuchukia hatua ya baadhi ya wanasiasa kuhama vyama vyao na kujiunga CCM kisha kupewa vyeo chapchap.
“Sipendi chama kinachojivunia kupata wananchama toka vyama vingine, kimsingi chama cha siasa kokote duniani kinatakiwa kiuze sera zake ndipo watu wajiunge nacho, siku hizi tunawashuhudia viongozi waandamizi wa vyama vya siasa wanasimama majukwaani wanapokea wanachama wapya toka chama fulani …mimi sipendi mamluki kabisa,” anasema Warioba kwa sauti ya ukali.
Mungu Ibariki Afrika Mungu Ibariki Tanzania
0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Oktoba 4,2009
No comments:
Post a Comment