Header Ads

MGAO WA UMEME SASA WAIVURUGA KESI YA SAMAKI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi katika kesi ya uvuvi haramu, inayowakabili raia 37 wa kigeni waliokamatwa kwenye meli ya Tawariq 1.


Ombi hilo lilitaka mahakama isipokee ombi la upande wa mashitaka la kutaka ifanye mapitio ya amri yake ya awali ya kutaka uuze samaki hao haraka kwa kuzingatia sheria ya manunuzi ya kimataifa kwa madai kuwa taifa linakabiliwa na mgawo wa umeme, hivyo wanaweza kuharibika.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Radhia Sheikh alisema anapokea ombi hilo la upande wa mashitika la kutaka kufanyia mapitio kwa amri aliyoitoa Oktoba mosi mwaka huu, kwamba uuzaji wa samaki hao, ufuate sheria ya manunuzi ya kimataifa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Jumatatu ambapo itakuja kwa ajili ya kusikilizwa maombi ya msingi ya upande wa mashitaka, yanayotaka masharti ya uuzwaji wa samaki hao yapitiwe upya kuhofia kuharibika kutokana na kuwapo mgawo wa umeme.

Kwa mujibu wa hati ombi hilo, inaonyesha Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP)Eliezer Feleshi alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wiraza ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,C.Nyamrunda ambayo alikuwa akimwalifu Katibu huyo amri iliyotolewa na Jaji Sheikh, Oktoba mosi mwaka huu, ya kuuza tani 296.3 za samaki baada baada ya kukubali ombi la upande wa mashitaka ambalo halikupingwa na upande wa utetezi.Na katika utekelezaji wa amri hiyo mahakama hiyo imeelekeza samaki wauzwe haraka.

Aidha Oktoba 6,mwaka huu, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo aliandika barua kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,nakala kwa DDP na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inasomeka hivi :Wizara ya Mifugo na Uvuvi iko tayari kutekeleza agizo la mahakama kwa haraka na kwa umakini kadri itakavyowezekana kwa manufaa ya taifa.Hata hivyo inaona kuna ugumu wa utekelezaji wa agizo linaposema samaki hao wauzwe kwa zabuni ya kimataifa.

“Ugumu huo unatokana na ukweli kwamba sheria ya Manunuzi Na.21 ya 2004 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2005 zinaelekeza ununuzi na uuzwaji wa mali za umma ufanyike kwa kuzingatia jedwali Na.3 ambalo linasema utangazaji ufanywe kwa siku 45 kwa zabuni ya kimataifa na kwa zabuni ya taifa hili ni siki 30.Tunaona muda wa kutangaza ni mrefu sana kwani bidhaa hii ina asili ya kuharibika mapema na pia samaki husika baada ya kupakuliwa kwenye meli wamekwisha hifadhiwa kwenye majokofu kwa takribani siki 207 hadi hivyo wapo ukingoni wa kuisha thamani yake.

“Baadhi ya matatizo makubwa yanoyotukabili hadi sasa kuhusu samaki hao ni gharama kubwa ya kuifadhi ambapo zinalipwa takribani sh milioni 103-104 kwa mwezi .Pia tunakabiliwa na tatizo la kuendelea kupungua kwa thamani na kuzimika kwa umeme mara kwa mara na sasa hivi jambo ambalo linapelekea athari ya kudorora zaidi kwa thamani ya samaki hao au hata kuaribika kabisa.

“Kwa maelezo haya tunashauri utaratibu wa uuzaji samaki hao ubadilishwe ili waezwe kwa njia iliyo rahisi zaidi kwa kutumia muda mfupi bila kuvunja taratibu na sheria ya ununuzi.”ilisomea barua hiyo.

Washitakiwa hao, wanakabiliwa na mashitaka mawili la kuvua samaki bila leseni na kuvua kwenye kina kirefu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na sheria ya uvuvi wa samaki ya mwaka 2009.

Ilidaiwa kuwa, Machi 8, mwaka huu, washitakiwa wote kwa pamoja, majira ya saa sita usiku katika ukanda wa Bahari ya Hindi, ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikamatwa wakivua samaki bila leseni.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 17, 2009

No comments:

Powered by Blogger.