Header Ads

MAWAKILI WA LIYUMBA WAMKABA KOO SHAHIDI

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, inayomkabili Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, Seif Kasanga Mohamed (49), ameiambia mahakama kuwa mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi wa Minara Pacha (Twin Tower), yaliidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa BoT.

Kasanga ambaye ni mchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambambana na Rushwa (TAKUKURU), alitoa madai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, mbele ya kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi Edson Mkasimongwa, anayesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwinga wakati akitoa ushahidi wake.

Shahidi huyo ambaye pia ni mhandisi wa ujenzi kitaaluma, alifafanua kuwa Bodi ya BoT iliidhinisha baada ya Liyumba kuwa ameishatoa maagizo ya utekelezaji wa upanuzi wa mradi kwa mkandarasi.

“Ni kweli bodi ilitoa idhini ya upanuzi wa Twin Tower, lakini ilitoa idhini hiyo wakati Liyumba tayari alikuwa ameishatoa maagizo ya upanuzi wa ujenzi na malipo kwa Kampuni ya Lead Consultant (Design and Services Ltd), kwa hiyo utaona bodi ni kama vile ilikuwa ni mhuri,” alidai Kasanga.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya mawakili wa utetezi; Majura Magafu, Hillary Mkate, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo dhidi ya shahidi:Wakili: Ndugu shahidi uliwahi kuchunguza ramani ya majengo?
Shahidi: Nilipata fursa ya kuchunguza ramani.
Wakili: Nani alileta mabadiliko ya upanuzi wa Minara Pacha?
Shahidi: Liyumba.
Wakili: Liyumba siyo injinia, aliwezaje kufanya hayo mabadiliko wakati yeye alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala?
Shahidi: (Kimya) Uchunguzi unaonyesha Liyumba alikuwa akitoa maagizo ya kuidhinisha ongezeko la ujenzi.
Wakili: Je, ukiambiwa ongezeko hilo liliidhinishwa na bodi utakubali?
Shahidi: Watakuja wajumbe wa bodi wenyewe waeleze na katika uchunguzi wangu sikubaini hili.
Wakili: Tukikuambia kulikuwa na idhini ya bodi utakubali?
Shahidi: Katika uchunguzi wangu, Aproval ya bodi inayozungumzwa hapa ni ile Approval baada ya Liyumba kufanya mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi.
Wakili: Huo mkataba wa ujenzi ulikuwa ni kati ya Liyumba na kampuni ya ujenzi?
Shahidi: Hapana, ulikuwa ni kati ya BoT na Kampuni ya Lead Consultant. Lakini baadaye Kurugenzi ya Utumishi na Utawala iliyokuwa ikiongozwa na Liyumba ndiyo ilikuwa ikiratibu mradi huo (Cordinator).
Wakili: Huyo Liyumba alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala ndiyo apewe mzigo wa kushughulikia ujenzi wa mradi huo, je inaingia akilini?
Shahidi: (Kimya) Nimesema ofisi ya Liyumba ilikuwa inaratibu na ilikuwa kiungo.
Wakili: Mshitakiwa kwa cheo chake ndiye aliyeidhinisha mabadiliko hayo wakati yeye siyo mhandisi?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Wewe ni mhandisi wa ujenzi hilo swali siyo la kufikiria… jibu hilo swali upesi.
Shahidi: Kimya.
Wakili: Mabadiliko yote hayo yanatakiwa yaidhinishwe na bodi?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwa hiyo mabadiliko yote hayo hayakuidhinishwa na bodi ya BoT?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Je, Gavana marehemu Daud Balali hakuusika na mabadiliko hayo?
Shahidi: Gavana hakuhusika kabisa.
Wakili: Mbona upande wa mashitaka wakati unamsomea maelezo ya awali mshitakiwa hivi karibuni, ulidai kuwa ni Liyumba na Ballali ndiyo walifanya mabadiliko hayo bila idhini ya bodi ya wakuregenzi?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Ulisema Liyumba alikuwa akiandika barua za maagizo ya mabadiliko hayo ya upanuzi wa ujenzi kama mtu binafsi au mtumishi wa BoT?
Shahidi: Mahakama itajua.
Wakili: Ballali alikuwa Gavana na kwa mujibu wa sheria ya benki, ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi, sasa unasemaje mabadiliko alifanya Liyumba bila idhini ya Bodi?
Shahidi: Kwa sababu Ballali ameishakufa, siwezi kumzungumzia hapa.
Wakili: Hapa, jibu swali kwani wakati Ballali alipokuwa hai, ndiye alikuwa na madaraka yote na maagizo aliyokuwa akiyatoa Liyumba angeweza kuyakataa?
Shahidi: Mshitakiwa asingeweza kuyakataa.
Wakili: Kwa sababu angeyakataa angeonekana ni mtovu wa nidhamu na hivyo basi Liyumba alikuwa ni mtiifu na alikuwa katika ofisi hiyo ya umma?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Katika uchunguzi wako ulibaini mshitakiwa kafanya kosa la rushwa?
Shahidi: Nimebaini kafanya kosa linaloendana na rushwa.
Wakili: Kwa hiyo unataka kuiambia mahakama hata bodi ya BoT ilikumbwa na rushwa?
Shahidi: Sina jibu.
Wakili: Shitaka linalomkabili mshitakiwa ni kuisababishia serikali hasara kwa sababu aliongeza upanuzi wa majengo, hivi Liyumba hayo majengo aliyachukua na kuyapeleka nyumbani kwake?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Hivi upanuzi wa ujenzi wa minara pacha ulitokea usiku wa manane, au uliota kama uyoga?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Hivi bodi ilikuwa haina akili hadi isikataze hayo mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi unayodai yalifanywa na Liyumba?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Katika uchunguzi wako, Liyumba alikuwa ni mjumbe wa bodi?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Tunakubalina kwamba yale majengo ya ghorofa 18 yapo na je, yana thamani nzuri?
Shahidi: Yapo
Wakili: Thamani ya majengo yale imeteremka?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Ebu iambie mahakama sasa, serikali inapata hasara ipi?
Shahidi: Kwa kuwa hakukuwa na idhini ya bodi, ndiyo hasara yenyewe na wajumbe wa bodi watakuja kueleza (kicheko).
Shahidi: Liyumba alikuwa ni mtu mdogo kwenye bodi na mabadiliko hayo angefanya bila idhini si bodi ingemtimua kazi?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Utakubaliana na mimi wewe huwezi kuwa mchunguzi?
Shahidi: Sikubaliani na wewe, mimi ni mchunguzi.
Wakili: Unajua kazi za Takukuru zilizoainishwa kwenye Sheria ya Takukuru kifungu cha 7?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Utakubaliana kimsingi kazi ya taasisi yenu ni kuchunguza kesi zinazohusiana na rushwa na si vinginevyo?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwa hiyo utakubaliana na mimi makosa yanayomkabili mteja wangu hayahusiani na rushwa na ndiyo maana yanaangukia kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Kwa hiyo kazi hii ya uchunguzi katika kesi hii haikupaswa kufanywa na Takukuru ilipaswa kufanywa na jeshi la Polisi?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Ni nani mwenye mamlaka ya mwisho ya kuamua nini kifanyike na kipi kisifanyike BoT?
Shahidi: Bodi ya BoT.
Wakili: Uliwahi kuwahoji wajumbe wa bodi kwanini waliidhinisha mabadiliko ya upanuzi wakati mabadiliko hayo yalishatekelezwa?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Uliwauliza wajumbe hao ni kwanini wasikatae mabadiliko hayo kwa sababu wao walikuwa pale kwa ajili ya kulinda maslahi ya benki hiyo na serikali?
Shahidi: Walisema walikataa bila mafanikio.
Wakili: Uliwahi kuzisoma hizo minute za vikao vya bodi ilikuona?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwanini hukuzileta hapa mahakamani?
Shahidi: Zitaletwa na mchunguzi mwenzangu.
Wakili: Uliwahi kuusoma mkataba wote wa ujenzi wa mradi huo?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwenye huo mkataba kuna kipengele kinaruhusu kampuni ya ukandarasi wa mradi na BoT kufanya marekebisho kutokana na thamani ya shilingi kushuka?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Timu yenu ya uchunguzi iliwahi kumhoji Ballali?
Shahidi: Haikuwahi kumhoji ila nilimhoji Liyumba.
Wakili: Ulivyomhoji Liyumba ulimuuliza hizo barua za marekebisho ya mkataba ya kupanua ujenzi wa majengo aliandika kwa maelekezo ya nani?
Shahidi: Sikumbuki.
Wakili: Ulimuuliza Liyumba ni kwanini Bodi ya BoT ilikubali ongezeko la ghorofa nne, nne badala ya 14 zilizoainishwa kwenye mkataba?
Shahidi: Ndiyo na alinijibu ilikubali kwa sababu kulikuwa na ongezeko kubwa la wafanyakazi BoT kwa hiyo kulikuwa na uhaba wa ofisi.
Wakili: Bodi ilikubali kuidhinisha baada ya kuridhika kwamba yale marekebisho ya upanuzi yalikuwa ni ya msingi na yasingeweza kuisababishia serikali hasara?
Shahidi: Hapa.
Wakili: Kama hapana, bodi nayo ilifanya makosa kuidhinisha marekebisho huku ikijua itaingiza serikali hasara?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Bodi ilikuambia hiyo na haikuwa na haja ya kukataa?
Shahidi: Bodi haikukataa, ila wajumbe wa bodi walikemea.
Wakili: Hayo mahesabu ya mteja wetu kusababishia hasara ya kiasi hicho cha fedha haliyafanya nani?
Shahidi: Mimi
Wakili: Haya tupe huo mchanganuo wa mahesabu uliyoyafanya hadi ukapata hiyo hasara?
Shahidi: Sina.
Wakili: Katika hayo maagizo ya upanuzi wa ujenzi yaliyokuwa yakitolewa na Liyumba yalikuwa yakitaja kiasi chochote cha fedha?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Hicho kiasi cha gharama umekipata wapi wakati hujui hata vifaa vya ujenzi hujui vilinunuliwa kiasi gani?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Nani alikuwa na jukumu la kutunza miniti za vikaa vya bodi licha uliieleza mahakama miniti nyingine hukuzipata na baadhi ulizozipata hazina saini?
Shahidi: Katibu ambaye ni Mwanasheria wa BoT, Bosco Kimela.
Wakili: Hivi miniti zisizokuwa na saini ya Mwenyekiti na Katibu ninakuwa miniti kweli?
Shahidi: Miniti ili ziwe miniti ni lazima ziwe na saini ya watu hao.
Kesi hiyo inayovuta hisia za wengi nchini imeahirishwa hadi leo ambapo shahidi wa pili ataanza kutoa ushahidi wake.
Ifuatayo ni mahojiano kati ya jopo la Mahakimu wakazi na shahidi huyo?
Jopo:Majengo yamejengwa hayajajengwa?Liyumba alifaidika binafsi na mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi huo?Je kulikuwa na udanganyifu katika kiasi cha fedha kilichotumika katika ujenzi huo?Sasa hasara inapatikanaje?
Shahidi:Kimya(watu wakaangua kicheko).
Awali kabla ya shahidi huyo kuhojiwa na upande wa utetezi, wakili wa serikali Juma Mzarau, Ben Lincoln,Thadeo Mwenepazi na Prospa Mwangamila,alimuongoza shahidi huo kutoa ushahidi wake:Yafuatayo ni mahojiano kati ya Mzarau na shahidi huyo:
Wakili:Je lini ulikabidhiwa jukumu la kuchunguza shauri hili?
Shahidi:Februali 2008.
Wakili:Baada ya kukabidhiwa jukumu hilo uligundua nini?
Shahidi:Niligundua shauri lilipokelewa April 2006 ofisi kwetu Takukuru.
Wakili:Baada ya kukabidhiwa shauri hilo ulifanya nini?
Shahidi:Kufanya uchunguzi wa wazi kwa kukusanya vielelezo na kukusanya vielelezo na kuhoji mashahidi pamoja na Liyumba na kutembelea mradi wa minara pacha na nilibaini Bot ilisaini mkataba na kampuni ya Group Five East(PTY) Ltd ya Afrika Kusini.
Wakili:Ulishawahi kuona mkataba huo?
Shahidi:Ndiyo naniaomba kuotoa mahakama kama kielezo(jopo limepokea kama kielezo Na.moja).
Wakili:Kwa mujibu wa mkataba huo gharama za ujenzi zilikuwa kiasi gani?
Shahidi:USD milioni 73.6
Wakili:Unakumbuka gharama za kazi zilizoainishwa kwenye mkataba huo?
Shahidi:Ni za ujenzi wa jengo la South Tower ghoroga 14,North Tower ghorofa 14,ukumbi wa mikutano,sehemu ya kuegesha magari ghorofa nne na kazi za nje.
Wakili:Je katika uchunguzi wako uliwahi kutembeleza ujenzi wa mradi wa Minara Pacha?
Shahidi:Ndiyo na niligundua jengo la South Tower,Noth zilijengwa ghorofa 18 badala ya 14 zilizoainishwa kwenye mkataba, vile vile kwenye ninara hiyo majengo hayo vilijengwa viwanja vya kutua Helkopta na kwenye kuta za majengo hayo kuliwekwa(glass curtain)badala ya rangi ya kawaida ambayo iliainishwa kwenye mkataba.
Wakili; Je kulikuwa na jengo lilojengwa nje ya mkataba?
Shahidi:Ndiyo.jengo la North block lilijengwa nje ya mkataba.
,Basement mbili badala ya basement moja.
Wakili:Nani alikuwa Meneja mradi wa Minara Pacha?
Shahidi:Deogratius Kweka.
Wakili:Kielelezo gani kingine unakumbuka ulikipata kwenye uchunguzi wako?
Shahidi:Cost Alasisy report toka 2002-2008 na ninaomba niitoe mahakamani kama kielelezo.
Ghafla aliinuka wakili wa utetezi Majura Magafu na kuiomba mahakama isipokea kielelezo hicho kwani kinaonyesha wazi kiliandaliwa kwani mbaya na hakikuandaliwa kitalaamu kwani ina saini,jina la mwandishi wala mhuri wa kampuni, tarehe na kwa kifupi hiko kielelezo ni cha kuokoteza barabarani na wala haijaandikwa na shahidi huyo.

“Tunapinga kupokelewa kwa kielezo hicho kwani ni cha kuokoteza barabarani na wala hakikuandikwa na shahidi huyu tunataka aliyoandika hiyo ripoti afike hapa tumuulize maswali ..shahidi huyu atakuwa bubu tukianza kumuuliza maswali na sisi atutaki awe bubu”alidai Magafu kwa sauti ya ukali .

Hata hivyo baada ya wakili Magafu kupinga kilelezo hicho kisipokelee wakili wa serikali Mzarau aliinuka na kudai hawataki kupoteza muda wa mahakama na hivyo upande wa mashitaka wanakiondoa kielelezo hicho na kisipokelewe na mahakama na kusababisha watu kuangua vicheko.

Kiongozi wa Jopo Mkasimongwa,aliarisha kesi hiyo hadi leo ambapo shahidi wa pili ataanza kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo ambayo umati wa wananchi wengi wanafika mahakamani hapo kwaajili ya kusikiliza kesi hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Oktoba 23, 2009

No comments:

Powered by Blogger.