Header Ads

RUFAA YA ZOMBE YATINGA KORTINI

*DPP atoa sababu 11 kupinga hukumu yake

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi, amewasilisha rufaa yake kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu na kuwaachilia huru aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe na wenzake wanane waliotuhumiwa kwa mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi.


Rufaa hiyo iliwasilishwa katika Mahakama ya Rufani, jana saa 9:00 alasiri na kupewa namba 254/09 ambapo ilitiwa saini na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Francis Mutungi.
Katika rufaa hiyo ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake, DPP ametoa sababu 11 za kukata rufaa.

Kwa mujibu wa rufaa hiyo, sababu ya kwanza, DPP anadai kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati aliyewaachilia huru Zombe na wenzake, alikosea kisheria na alijichanganya katika kuumba na kutafsiri misingi ya shitaka la mauaji lililokuwa likiwakabili washitakiwa.

Sababu ya pili, anadai kuwa, kwa mujibu wa mazingira ya kesi hiyo, Jaji Massati alichanganya katika kutafsiri misingi ya dhamira ya pamoja kwa washitakiwa kutenda kosa hilo na kwamba anadaiwa kukosea kutoa tafsiri ya ungamo.

Mrufani anadai kuwa Jaji Massati, alikosea kumwachia huru mshitakiwa wa kwanza, Zombe, kwa sababu kulikuwa na ushahidi wa mazingira unaombana.

Pia alikosoa kumwachilia huru mshitakiwa wa pili, Mrakibu wa Polisi, Christopher Bageni, kwa sababu upande wa mashitaka uliwasilisha ushahidi uliomgusa katika kutenda kosa hilo.

Aidha, alishindwa kutoa sababu za muda wa kisheria za kutomtia hatiani mshitakiwa wa tatu, ASP- Ahmed Makelle, kwa kosa la mauaji.

“Jaji pia alikosea kumwachilia huru mshitakiwa wa nne (Jane Andrew) na saba (Koplo Abineth Sarro) kwa sababu wao ni waathirika wa kimazingira bila kufafanua na kuonyesha mazingira hayo ni yapi.

“Sababu ya nane, Jaji alikosea kumwachilia huru mshitakiwa wa tano, Koplo Emmanuel Mabula na wa sita, Michael Shonza, kwa kuukubali ushahidi wao usioaminika uliotolewa na washitakiwa wakati wakijitetea,” inaeleza sehemu ya rufaa hiyo.

Mrufani alidai sababu ya tisa ni kwamba, Jaji Massati alikosea kumwachilia huru mshitakiwa wa nane, Koplo Rajabu Bakari, kwa sababu kulikuwa na ushahidi mzito dhidi yake.

Sababu ya 10 iliyotolewa na mrufani ni kwamba, katika mazingira ya kesi hiyo, jaji alishindwa kumtia hatiani mshitakiwa wa kwanza (Zombe) na wa tisa (Koplo Festus Gwabisabi), kwa mujibu wa kifungu cha 300 (2) cha Sheria ya Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002; ambacho kinasema mshitakiwa anaweza kutiwa hatiani kwa kosa dogo.

Alidai sababu ya 11 anadai kuwa jaji huyo alikosea kisheria kuchambua ushahidi katika kumbukumbu na kusababisha kupoteza mwelekeo wa kesi na kujichanganya alipotoa hukumu hiyo.

Rufaa hiyo ya DPP imekuja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwaachilia huru washitakiwa hao Agosti 17, mwaka huu, pale Jaji Massati aliposema amebaini kuwa washitakiwa hao sio waliowaua marehemu na akaliagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta waliofanya mauaji hayo.

Jana, gazeti hili lilichapisha habari kubwa ambayo ilikuwa ikimnukuu Zombe ambaye alisema atishiki na rufaa itakayokatwa dhidi yake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 7,2009

No comments:

Powered by Blogger.