Header Ads

UPELELEZI KESI YA WIZI KWA DPP UMEKAMILIKA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya wizi wa gari, mali ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), inayowakabili washitakiwa 12, jana umeiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwamba upelelezi kwa kesi hiyo umekamilika.


Wakili wa Serikali, Timon Vitalis mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, aliiambia mahakama hiyo kwa kuwa upelelezi umekamilika, wanaomba wapangiwe tarehe ya kuja kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali, ombi ambalo lilikubaliwa na hakimu huyo ambaye alipanga Oktoba 12.

Awali, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Machi 5, mwaka huu, eneo la Tabata Liwiti CCM, washitakiwa hao waliiba gari STK 5002 Toyota Hiace modeli mpya lenye thamani ya sh 56,972,000, komyuta sita zenye thamani ya sh 4,250,000, printa zenye thamani ya sh 7,435,000, seti ya UPS, laptop na vitabu vya sheria mali ya ofisi ya DPP, na vitu vyote hivyo vikiwa na thamani ya sh 111,500,000.

Ilidaiwa kwamba, kabla ya kuiba vitu hivyo, walimtishia kwa bunduki Alfa Makamba, mlinzi wa gereji ambayo gari hilo lilikuwa limelazwa.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni dereva wa Ofisi ya DPP, Ally Ramadhani Mustapha, Haji Mwanga, Bakari Makara, Deogratus Coster, Philipo Jose, Athony Mengi, Mary Lyimo, Jacob Mosha, Wilfred Maleko, Alex Kimario, Hajat Faraji Kileo na mfanyabiashara Abubakari Kamugisha (31).

Wakati huo huo, kesi ya wizi wa sh bilioni 1.086 wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inayowakabili Bahati Mahenge, Manase Makale, Davis Kamungu, Godfrey Mosha na Edda Makale jana iliahirishwa hadi kesho kwa sababu wakili wa mshitakiwa wa kwanza, hakuwepo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumanne, Septemba 29, 2009

No comments:

Powered by Blogger.