Header Ads

MTOTO WA KEENJA AKUTWA NA 'UNGA'

*Ulibambwa kwenye gari alilopanda
*Apanda kizimbani kujibu mashitaka

Na Happiness Katabazi
MTOTO wa Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Charles Keenja (CCM), Agatha Keenja, jana alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na kosa la kukutwa na dawa za kulevya.


Mwendesha Mashitaka, Mussa Gumbo, mbele ya Hakimu Janeth Kiwage, alidai kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa kosa moja la kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin, zenye uzito wa gramu 6.6 zinazokadiriwa kuwa na thamani ya sh 60,000.

Gumbo alidai mshitakiwa huyo alikamatwa juzi katika Mtaa wa Makunganya jijini Dar es Salaam ambapo dawa hizo zilikutwa ndani ya gari alilokuwa amepanda.

Agatha, alifanikiwa kupata dhamana baada Hakimu Kiwage kutaka adhaminiwe na wadhamini wawili watakaotimiza masharti kwa kusaini dhamana ya sh 500,000 kila mmoja.
Hakimu Kiwage aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 2, itakapotajwa.

Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na taarifa za kuhusika kwa vigogo kadhaa wa kisiasa nchini katika biashara ya dawa za kulevya ambapo huwatumia vijana kuingiza na kuuza.
Vyombo mbalimbali vya usalama, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, kwa nyakati tofauti walitangaza kuwa na orodha ya watu wanaojihusisha na dawa hizo na kuwataka kujisalimisha au kuacha kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi.

Rais Kikwete alikwenda mbali zaidi kwa kuahidi kuwa msako wa vigogo hao utakuwa mkali kuliko ule ambao unaendeshwa dhidi ya majambazi, hali iliyojenga imani kubwa kwa wananchi, lakini matokeo yameendelea kuwa siri.

Mbali ya Rais Kikwete, maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi, akiwemo Kamishana wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo, waliwahi kusema kuwa hivi sasa serikali inaandaa mkakati wa kubadili sheria ya dawa za kulevya ili kuwabana zaidi vigogo na wafanyabiashara haramu wa dawa hizo.

Shekiondo alisema sheria ya sasa ina upungufu na inatoa mwanya kwa wafanyabiashara wakubwa kuendelea kufanya biashara ya dawa za kulevya bila kukamatwa na ushahidi licha ya majina yao kutajwa mara kwa mara na watu kuwa wanajihusisha nayo.

Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), ni miongoni mwa vigogo maarufu hapa nchini ambaye alikuwa akihusishwa na kupewa vitisho kuwa jina lake limo kwenye orodha aliyokuwa nayo Rais Kikwete.

Azzan alikiri kupata taarifa za namna hiyo kutoka kwa watu ambao hata hivyo hakuwataja, lakini akasema bado hajaitwa kuhojiwa na chombo chochote na kuiomba serikali kuzifanyia kazi tuhuma zinazotolewa kwani zinachafua majina ya watu.
Mbunge huyo aliyewahi kufanya mahojiano maalumu na Tanzania Daima kuhusu tuhuma hizo, alivitaka vyombo vya dola kufanyia kazi haraka madai hayo na ripoti yake itangazwe kwa wananchi ili Watanzania wote wajue ukweli.

Alibainisha kuwa, kelele na shutuma hizo ipo siku siri iliyojificha nyuma yake itabainika na watu wanaoshutumiwa na wale wanaoshutumu watajulikana na jamii pamoja na malengo yao.

Aliongeza kuwa litakuwa jambo zuri iwapo watu wote wanaohusishwa na biashara hiyo haramu, ambayo imegharimu afya na maisha ya vijana wengi, wakatajwa ili kuondoa hofu, wasiwasi na minong’ono inayozidi kusambaa katika jamii.

“Nimesikia jina langu limo kwenye orodha, lakini hizi ni habari za kusikia tu, hivyo siwezi kuzifanyia kazi au kuchukua hatua yoyote… binafsi sijahojiwa na wana usalama au mtu yeyote kuhusiana na tuhuma hizi, lakini madai haya yamewaweka wengi roho juu.

“Sitaki kulizungumzia hili kwa undani maadam najifahamu vizuri kuwa sihusiki hata chembe na biashara hiyo, lakini nafikiri kuna haja ya lazima ya kufanyika kwa uchunguzi wa haraka na wa kina, na ripoti ya uchunguzi huo itolewe kwa vyombo vya habari ili Watanzania wote wajue ukweli,” alisema mbunge huyo wakati akifanya mahojiano na Tanzania Daima wakati huo.

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba amekuwa akisisitiza kuwa suala hilo sasa liko mikononi mwa Rais Kikwete kwa vile wao wamekwishatimiza wajibu na kukabishi majina ya vigogo.

“Sisi hatuna tena mengi ya kusema, majina ya vigogo hawa tumeyakabidhi Ikulu… kama tulivyotakiwa, nadhani tunapaswa kuendelea kuwa na subira wakati hatua zaidi zinaandaliwa,” alisema DCI.

Alisema licha ya kukabidhi majina hayo, vita hiyo imeendelea kuwa ngumu kutokana na kuwepo mianya mingi karibu kila kona ya taifa hili.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 4,2009

No comments:

Powered by Blogger.