Header Ads

JAJI MKUU 'AWATULIZA' WATUMISHI WA MAHAKAMA

Na Happiness Katabazi

JAJI Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhani amewataka watumishi wa Mahakama kumpa ushirikiano katika kipindi hiki anacho hakikisha watumishi wote wa mhimili huo, wanaboreshwa maslahi yao kwa kufuata msingi wa sheria.


Jaji Ramadhani alitoa wito huo alipozungumza na watumishi wa Mahakama za Mkoa wa Dar es Salaam, uliofanyika katika moja ya kumbi za Mahakama Kuu na kusema amelazimika kufanya hivyo kutokana na habari za mgomo unaokusudiwa kufanywa na watumishi wa mahakama za Iringa.

Katika habari hizo, imedaiwa kwamba, watumishi hao wameipa serikali siku 60 ili kuboreshea maslahi zao vinginevyo watagoma na kutaka ongezeko la bajeti ya mahakama.

“Kwanza ni kweli mishahara ya majaji na mahakimu imeongezeka tena kwa kiasi kikubwa…alhamdulah ila makarani, madereva na watumishi wengine wa mhimili huu, wamepandishiwa kidogo kuanzia Julai mwaka huu.

…Uongozi wa mahakama unaendelea na jitihada za kudai maslahi kwa ajili ya kndi hilo la watumishi nalo liangukiwe na rehema hiyo.

Nitakwenda Iringa muda wowote kuanzia sasa kwani huko ndipo kwenye chimbuko la habari hiyo ili nikajiridhishe kama ni kweli wale watumishi 60 waliweka saini kwenye ule waraka wao. Kama ni kweli ni watumishi wetu na ninaahidi sijawachukulia hatua kwani binafsi naifahamu fika njaa iliyopo kwenye mhimili huu wa mahakama,” alisema Jaji Mkuu Ramadhani.

Jaji Ramadhani ambaye aliongozana na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Francis Mutungi, alisema chanzo cha majaji na mahakimu kupandishwa mishahara kimetokana na mapendekezo yaliyowasilishwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuwa chombo hicho kinashughulikia ajira, upandishwaji vyeo na maslahi ya mahakimu na majaji pekee.

“Kiongozi wa chombo hicho ni Jaji Mkuu na ndicho chombo kilichopeleka mapendekezo ya ongezeko la mishahara kwa majaji na mahakimu na mishahara ikapandishwa na ninawataka mfahamu chombo hicho kimeundwa na Katiba ya nchi na kazi zake zimeainishwa katika Katiba.

Sasa ili chombo hiki kiweze kushughulikia mishahara na kupandisha vyeo watumishi wengine wa mahakama, ni lazima Katiba ya nchi ibadilishwe na ikibadilishwa ndiyo itaweza kuwahusisha watumishi wote wa Mahakama.

…Hivyo naomba tuvute subira mabadiliko yatatokea. Mimi ni miaka miwili tangu niteuliwe kuwa Jaji Mkuu na hayo mabadiliko ya mishahara kwa mahakimu na majaji ni makubwa katika kipindi kifupi tu tangu nishike wadhifa huu. Naitaji nguvu toka kwenu ili niweze kusikilizwa katika sehemu husika,” alisema Jaji Mkuu kwa unyenyekevu.

“Nipeni muda ili tuweze kufanikisha madai yenu kwani majaji na mahakimu peke yao hawawezi kutoa huduma katika mahakama…siwafichi, nawaambia ukweli kwamba nafanya kile kiloiho ndani ya uwezo wangu kwani mimi sio Bunge la kubadilisha Katiba. Tume ya Utumishi wa Mahakama nimeikuta, sijaiunda mimi,” alisema.

Akizungumzia kuhusu bajeti ya mahakama alisema bado ni ndogo ukilinganisha na mihimili mingine na kwamba uongozi wa mahakama unaendelea kupambana ili uweze kupata bajeti itakayotosheleza mahakama ambazo katika mikoa yote 21 ya nchi.

Wiki mbili zilizopita moja ya gazeti la kila siku (Sio Tanzania Daima), lilishapisha habari iliyosema watumishi wa mahakama ambao si majaji wala mahakimu, mkoani Iringa wametoa siku 60 kwa serikali kuboreshewa maslahi na mishahara yao vinginevyo wangegoma kushinikiza maboresho hayo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 14,2009

No comments:

Powered by Blogger.