Header Ads

MAHAKAMA YAMWEKEA 'NGUMU' MTUHUMIWA EPA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imekataa ombi la upande wa utetezi katika kesi ya wizi wa sh bilioni 3.8 za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayomkabili mfanyabiashara Farijala Hussein na wenzake watano, lililotaka kesi hiyo iahirishwe kwa kuwa mshitakiwa wa kwanza anasumbuliwa na figo, hivyo anahitaji matibabu zaidi.


Sambamba na uamuzi huo, mahakama hiyo jana ililazimika kumruhusu zaidi ya mara tatu Farijala aliyekuwa akiomba kupitia wakili wake, Majura Magafu, kwende maliwatoni, hali iliyosababisha wakati mwingine shahidi kusitisha kutoa ushahidi wake hadi mshitakiwa huyo aliyeonekana kuwa na maumivu, arejee kizimbani.

Uamuzi huo ulitolewa na mahakimu wakazi Samwel Karua, Elvin Mugeta na Mutungi, ambapo walisema wanakataa ombi hilo la wakili wa utetezi kwa sababu vyeti vya matibabu vilivyowasilishwa mahakamani hapo vilikuwa havionyeshi kama daktari ametoa maoni yanayotaka mshitakiwa huyo apumzike.

“Tunatupilia mbali ombi hilo na tunakubaliana na ombi la wakili wa Serikali Oswald Tibabyekomya, kupinga ombi la utetezi kwa madai kwamba cheti hicho hakikuonyesha kuwa mshitakiwa anatakiwa kupumzika.

Kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Sheria ya Makosa ya Jinai, kinasema kesi inaweza kuendelea kusikilizwa bila mshitakiwa kuwepo… na kwa sababu hiyo tunaagiza shahidi apande kizimbani atoe ushahidi wake,” alisema Hakimu Mkazi Karua.

Awali, Magafu aliomba kesi hiyo iahirishwe kwa kuwa Farijala hayupo katika nafasi nzuri ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo kutokana na maumivu na kwamba yeye kama wakili hayupo tayari kuendelea na kesi hiyo kwa sababu mteja wake anaumwa.

Wakati shahidi, Rehema Kitambi ambaye ni Msajili Msaidizi wa (BRELA) alieleza mahakama kuwa Kampuni ya Mibale Farm inayotuhumiwa kuchota kiasi hicho cha fedha ilisajiliwa kwenye ofisi anayofanyia kazi isipokuwa saini iliyowekwa kwenye jina la usajili wa kampuni hiyo inafafana na yake, hivyo, imeghushiwa.

Hata hivyo, Hakimu Karua aliahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo shahidi mwingine atakuja kutoa ushahidi wake na kukubali ombi la Farijala, la kupatiwa ruhusa ya kutofika mahakamani hapo kwa kuwa anakwenda hospitali.Hata hivyo, mahakama ilimtaka mshitakiwa huyo afike mahakamani hapo kesho.

Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa mfululizo, licha ya juzi jopo hilo kushindwa kuisikiliza kwa sababu afya ya mtuhumiwa huyo ilibadilika na kukimbizwa katika Hospitali ya Burhani.

Mbali na Farijara, washitakiwa wengine ni Rajabu Maranda, Ajay Somay na maofisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambao ni Iman Mwakosya, Ester Komu na Sophia Kalika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 28, 2009

No comments:

Powered by Blogger.