ZOMBE:SITISHIKI
*Atamba rufaa inayokatwa dhidi yake haimtishi
*Aitaka serikali kuacha kubambikia watu kesi
Na Happiness Katabazi
ALIYEKUWA Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe (55). ambaye hivi karibuni alishinda kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, ameibuka na kusema hatishwi na rufaa inayokusudiwa kukatwa dhidi ya hukumu yake.
Zombe alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, katika mahojiano maalum na Tanzania Daima, yakiwa ya kwanza kwake tangu aachiwe huru na Mahakama Kuu ya Tanzania, Agosti 17 mwaka huu.
Katika mahojiano hayo, Zombe alisema hatua hiyo ya serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ni ya kutaka kujikosha kwa umma kuwa inafanya kazi vizuri wakati inajua kuwa wapelelezi wake walikiuka taratibu na sheria, na kwamba rufaa hiyo ni mwendelezo wa kufuja fedha za walipa kodi.
Zombe alisema uamuzi wa ofisi ya DPP kukata rufaa dhidi yake, anaufananisha na mcheza mpira anayemfanyia faulo mchezaji mwenzake na kisha adhabu ya penati inapigwa kwenye lango la mchezaji aliyefanyiwa faulo na kufafanua kuwa, Jeshi la Polisi na DPP walimchezea mchezo mchafu wa kisheria, hivyo hawawezi kupiga penati kwake.
“Nasubiri kwa hamu kuona huo mtindo wa msuko (wa rufaa) unaousukwa na ofisi ya DPP, kama ni ‘Twende kilioni’, ‘Kilimanjaro’ au ‘Jicho la kuku’ dhidi yangu… Ofisi ya DPP ina wataalamu wengi wa sheria, kwanini inashindwa kukubali ukweli kwamba kesi dhidi yangu ina upungufu mkubwa wa kisheria ambao hata mtoto wa shule ya chekechea anauona?
“Wananing’ang’ania tu, huku ni kufuja fedha za umma… mbona wale askari waliopeleka maiti za watu wanne katika Hospitali ya Muhimbili siku ile ya Januari 14 mwaka 2006, hawajashitakiwa? Hadi sasa wanaendelea na kazi na serikali inawafahamu fika, lakini ajabu wananishupalia mimi nisiyehusika na mauaji hayo.
“DPP na polisi waende mochwari pale Muhimbili, waombe kitabu cha mapokezi, waangalie Januari 14 mwaka 2006 ni askari gani walipeleka zile maiti za watu wanne, wakiwapata majina yao ndiyo wawakamate na kuwahoji maiti zile walizipata wapi, siyo kunifuatafuata mimi,” alisema Zombe.
Aliutaka umma wa Watanzania na wanasheria uamke na uiulize ofisi ya DPP na Jeshi la Polisi maswali matatu, kwamba ni nani aliyeandika maelezo yake ya onyo katika kesi aliyoshitakiwa? Je, maelezo ya ushahidi yanaweza kutumiwa kumpeleka na kumshitaki mtu yeyote mahakamani? Na je, kwa kutumia hati ya mashitaka pekee bila maelezo ya onyo, inawezekana kumshitaki mtu yeyote mahakamani kwa jinai?
Zombe alisema anachokiona sasa ni fedha za walipa kodi kuteketea kwa kufungulia watu kesi kwa ajili ya visasi, chuki binafsi, na kutaka kujionyesha ofisi hizo zipo imara, na kwamba polisi na ofisi ya DPP zikijibu maswali hayo ndipo uimara wao utakamilika, vinginevyo zitakuwa zikipoteza muda juu yake.
“Nasikitika sana serikali imenipotezea muda mwingi gerezani, ila hivi sasa namuachia Mungu, naamini kwa wakati wake atashughulika na wale wote walioshiriki kuniangamiza, kwa sababu fitna hizo za kunibambikia kesi ya mauaji zilikuwa kubwa mno.
“Serikali iache mchezo wa kubambika watu kesi kwa visasi na kutaka umaarufu wa kijinga, kwani mwisho wa ubaya ni aibu,” alisema Zombe kwa hisia, huku akilionyesha nyaraka mbalimbali gazeti hili.
Alihoji ikiwa yeye ana mwanga wa sheria na amefanya kazi ya upelelezi kwa muda mrefu amebambikiziwa kesi, je, wale wananchi waliobambikiwa kesi na wanaosubiri kesi zao wakiwa mahabusu ni nani atawaokoa?
“Kule gerezani nimekaa, watu wanateseka kwa kubambikiwa kesi, nashauri serikali ikaangalie watu wale na kwa mtindo huu wa kubambikia watu kesi, tukae tukijua mrundikano magerezani hautaisha hadi ofisi ya DPP na polisi wanaopeleka watu mahakamani waache mtindo wa kubambika watu kesi.
“Kwani hao waliobambikwa kesi ambao wanaendelea kusota mahabusu, siku wakiamka usingizini wakajua haki zao kwa undani, serikali itakuwa ikisumbuliwa kila siku kuwalipa fidia, na hii ni hatari kwani waliobambikizwa kesi wataanza kuichukia serikali yao, huku waliowafanyia unyama huo ni watumishi wachache tu,” alisema.
Zombe alisema kuwa, wakati akibambikwa kesi, umma wa Watanzania ukapumbazwa na propaganda zilizokuwa zikienezwa na baadhi ya vyombo vya habari, ambavyo vilimchafua na kuamini kuwa yeye ni katili, muuaji na hafai kuwepo katika jamii.
“Dhana hiyo ya propaganda ya baadhi ya vyombo vya habari ni ya kisiasa, ambayo inatumika kummaliza adui ili jamii ijenge chuki dhidi yake, na mfano mzuri ni Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, baadhi ya vyombo vya habari vilitumika kuwachafua wagombea wengine na waliochafuliwa walionekana ovyo mbele ya jamii.
“Naomba ieleweke kesi zangu nilizoyafungulia baadhi ya magazeti sitazifuta hadi pale mahakama itakapozitolea maamuzi,” alisema Zombe huku akionyesha kujiamini.
Akizungumzia maisha aliyokuwa akiishi gerezani kwa miaka minne, alisema yalikuwa mazuri kwake kwa sababu alikubali matokeo na akamwachia Mwenyezi Mungu, kwamba alipelekwa gerezani kwa dhuluma kama alivyopelekwa Nabii Yusufu, na kuwa aliamini siku moja ukweli utajulikana na Jaji Salum Massati ndiye aliyeanika ukweli wa kesi dhidi yake.
Alisema kuhusu mahitaji yake katika kipindi chote alichosota gerezani, familia yake iligharamia kila kitu, ikiwa pamoja na chakula alichokuwa akiletewa na mke wake kila siku, na alikuwa pia akifanya mazoezi ili kuuweka fiti mwili wake na kulinda afya yake.
“Nilikuwa nakula chakula cha nyumbani kwangu ambacho nilikuwa naletewa na mke wangu Fatma. Familia yangu iliingia gharama kubwa ya usafiri wa kuniletea chakula na mahitaji mengine wakati nipo gereza la Ukonga na Keko, na nilipokuwa huko nilikuwa nafanya mazoezi na mpaka sasa nafanya mazoezi ya viungo… ila nasema huo ulikuwa ni mtihani na ninasisitiza kuwa yote namwachia Mwenyezi Mungu,” alisema Zombe huku akionekana kulengwa na machozi.
Kuhusu ajira yake serikalini, Zombe alisema tayari amewasilisha notisi ya kuacha kazi Agosti 18, mwaka huu ikiwa ni siku moja tangu ashinde kesi, kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ambayo gazeti hili lina nakala yake.
“Nilipokuwa nikiishi gerezani, nilikuwa nikiwaza mambo mengi, likiwemo hilo la kuacha kufanya kazi serikalini, nimeamua kuchukua hatua hiyo nikihofia kuwa kama nikiendelea kufanya kazi serikalini nitaweza kubambikiziwa kesi nyingine,” alisema Zombe.
Notisi hiyo ambayo ina kichwa cha habari kisemacho; ‘Ombi la kustaafu kwa hiari baada ya kutimiza miaka 55 katika utumishi Jeshi la Polisi jalada Na. PF 12599 Check Na. 48812558’ inaonyesha kuwa ilipokelewa na ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI).
“Ifikapo Septemba 21, mwaka huu, nitakuwa natimiza umri wa miaka 55 ambapo kwa hiari yangu mwenyewe pasipo kushawishiwa na mtu yeyote, nimeamua nistaafu kwa hiari, hasa nikizingatia matatizo ambayo nimeyapata kwa kubambikiziwa kesi ya mauaji na huku taratibu za kisheria zikikiukwa wazi wazi kwa hila na kunikomoa.
“Napenda kufahamisha ofisi yako kuwa, ifikapo Septemba 21, mwaka huu, mimi naomba nistaafu kwa hiari na nilipwe mafao yangu yote kama sheria inavyoelekeza katika kifungu Na.58(4) cha “Police Force and Auxilliary Service Act, R.E 2002’, baada ya kuonekana sina hatia ya kosa hilo la mauaji na nilipoachiliwa na Mahakama Kuu Agosti 17 mwaka huu, na vifaa vya serikali ikiwemo sare za jeshi nitazirudisha pasipo shaka,” inasema sehemu ya notisi hiyo.
Aidha, kwa mujibu wa barua yake kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), aliyoiandika Septemba 22, mwaka huu, ambayo ilipokelewa na ofisi ya IGP, alimwarifu mkuu huyo kuwa anakabidhi kitambulisho cha kazi Na. 8051 kilichotolewa Machi 8, mwaka 1999 kwa cheo cha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Abdallah Zombe.
“Katika barua hii ya pili kwako IGP, napenda kurudia tena nimeamua kustaafu kwa hiari katika Jeshi la Polisi Tanzania baada ya kubambikiziwa kesi ya mauaji kwa makusudi yaliyo wazi, huku vifungu vya sheria ya nchi hii vikikiukwa wazi wazi kwa lengo la kunikomoa.
“Ibara ya 15(2)(a) ya katiba ya nchi inaeleza wazi nanukuu: ‘Ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake, vinginevyo isipokuwa tu kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria
“Kifungu cha 131 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, kinaeleza wazi kwamba mtuhumiwa yeyote wa kesi ya jinai ni lazima ahojiwe na maelezo yake yaandikwe kwa njia ya onyo ‘All accused person to be cautioned’.
“Kanuni ya Sheria ya Polisi (Police General Order Na.236 haya ya 18 ) inaeleza wazi utaratibu maalum unaowataka maofisa wa polisi waufuate kwa kumhoji mtuhumiwa wa kesi ya jinai, na utaratibu huo umeainishwa kwenye ‘Jugdes Rules’ katika kiambatanisho A cha PGO 236 ambapo ukisoma na kiambatanisho A cha Sheria Na. 2 na 5 ya ‘Jugdes Rules’ ambavyo vinasema mara tu ofisa wa polisi anapofikiria kwamba anataka kumshitaki mtuhumiwa wa kesi ya jinai, lazima kwanza achukue maelezo ya onyo ya mshitakiwa na utaratibu huo wa kuchukua maelezo ya onyo unatakiwa ufuatwe na Jeshi la Polisi na umeainishwa katika haya ya 8(b) ya PGO 236.
“Na Sheria ya Jeshi la Polisi ambapo zamani ikiitwa Police Force Ordinance sura ya 322 ambayo hivi sasa inaitwa The Police Force and Auxilliary Services Act Cap 322 ya mwaka 2002, kifungu cha 32(4) kinaeleza umuhimu wa askari polisi kuchukua maelezo ya onyo kwa mtuhumiwa anayekabiliwa na kesi ya jinai,” anasema Zombe kwenye barua hiyo.
“Kama sheria hizo tatu nilizozitaja hapo juu, polisi walizikiuka dhidi yangu, sheria hizo sikuzitunga mimi, zilitungwa na Bunge ila kwa makusudi walizikiuka na kunibambikizia kesi ya mauaji… sasa nimeona nikiendelea tena kufanya kazi serikalini, watanibambikizia kesi nyingine, hata kesi ya kubaka, na kwa sababu hiyo nimeona watu hawa sio wazuri tena kwangu,” anasema Zombe.
“Je nani aliyeandika maelezo yangu ya onyo katika kesi mliyonishitaki nayo? Je maelezo ya ushahidi unaweza kuyatumia kumpeleka na kumshitaki mtu yeyote mahakamani? Je, kwa kutumia hati ya mashitaka pekee bila maelezo ya onyo, unaweza kumshitaki mtu yeyote mahakamani kwa jinai?
“Maelezo yaliyotumika mahakamani na upande wa mashitaka yaliandikwa chini ya kifungu 34(B)2(C) cha Sheria ya Ushahidi ya mwaka 2002, ndiyo yaliyotumika ‘is this not a fatal illegality? Huu ni ukiukwaji wa hali ya juu wa sheria za nchi, hivyo nimeona ni heri nipumzike nyumbani na familia yangu kuliko kuendelea kufanya kazi serikalini.
“Nilichoeleza hapa ni mfano mmoja tu kati ya sheria zilizokiukwa dhidi yangu wazi wazi, hivyo leo hii ninakabidhi kitambulisho cha kazi nilichokuwa nacho, chenye cheo cha Mrakibu wa Polisi. Nawatakia mafanikio mema katika ujenzi wa taifa, lakini kumbuka usemi wa Kiingereza usemao ‘If you want to go equity you must go with clean hands’ - yaani unapotaka kwenda mbinguni lazima uwe na mikono misafi,” ilisomeka barua hiyo ambayo pia gazeti hili inayo nakala yake.
Aidha, alisema katika utumishi ndani ya jeshi hilo, kuna mengi mazuri aliyafanya na kuna mabaya aliyafanya kama binadamu, lakini baadhi ya watumishi wenzake wameamua kumlipa maovu kwa hila na fitina zao, na huku wakijua wanakiuka taratibu za sheria.
“Nimetolea mfano huo mmoja, lakini ninayo mingi, kwani kwenye tukio la mauaji ya marehemu wale sikuwepo na upande wa mashitaka ulikiri wenyewe katika mambo yasiyobishaniwa kisheria pale Mahakama Kuu kesi ilivyoanza, kwamba mimi sikwenda eneo la tukio… sasa kama sikwenda eneo la tukio, wale watu wanne niliwauaje hadi serikali iniunganishe kwenye kesi ya mauaji?” alihoji.
Pamoja na hatua hiyo ya Zombe, wakili wake Jerome Msemwa, Septemba mosi, mwaka huu, aliwasilisha barua kwa IGP na nakala kwa Waziri wa Mambo ya Ndani yenye kumbukumbu Na. JM/ADV/047/2009 ambayo analiomba jeshi hilo limlipe malimbikizo ya makato ya nusu mshahara waliyokuwa wakimkata mteja wake tangu Juni mwaka 2006 hadi sasa, na kwamba amekuwa akikatwa makato hayo bila ya Wizara ya Mambo ya Ndani kumharifu kwa maandishi.
“Baada ya kuwasilisha barua hizo, nikaenda kufuatilia majibu yangu, nikaonana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Nyambibo, akaniambia jalada langu la kuomba kustaafu kwa hiari limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Nikashangaa kuona ofisi ya AG ndiyo ilipindisha sheria na kunifikisha mahakamani, sasa huyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali anataka kutoa maamuzi gani?
“Namuonya Mwanasheria Mkuu wa Serikali asije akathubutu kutoa maamuzi yasiyozingatia misingi ya sheria ambayo mwisho wa siku yataligharimu taifa, na mfano mzuri namkumbusha arejee kesi iliyoamuliwa Mahakama Kuu Dar es Salaam na Jaji Kyando, iliyomhusu Kamisha wa Polisi, Hilary Hemed Rashid na wenzake, ambapo serikali iliwalipa mamilioni ya fedha kwa ajili ya uzembe wa watumishi wachache wasiozingatia sheria za nchi,” alisema Zombe.
Agosti 17, mwaka huu, Zombe na wenzake tisa ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, walishinda kesi hiyo baada ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati kutoa hukumu yake ambapo alisema anawaachilia huru kwa sababu hawakuhusika na mauaji hayo na akaagiza Jeshi la Polisi likawatafute walioua.
Siku mbili baadaye baada ya hukumu hiyo kutolewa, ofisi ya DPP iliwasilisha hati ya nia ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani, kupinga uamuzi huo.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Oktoba 6,2009.Hii story ilishtua jamii, kwani nilikuwa mwandishi peke yangu ambaye niliweza kumhoji Zombe, nilipongezwan ofisi na jamii kwa ujumla.Story hii sitaisahau kwani iliendelea kuniletea heshima katika jamii.
No comments:
Post a Comment