Header Ads

MWALIMU NYERERE NATAMANI UONE TUNAVYOKUENZI-(3)


Na Happiness Katabazi

BABA wa Taifa letu la Tanzania, Julius Nyerere, kwa mara nyingine nachukua kalamu kuandika kumbukizi yako. Oktoba 14 mwaka huu, ulitimiza miaka 10 tangu Mwenyezi Mungu alipokuita nawe ukaitika.


Tunazidi kukukumbuka baba japo mwili wako umelala mavumbini kule Mwintongo-Butiama, mkoani Mara.

Ni ajabu na kweli kwamba mawazo yako, falsafa na fikra zako zinaendelea kuishi miongoni mwetu.

Baba wanao tulio hai hadi sasa tunaamini kabisa hautasaulika kamwe.
Tunakukukumbuka baba kila tunaposikiliza na au kuzisoma hotuba zako. Bado zina utamu ule ule na uzito ule ule usiochuja siku hadi siku.

Wosia wako uliukita katika mtindo wako wa maisha binafsi, uongozi wako uliotukuka, matamshi na matendo yako. Miongoni mwa mambo uliyotuusia yanahusu elimu.
Ulipenda watu wote wapate elimu na ukatuambia kila apataye elimu afanye nini.

Baba, uliwahi kutuambia kwamba; aliyepata bahati ya kusoma na akapata elimu ni kama mtu ambaye kijiji kimempa chakula chote kilichopo ili ale ashibe, avuke ng’ambo akakiletee kijiji chote chakula , na asipofanya hivyo akajenga kiburi ni sawa na msaliti, tunakuenzi kwa hilo.

Tunakuenzi kuanzia katika suala la elimu, ambalo ulibobea katika hilo ukiwa mwalimu na mwanafalsafa.

Ulitufundisha falsafa ya elimu ya kujitegemea, uliyoiasisi mwenyewe; ulituusia kwamba elimu itujengee akili za udadisi.
Leo tunakuenzi baba kwa kupuuza kuwa wadadisi na wabunifu.

Shuleni tunasoma kwa kukariri ili tufaulu mitihani. Baba, hata udadisi wa kisiasa umepigwa marufuku katika taasisi za elimu ya juu, ili tuwe mbumbumbu, mazumbukuku, mzungu wa reli, wasioweza kuhoji lolote.

Usiwe na wasiwasi baba, viranja wanaimudu kazi hiyo vizuri sana, hii ni katika kuhakikisha tunaienzi vyema taaluma yako ya ualimu kwa kuifanya si taaluma tena, bali kichwa cha mwenda wazimu ambacho hata asiyejua kushika wembe anaweza kukinyoa, kwani baba, lazima mtu ajue kusoma ndiyo awe mwalimu?

Tunakuenzi baba kwa kuendelea kusoma tukiwa watu wazima na katika siku zote za maisha yetu. Chungulia baba uone jinsi wengi wetu walivyofanikiwa kusoma ukubwani na kujipatia shahada za juu kabisa.

Tangu uondoke baba idadi ya wanao wenye shahada za falsafa (PhD) imeongezeka kwa kasi. Usishangae baba tumewezaje hilo, siku hizi kuna shahada tunazipata kiurahisi kwenye mtandao. Wenyewe baba wanaziita za ‘on line’.

Kwahiyo tunakuenzi kwa kurahisisha mambo, tunatafuta wenzetu wenye uwezo kichwani tunawapa visenti kidogo wanatufanyia ‘assignments’ na kutuandikia thesis, tunawasilisha kwenye vyuo vya ughaibuni, kisha kufumba na kufumbua tunaitwa ‘madokta’. Hicho cheo tunakitumia vilivyo kukuenzi katika siasa, maana kitaaluma hatuwezi kukitumia, samahani baba hatuna ujuzi wowote katika nyanja za shahada tunazotunukiwa.

Kukuenzi kwetu hakuishii hapo baba. Si unakumbuka ulituachia vyuo vikuu. Tumekuenzi si tu kwa kuviboresha bali tumeongeza na vingine vingi. Kwa sasa tunavyo visivyopungua thelathini (30). Zaidi tumekuenzi kwa kuongeza kwa kiasi kikubwa udahili katika vyuo hivyo.

Tunaendelea, maana kupata mwongozo wa mambo mbalimbali kutoka katika wosia wako.

Utakumbuka baba kwamba kila baada ya miaka mitano kwa mujibu wa utaratibu ulioshiriki kuasisi, kunakuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa hatimaye rais,wabunge na madiwani.

Tunakuenzi baba kwa kuzingatia sifa uliotuhusia za viongozi wanaofaa.
Ulituasa baba tuepuke kuchagua viongozi kwa kigezo cha fedha.

Tupo tunaolizingatia hilo, lakini wapo wanao watukutu walioamua kukuenzi kwa kufanya kinyume kwa kuzidisha matumizi ya fedha chafu nyakati za chaguzi hizo.

Baba tunaadhimisha miaka 10 ya kuondoka kwako kwa taarifa kutoka kwa wanao wanaojihusisha na utafiti kwamba kwa sasa hivi gharama za kugombea na kufanya kampeni za urais ni mabilioni ya fedha.

Ilhali za kufanya kampeni za ubunge na udiwani wenyeviti wa serikali za mitaa ni mamilioni ya fedha.

Ni wazi baba tumeamua kukuenzi kwa kuzifanya nafasi zote za uongozi wa siasa kuwa mali ya kudumu kwa wenye fedha na jamaa zao.

Utusamehe baba kwakuwa tumepuuza wosia wako kwamba Ikulu ni mahala patakatifu na uongozi ni kazi takatifu na haipaswi kukimbiliwa kwa kutumia fedha, maana hakuna biashara huko.

Uliuliza anaye tumia fedha kupata uongozi kazipata wapi? kama kakopa atazilipaje. Baba tumeishaanza kujua vyanzo vya fedha za hawa wanao watukutu ambao hivi sasa tunawaita ‘mafisadi’.

Tunakukumbuka ulivyotunusuru kwa kukata mirija ya wanyonyaji ‘weupe’waliowahi kuivamia nchi yetu hivi sasa tunao wanyonyaji ‘weusi’ wanaojitahidi kunyonya kila palipokuwa na rasilimali ya nchi hii, kila palipo na hazina ya taifa na kila palipo na chenye thamani na wanafanya hivyo bila haya na wanalindwa na sheria za dola.

Tunakusihi uzidi kutuombea kama ulivyotuaidi ili kwa kudra za Mwenyezi Mungu tunusurike kwenye mirija hii ya watu weusi ambao wamekubuhu kwa ufisadi.

Utuombee tufunuliwe na kuwatambua mafisadi ili kwenye uchaguzi tuweze kuwanyima kura kwa lengo la kuwazuia kakalia uongozi.

Vile vile baba tunaendelea kukuenzi kwa urithi wa aina pekee uliyotuachia ambao si mwingine ila Muungano uliozaa Tanzania.

Baba tunasema ni urithi wa kipekee kwa sababu mataifa mengi duniani yamejaribu kuungana lakini yalishindwa.

Yale yaliyoungana tunashuhudia yakisambaratika lakini sisi wanao tunakuenzi kwa kuudumisha muungano hadi leo.

Baba ulituasa tuudumishe muungano huu kwa kuziona nyufa kila zinapojitokeza na kuziziba, bahati mbaya wapo wanao wamemua kukuenzi kwa kuuchokonoa nyufa kwenye ukuta wa muungano mara kwa mara.

Katika siku za karibuni baba kumekuwa na chokochoko zinazohusiana na suala la kupatikana mafuta katika upande mmoja wa Muungano.

Ni ajabu kwamba wapo wanaokuenzi kwa kuleta chokochoko ati suala la mafuta ni la upande mmoja tu.

Utuombee ili wanao wote wenye mawazo ya kutumia rasilimali za nchi hii kuvunja Muungano, washindwe na walegee.

Siku za nyuma kidogo wapo wengine waliuchokonoa Muungano kwa kuzua hoja ya Zanzibar ni nchi, wengine wakasema si nchi na wengine walifikia hatua ya kumuambia mwano mmoja ambaye amerithi cheo chako cha kwanza cha uongozi cha (uwaziri mkuu), Mizengo Pinda, akapimwe akili. Eti kosa lake ni kukuenzi wewe kwakusema Tanzania ni nchi moja. Tunashukuru hilo lilipita salama bila madhara makubwa zaidi.

Baba mwaka huu, tunakuenzi katika kukumbuka miaka 30 tangu kumalizika kwa Vita ya Kagera.

Tumekuenzi kwa kukumbuka ushindi tulioupata dhidi ya majeshi ya nduli Idd Amin.
Tunakuenzi baba kwa kutambua kwamba kimsingi kuzuka kwa vita hiyo hakukuwa na maana ya uadui kati ya Watanzania na Waganda.

Tunazidi kupendana na majirani zetu hawa, zaidi ya hayo, baba hata mtoto wa marehemu Idd Amin, amekuenzi kwa kuzuru kaburi lako na kuzungumza kindugu na familia yako iliyopo Butiama.

Tunaendelea kukuenzi kwa kukidumisha chama cha siasa ulichokiasisi, chama ulichokijengea misingi ya kipekee iliyotukuka, cha ajabu wapo wanaokuenzi kwa kuimomonyoa vilivyo misingi ya chama hicho.

Hivi karibuni baadhi ya wanachama waandamizi waliwaziba midomo wanachama wenzao wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kilichofanyika Dodoma.

Baba walizibwa midomo wasikemee maovu na wanazibwa midomo wasiwasakame wanaoliibia taifa, wanaopotoka kimaadili, wamezibwa midomo wasihoji wala kutoa ukali dhidi ya wanaopindisha miiko na kanuni za chama hicho! Hakika baba huku ni kukuenzi kwa aina yake.Hakika baba taifa lina kuenzi kwa staili za aina mbalimbali.

Stahili ya kupotoka kimaadili nayo imetia fora. Usishangae baba kusikia hayo, kwani hata sisi hatukutarajia kwamba tutafika mahali tukuenzi kwa kuwatandika vibao, warithi wa nafasi yako kuu ya uongozi.

Eti kwa sababu wako mstari wa mbele kupambana na gonjwa la ukimwi katika misingi inayozingatia uhalisia. Baba wanao wanakuenzi kwa vitendo vilivyo kithiri vya kujichukulia sheria mkononi ikiambatana na utovu wa nidhamu.

Hatukutarajia baba kukuenzi kwa kupopoa kwa mawe msafara wa mrithi wako mwingine, Rais Jakaya Kikwete, ati kwasababu msafara wake ulichelewa kufika na kuongea na wananchi wa mkoa wa Mbeya.

Tunakuenzi baba kwa kuimarisha ulinzi wa nchi kiasi kwamba hata baadhi ya silaha ulizotuachia bado zipo kwenye maghala yetu.

Sitalaumu baba sisi si wazembe sana, japo Aprili 29 mwaka huu, zililipuka na kuyakatisha maisha ya baadhi ya watu huku wengine wakiharibiwa mali zao.

Kadhalika Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), nalo mwaka huu, limekuenzi kwa kuadhimisha miaka 45 tangu kuanzishwa kwake, kwa namna ya kipekee kabisa, maadhimisho yaliyoambatana na maonyesho ya zana mbalimbali za kivita.

Utuombee tuweze kukuenzi kuzingatia falsafa yako ya kujitegemea kupitia uzalishaji wa wingi wa magari ya kizalendo aina ya ‘Nyumbu’. Baba utuombee ili siku moja tukuenzi kwa kutumia magari hayo hata kwa viongozi wetu ambao wanakuenzi kwa njia iliyopotoka, kwa kutumia magari ya kifahari huku wananchi wanaowaongoza ni maskini.

Baba nikudokeze kwamba mwanao mmoja mwaka huu, amekuenzi kwa kubadili magari Ikulu, hautumii tena Benz au Land Rover kama wewe, kanunua mabima (BMW) ya kifahari kutumika katika shughuli mbalimbali, ikiwamo Ikulu, mahali ulipotuambia ni patakatifu.

Baba tumekuenzi kwa kukodisha lililokuwa Shirika la Reli (TRC). Samahani mwekezaji tuliyemkodishia hana fedha kiasi kwamba kila siku anakwenda serikalini kulialia asaidiwe kuwalipa mishahara wafanyakazi.

Baba, nitakuwa natenda dhambi kama sitakueleza hili kwamba uendelee kumuombea mkuu wetu wa Kaya, Rais Jakaya Kikwete, aendelee na moyo wake wa uongozi, aendelee kuruhusu uhuru wa watu kutoa maoni, kwani katika hili binafsi nampongeza.

Huko uliko baba, uendelee kumuombea kwa Mungu ili asibadilishe msimamo wake wa kuturuhusu sisi wananchi wake kutoa maoni.

Katika hili, baba nampongeza Kikwete kwani hivi sasa baba ni ruksa kuikosoa serikali na viongozi wake, licha ya kwamba kuna baadhi ya watendaji wake wanakosa uvumilivu.
Tunakuenzi baba kwa kudumisha demokrasia ya vyama vingi.

Na utakumbuka ulishauri vyama vingi viwepo lakini visiwe utitiri kiasi cha kukosa maana kwa jamii.

Utuwie radhi baba, kwani kadiri muda unavyozidi kwenda, vyama vingi vilivyoanzishwa nchini vinazidi kuwa dhaifu.

Sababu za udhaifu ni nyingi, ikiwamo kuhama hama kwa vijana wako walioamua kukuenzi kwa kuendekeza uchu wa madaraka na ubinafsi.

Leo hii wakikosa madaraka hapa, kesho wakikosa ruzuku pale, wanaamua kukimbilia kwingine.

Kwa upande mwingine baba, wapo wanaandishi wa habari wenzetu wasomi, tena ni wasomi sana, ambao kwa makusudi wameamua kujigeuza ‘matambala ya deki’ ya wanasiasa manyang’au, ambao wanabaka uchumi wa taifa kwa kuwaandikia habari na makala za kuwasafisha ili jamii iwaone ni wanasiasa wema.

Aidha, baba tunakuenzi kwa mifumuko ya migomo na maandamano ya kila kukicha. Hata Oktoba 14 mwaka jana, pale Diamond Jubilee walimu walifanya vurugu na kumpiga rais wa chama chao kwa meza, viti, mawe na siku iliyofuata wakagoma kufundisha karibu nchi nzima kuishinikiza serikali iwalipe haki zao.

Lakini baba pia tunakuenzi kwani taifa lako uliloliasisi limeweza kupiga hatua za kimaendeleo katika sekta ya afya, miundombinu, teknolojia, afya na jitihada zaidi za kuliletea maendeleo taifa zinaendelea licha ya watoto wako baadhi ambao ni watukutu wanajaribu kurudisha nyuma jitihada hizo kwa kuendekeza kutafuna rasilimali za umma.

Tuombee baba, ili mfumo wa elimu yetu ukuenzi, mfumo wa uchumi wetu nao ukuenzi na mfumo wa siasa ukuenzi pia.Kadhalika viongozi wetu wakuenzi kwa maneno yao, mawazo yao na matendo yao.

Baba, viongozi wetu inabidi wakumbuke maneno ya Yesu Kristo aliyowaambia watu wa taifa la Uyahudi, kwamba “Hamjui kuwa mnaye baba mwingine, ninyi si watoto wa Ibrahim, ninyi ni watoto wa ibilisi, kwa kuwa ibilisi amekuwa mwongo na mnafiki tangu mwanzo, nanyi mnayatenda hayo hayo kama baba yenu”.

Sasa baba , wanao tunapojivunia ubaba wako, baadhi yetu wanaye baba mwingine ambaye si wewe!

Baba yao ni ibilisi ‘fisadi’, ndiye wanayempenda, kumsikiliza, kumuenzi na kumtumikia.Hata leo hii,angali akinyonya kwakutumia utandawazi, ubinafsishaji na kuendekeza masilahi binafsi.

Viongozi wetu wa leo mnamuenzi baba yupi? Baba Mungu alikuumba na ukiisha kuifanya kazi yake hapa kwetu, akakutwaa. Jina la Bwana lihimidiwe na aipumzishe roho yako mahali pema peponi. Amina.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Oktoba 18,2009

1 comment:

Anonymous said...

Haya Happy! Kweli tunam-enzi Mwalimu kwa staili mbalimbali, laiti staili sahihi ndizo zingetawala na kuboreshwa zaidi

Powered by Blogger.