Header Ads

WALIOGUSHI KUDHAMINI KIGOGO BOT KORTINI

Na Happiness Katabazi

BAADA ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuamuru wafanyabiashara wawili wakamatwe kwa kuwasilisha ripoti za uthamini wa majengo za kughushi, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka saba.


Mbele ya Hakimu Mkazi Liad Shamshana, Wakili wa Serikali Frola Massawe, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Teligon Rutaihwambyemo “David Majebele” (46), na mwenzake Koli Syikiliwe Sanga “Felix Mussa Nyuki” (53), wakazi wa Mwanyamala, Mchangani jijini Dar es Salaam.

Wakili Massawe alidai kuwa, shitaka la kwanza kwa washitakiwa hao ni la kula njama kwa nia ya kutenda kosa, ambapo kwa pamoja, wanadaiwa kuwa Oktoba 20, mwaka huu, katika sehemu isiyofahamika jijini Dar es Salaam, walikula njama na kutenda kosa la kughushi.

Alidai shitaka la pili na la tatu linamhusu kila mshitakiwa peke yake. Mshitakiwa wa kwanza anadaiwa kuwa siku hiyo alijitambulisha kwa Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu, Lameck Mlacha kwa jina la David Majebele, wakati mshitakiwa wa pili alijitambulisha kwa msajili huyo kama Felix Nyuki, huku wakijua si kweli.

Wakili huyo wa serikali alidai kuwa, shitaka la tano ni kwa ajili ya mshitakiwa wa kwanza, Rutaihwambyemo, ambaye anadaiwa kuwa Septemba 14, mwaka huu, katika eneo lisilofahamika katika Manispaa ya Kinondoni, alitengeneza taarifa ya tathimini ya kughushi inayoonyesha kitalu E, namba 247 cha Mbezi, kina thamani ya sh bilioni tatu huku akiwa na lengo la kuonyesha kuwa taarifa hiyo ni halali na imetolewa na Mthamini Mkuu wa Serikali.

Aidha, alidai shitaka la tano ni kwa ajili ya mshitakiwa wa pili (Sanga), ambaye anadaiwa kuwa Septemba 29, mwaka huu, ndani ya Manispaa ya Kinondoni, aliandaa ripoti ya tathimini inayoonyesha kuwa jengo lililopo katika Kitalu 74, eneo la Gerezani, lina thamani ya sh bilioni 5.8 na kuonyesha taarifa hiyo ilitolewa na Mthamini Mkuu wa Serikali, huku akijua si kweli.

Alidai shitaka la sita na saba linamhusu mshitakiwa mmoja mmoja ambapo Oktoba 20, mwaka huu, wanadaiwa waliwasilisha taarifa hizo za uthamini, huku wakijua zimeghushiwa kwa Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu, Lameck Mlacha.

Hata hivyo, washitakiwa walikana mashitaka yote na kurejeshwa rumande hadi Novemba 4 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

Wiki iliyopita, Hakimu Mlacha aliamuru washitakiwa hao waliokuja kumdhamini mshitakiwa wa nne ambaye ni Mkurugenzi Mstaafu wa Benki Kuu (BoT), Ally Bakari, katika kesi ya kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 104.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Oktoba 23, 2009

No comments:

Powered by Blogger.