Header Ads

LIYUMBA AYASUTA MASHITAKA DHIDI YAKE

*Akanusha kubadili michoro ya majengo BoT
*Amtupia mzigo marehemu Dk. Daud Ballali

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, anayekabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia hasara serikali ya sh bilioni 221, jana alivunja ukimya na kudai kuwa mradi wa ujenzi wa Minara Pacha (Twin Tower), uliidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi na kamwe yeye hausiki.

Liyumba alitoa madai hayo mbele ya jopo la mahakimu wakazi, linaloongozwa na Edson Mkasimwango, Lameck Mlacha na Benedict Mwinga, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya mshitakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali, na mara baada ya kumalizika kusomewa maelezo hayo na Wakili wa Serikali, Juma Mzalau, alitakiwa kuyakubali au kuyakataa.

Mshitakiwa huyo ambaye anaendelea kusota rumande kwa miezi kumi sasa, kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, alidai kuwa ujenzi wa mradi huo uliidhinishwa na bodi ya BoT na kuongeza kuwa, kisheria idhini ya ujenzi na malipo ya ujenzi, kamwe haiwezi kutolewa bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi.

Liyumba aliyekuwa akijibu maelezo hayo kwa kutumia zaidi lugha ya Kiingereza, alidai kuwa anakubali kwamba kulikuwepo na mkataba kati ya BoT na kampuni ya ukandarasi ya Group Five, uliosainiwa Juni 25 mwaka 2002.

Huku akizungumza kwa kujiamini, Liyumba alidai kuwa mkataba huo, ulielekeza gharama za kazi ya ujenzi, lakini yeye kwa wadhifa wake, hakuhusika kuuandaa kwa sababu si mwanasheria kitaaluma na kuongeza kwamba, mkataba huo uliandaliwa na Idara ya Wanasheria wa BoT.

“Kuhusu vifaa, michoro na shughuli nyingine za ujenzi huo, mimi kwa cheo changu cha Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala havinihusu, kwani vinamhusu meneja mradi wa ujenzi huo ambaye hata hivyo katika hayo maelezo ya awali niliyosomewa na upande wa mashitaka leo (jana), hamjamtaja.

“Waheshimiwa, ni sawa na wewe unajenga nyumba yako kwa miaka sita, na wakati unaendelea na ujenzi, unaamua kubadilisha dirisha, unaweka dirisha la aina nyingine, naomba muwe makini katika kesi hii, kwani ina mambo mengi ya kitaaluma.

“Pia ni kweli yalifanyika mabadiliko ya ujenzi wa mradi huo baadaye na mabadiliko hayo yalipelekwa kwenye bodi na bodi iliyaidhinisha. Na nitoe angalizo hapa kwamba, Mwenyekiti wa Bodi ni Gavana ambaye wakati huo alikuwa marehemu Daudi Balali na ndiye aliyeidhinisha na saini zake zipo.

“Sasa hayo madai kwamba mabadiliko ya ujenzi hayakuidhinishwa na bodi ni ya kushangaza sana, kwani nayalinganisha na maneno ya kusikia mitaani,” alidai Liyumba na umati wa watu uliofika mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo, kuangua vicheko.
Akijibu madai kuwa yeye ndiye aliyeisababishia hasara serikali ya kiasi cha sh bilioni 221, Liyumba alijibu:

“Nakataa kabisa, ni uongo mkubwa, kwani ni lini BoT imesema imepata hasara? Kwanza Serikali ya Tanzania haikufadhili mradi wa ujenzi ule, sasa nani kasema nilisababisha hasara? Hivi tangu lini Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala akahusika na masuala ya kubadilisha michoro ya ujenzi? ‘It’s very funny,” alisema Liyumba huku akionyesha kujiamini na kusababisha watu kuangua vicheko.

Aidha, alidai anakubali kuwa alianza kuitumikia BoT tangu mwaka 1973 hadi 2007 na kuomba upande wa mashitaka ufanye marekebisho katika hati ya maelezo iliyoonyesha alimaliza utumishi wake katika benki hiyo mwaka 2008 na kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala hadi alipostaafu.

Pia alikubali kwamba anashitakiwa kwa makosa mawili ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma kwa kuidhinisha mradi wa Minara Pacha bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi ambapo uamuzi huo uliisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Awali, kabla ya Liyumba kujibu malezo hayo, Wakili Kiongozi wa Serikali, Justus Mulokozi aliyekuwa akisaidiwa na Juma Mzalau, Thadeo Mwenepazi, Prosper Mwangamila na Tabu Mzee, aliiambia mahakama kuwa wapo tayari kuanza kusoma maelezo hayo na kuiomba mahakama iuruhusu upande wa mashitaka ufanye marekebisho katika shitaka la pili, ambalo kwa sasa litasomeka kusababisha hasara, ombi ambalo lilikubaliwa na jopo hilo.

Akisoma maelezo ya awali, Wakili Mzalau, alidai kuwa mshitakiwa anashitakiwa na mashitaka mawili ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kusababisha hasara serikali kinyume na kifungu 284(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 na kuwa makosa yote aliyafanya kati ya kipindi cha mwaka 2001-2008.

Mzalau alidai Liyumba aliajiriwa na BoT mwaka 1993 na alishika nyadhifa mbalimbali hadi mwaka 1999, alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Utumisi na Utawala, kazi aliyoifanya hadi mwaka 2008.

Alidai kuwa, mwaka 1984 Makao Makuu ya BoT, yaliungua moto na aliyekuwa msanifu wa jengo hilo alikuwa Shaah wa Kampuni ya Design & Services Ltd (D/S Ltd Dsm), aliyepewa jukumu la kutoa michoro kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo lililoungua.

Mzalau aliendelea kudai kuwa, mwanzoni mwa mwaka 1990 lilitolewa wazo la kujenga ofisi mpya ya BoT na michoro ya ujenzi wa jengo hilo, iliandaliwa na Kampuni ya D/S Ltd na kwamba hapo ndipo mradi wa ujenzi Ten Mirambo Office Station, ulipojitokeza.

Wakili huyo alieleza kuwa, mchoraji wa D/S Ltd alipewa maelezo na BoT kukamilisha michoro kabla ya zabuni kutolewa kwa makandarasi na mwaka 1999 aliyekuwa gavana, Balali, alitoa mawazo mapya ya ujenzi wa Twin Tower.

“Kampuni ya D/S Ltd iliandaa michoro mipya kwa ajili ya kutekeleza mawazo ya Gavana Balali na michoro hiyo iliidhinishwa na Bodi ya BoT, hata hivyo kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi, ujenzi huo haukuanza hadi mwaka 2002,” alidai Mzalau.

Aidha, alidai baada ya mchakato wa zabuni, Kampuni ya Group Five East ilishinda zabuni ya ujenzi wa Minara Pacha na mkataba wa BoT na kampuni hiyo ulisainiwa Juni 25 mwaka 2002 na kipindi cha mkataba mradi ulitakiwa kumalizika ndani ya miaka mitatu, yaani mwaka 2005.

Aliendelea kudai kuwa, mkataba wa ujenzi wa BoT ulipata ridhaa ya Bodi ya Benki Kuu na gharama ya ujenzi iliyopitishwa ni dola za Kimarekani 73,600,000 na mkataba huo uliainisha kiwango cha kazi kuwa katika maeneo makubwa matano:

Mzalau alidai eneo la kwanza ni la ujenzi wa jengo la North Tower liwe na ghorofa 14 na upana wa mita 15,000 na gharama za ujenzi ni dola 26,929,953, eneo la pili, South Tower kwa kiwango cha ghorofa 14, ukubwa wa mita 9,700 lingekuwa na gharama ya dola za Kimarekani 851,431.

Alitaja eneo la tatu kuwa ni ujenzi wa ukumbi wa mikutano wenye ukubwa wa mita 4,360, utakaokuwa na thamani ya dola za Kimarekani 10,595,176, eneo la nne, ni la ujenzi wa maegesho ya magari, lenye ukubwa wa eneo la mraba 6990 na thamani ya dola za Kimarekani 4,313, 420 na eneo la tano ni la kazi za uendeshaji wa nje ambalo lingegharimu dola za Kimarekani 1,890,019, hivyo kufanya jumla ya kiasi cha dola za Kimarekani milioni 73,600.

Alidai kuwa mara baada ya mkataba huu, Balali ndiye aliyekuwa gavana na Liyumba alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi wa Utawala na mkuu wa idara hiyo.

Mzalau alidai Liyumba alikuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi huo kutokana na wadhifa wake, pia alikuwa na mamlaka ya ujenzi wa Minara Pacha kwa kuratibu mahusiano yaliyopo kati ya D/S Ltd, mkandarasi na Meneja Mradi.

“Katika usimamizi wa uratibu wa ujenzi wa Twin Tower, Liyumba pamoja na gavana Balali bila ya kupata kibali cha Bodi ya Benki Kuu, wakaamua kubadili michoro ya ujenzi wa majengo hayo bila ridhaa ya bodi ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kupitisha hayo,” alidai Mzalau.

Akifafanua mabadiliko ya michoro ya ujenzi yaliyofanywa na Liyumba na Balali, alisema ni pamoja namba za maghorofa yote kutoka ghorofa 14 kwenda 18, mchoro wa kiwanja cha helkopta na thamani, talazo na kuongeza kuwa bodi ilijaribu kupinga ukiukwaji huo wa taratibu bila mafanikio na kwamba mabadiliko hayo ndiyo yalisababisha serikali kupata hasara ya sh bilioni 221.

Hata hivyo, upande wa mashitaka uliomba kutoa mkataba kivuli uliosainiwa Juni 25 mwaka 2002 kama kielelezo, lakini mawakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke walipinga mahakama isipokee vielelezo hivyo kwa sababu ni kivuli na kuongeza kwamba, kwa teknolojia ya sasa kielezo hicho kinaweza kuchezewa.

Aidha, kiongozi wa jopo la mahakimu hao, Mkasimwango, aliutaka upande wa mashitaka utaje orodha ya mashahidi kwa sababu tayari wameishamaliza kusoma maelezo ya awali.

Januari 27, mwaka huu, Liyumba na aliyekuwa Meneja Mradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashitaka hayo.

Lakini Mei 27, mwaka huu, Hakimu Mkazi Waliarwande Lema aliwafutia mashitaka baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa na dosari za kisheria.

Hata hivyo, baada ya kuachiwa, walikamatwa tena, lakini Liyumba peke yake ndiye aliyepandishwa tena kizimbani Mei 28 na kusomewa mashitaka upya.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Septemba 26, 2009

No comments:

Powered by Blogger.