Header Ads

WARIOBA AMUONYA KIKWETE

*Amshangaa kuzungumzia kesi za vigogo
*Aingiwa wasiwasi na wanaomshauri
*Afananisha kesi za EPA na Operesheni Mitumba
*Asikitika kesi ya Zombe kupelekwa chapuchapu

Na Happiness Katabazi

WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema hatua ya Rais Jakaya Kikwete, kuzungumzia kesi kubwa kubwa zinazotarajiwa kufikishwa mahakamani si sahihi, kwa sababu zinaweza kumshushia hadhi yake.


Amesema Rais Kikwete anaweza kujikuta katika wakati mgumu iwapo washtakiwa katika kesi hizo watashinda kesi zao, kwa sababu wanaomshauri kuzizungumzia sasa, hata kabla hazijafikishwa mahakamani, wanaweza kumruka na kueleza kuwa ni yeye aliyeagiza kesi hizo zipelekwe mahakamani badala ya vyombo husika.

Jaji Warioba aliyasema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika ofisini kwake Masaki, jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, alizungumzia mustakali wa taifa na miaka kumi ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza taratibu, lakini kwa maneno yanayosikika, Jaji Warioba alieleza kuwa alishtuka baada ya kusikia kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa hivi karibuni wakati akizungumza na taifa kupitia Televisheni ya Taifa kuwa, kuna kesi tatu kubwa ambazo ziko mbioni kufikishwa mahakamani.

“Huu mtindo wa kumshauri rais aseme hayo, mwisho wa siku washtakiwa watashinda kesi, wale maofisa wa serikali waliokuwa wakimshauri rais aseme hayo watamruka, watasema ni rais ndiye aliyeagiza kesi hizo ziende mahakamani na si vyombo husika,” alisema Jaji Warioba huku akionyesha kukerwa na hali hiyo.

Jaji Warioba alitoa kauli hiyo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua maoni yake kuhusu wingi wa kesi za matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi zinazoendelea kufunguliwa mahakamani na serikali ya awamu ya nne.

Ingawa alisema hataki kulizungumzia kwa undani suala la kesi hizo kwa sababu zipo mahakamani, alieleza kuwa hatua hiyo ya kufikisha vigogo mahakamani inatia matumaini kwamba vita ya ufisadi imewanasa hata vigogo.

Lakini alionya kuwa ni vema kukawa na tahadhari kubwa katika ufunguaji wa kesi hizo, kwa sababu zipo zinazofanana na zinazofunguliwa sasa ambazo zilifunguliwa mwaka 1979, lakini kwa sababu taratibu husika hazikufuatwa, serikali ilijikuta ikishindwa katika kesi hizo.

“Nimefikia hatua ya kutahadharisha kuhusu kesi hizo, kwa sababu ninaona zoezi hilo linafanana na Operesheni Mitumba iliyofanyika mwaka 1979, ambapo kamati ziliundwa na kukamata watu kisha wakafikishwa mahakamani bila kufuata taratibu mahususi za kisheria. Mwisho wa siku serikali ilishindwa zile kesi na ikawalipa fidia wale wananchi, lakini operesheni ile ilikuwa maarufu sana kama kesi za sasa.

“Pia mwaka 1983 kulikuwa na operesheni ya kuwakamata wahujumu uchumi, nayo ilikuwa na msukumo wa kisiasa tu, watu wengi walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Vile vile serikali ilishindwa kesi hizo na mwisho wa siku serikali iliwalipa fidia kwani serikali ilifungua kesi hizo bila kufuata taratibu mahsusi za kisheria. Kama Operesheni Mitumba, operesheni hiyo nayo ilikuwa maarufu sana. Sasa kwa mifano hiyo tuwe makini katika ufunguaji wa kesi.

“Kutumia tume katika kuandaa kesi, sina hakika kama tume zinafanya kazi ipasavyo kwa vile tume nyingi zinafanya kazi kisiasa zaidi…nimesoma hukumu ya kesi ya aliyekuwa ACP, Abdallah Zombe na wenzake iliyotolewa na Jaji Salum Massati, ni kweli watu wale wanne waliuawa hakuna ubishi, lakini tume iliandaa ushahidi kwa kupewa siku kadhaa na aliyeiunda tume hiyo.

“Nimeshangazwa na upelelezi wa tume hiyo kushindwa kumpata aliyewaua watu wale, kwani watuhumiwa wa ujambazi wa kwenye mabenki wanapoiba, polisi inawakamata lakini aliyeua watu wanne imeshindwa kuwapata…haiingii akilini! Sasa sijui kesi ya Zombe ilipelekwa haraka haraka kwa ajili ya kisiasa!” alisema Warioba kwa masikitiko.

Akizungumza kuhusu kesi za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Jaji Warioba alisema tume iliyoundwa kuchunguza wizi huo ilipaswa kufanya kazi zake kwa misingi ya kisheria, badala ya kumuingiza rais katika sakata hilo.

Alisisitiza kuwa, haikuwa sahihi kwa Rais Kikwete kutoa amri kwa watuhumiwa wa kashfa hiyo warudishe fedha na kwamba hatua hiyo aliichukua baada ya kushauriwa vibaya.

“Sasa sijui watuhumiwa hao walirudisha fedha hizo kwa misingi gani. Na ifike mahala tujiulize, washitakiwa hao wakishinda kesi mtawarudishia nini wakati fedha walizozirejesha zilishapelekwa kwenye matumizi mengine ya serikali kwenye sekta ya kilimo?” alisema Jaji Warioba ambaye ni mwanasheria kitaaluma.

Akizungumzia hali ya mshikamano wa taifa, alisema hivi sasa kuna dalili ya umoja wa kitaifa kuanza kusambaratika tofauti na zamani ambapo Tanzania ilikuwa nchi yenye mshikamano na wananchi wote walikuwa wakiitana ndugu.

“Miaka ya nyuma, maskini walikuwa na sauti katika kuendesha nchi, lakini hii leo matajiri ndio wenye sauti katika kuendesha nchi, na leo hii uongozi wa nchi upo karibu mno na matajiri kuliko wananchi maskini,” alisema Jaji Warioba.

Alieleza zaidi kuwa, hata ndani ya serikali kwa sasa kuna matabaka kati ya watumishi wa umma ambao wanapata mishahara mikubwa na wale wanaopata mishahara midogo jambo ambalo liliweza kudhibitiwa katika awamu za uongozi zilizopita.

Jaji Warioba ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Sheria, alisema zamani siri za serikali zilikuwa zinatunzwa, jambo ambalo kwa sasa halipo, kwa sababu siri nyingi zinavuja kutokana na kuwepo makundi kati ya walionacho kikubwa na wanaopata mishahara midogo.

“Hakuna kitu kilichonishangaza kama wakazi wa Ngorongoro kuandamana hadi Ikulu, ebu tazameni Ngorongoro kuna safu ya uongozi, lakini walishindwa kuomba ahadi ya kumuona rais ofisini kwake na wananchi hao wakaamua kuchukua utaratibu wao wa kuandamana na kufika Ikulu…sasa katika hili tunaona wazi imani ya wananchi kwa viongozi wao haipo tena, na hii inaendelea kutugawa kwenye matabaka,” alisema.

Aidha, Jaji Warioba alieleza kuwa taifa sasa limeanza kutafunwa na ukabila na udini jambo ambalo pia linachangia kuwagawa wananchi kikanda na kikabila.

Alisisitiza kuwa, dhambi ya dini imeingia na udini sasa unazungumzwa sana baada ya kusambazwa kwa waraka uliotolewa na viongozi wa Kanisa Katoliki.

“Suala la udini nililiona mapema tangu mjadala wa OIC. OIC ilikuwa chimbuko la G55 mwaka 1993 wakati Zanzibar ilipotaka kujiunga na jumuiya hiyo, mjadala wake ulijikita kitaifa siyo misingi ya kidini kama ilivyo sasa, na ndipo wabunge kama Njelu Kasaka, Jenerali Ulimwengu walisimama kidete kwa maslahi ya taifa,” alisema.

Alisema alihudhuria mkutano wa Bunge uliopita na alishuhudia jinsi hoja ya taifa kujiunga na jumuiya ya OIC, Mahakama ya Kadhi na Waraka wa Kanisa Katoliki, ilizungumzwa kwa misingi ya kidini wazi wazi ambapo wabunge Waislamu walitaka nchi ijiunge na jumuiya, huku Wakristu wakipinga.

“Kwanza naomba nikiri sijui msingi wa tatizo la waraka wa Kanisa Katoliki hadi sasa kwani mwaka 1994, 1999, 2004 kanisa hilo lilitoa waraka uliokuwa ukiwaelekeza waumini wao, mambo waliyokuwa wakizungumza ni yale yale isipokuwa waraka wa sasa wa mwaka 2008 umeweka msisitizo katika mambo ambayo viongozi Wakatoliki wamekuwa wakiyasema kila kipindi cha uchaguzi. Sasa imezuka hoja eti nchi inaweza kuwa kama Lebanon, inatokea wapi?

“Ndugu waandishi, ukisoma waraka wa Katoliki, utaona unalaani rushwa na unasisitiza maadili, mambo ambayo viongozi wa dini wamekuwa wakiyahubiri sana, sasa maneno hayo yamewekwa kwenye maandishi imekuwa kelele. Kama ni hivyo basi itafika mahali hata viongozi wa dini watakapotaka kuhubiri vita ya rushwa tuwakataze,” alisema.

Kuhusu miaka 10 baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, alisema Mwalimu alikuwa ni mcha Mungu na kila siku alfajiri alikuwa akienda kusali katika Kanisa la Mtakatifu Petro kabla ya kwenda ofisini.

Alisema pamoja na ucha Mungu wake, hata siku moja hakuwahi kuchanganya dini na uongozi wa nchi.

Jaji Warioba alisema tangu kufariki kwa Mwalimu Nyerere, taifa limepiga hatua kubwa kimaendeleo kwa sababu wananchi wengi sasa wana kasumba ya kuangalia upungufu kuliko mafanikio, jambo ambalo hata kama Mwalimu angekuwa hai, angesema nchi imepiga hatua kielimu, kiafya na miundombinu licha ya vuguvugu la mtikisiko wa uchumi lililopo sasa.

Kuhusu hali ya kisiasa hivi sasa tofauti na wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, alisema uhuru wa kutoa maoni umepanuka tofauti na wakati wa enzi za chama kimoja ambapo sera zake zilikuwa zikitumikia umma tofauti na sasa ambapo kuna siasa za ubinafsi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Septemba 20, 2009

No comments:

Powered by Blogger.