MAGEREZA WAWAZUIA WANAHABARI KORTINI
Na Happiness Katabazi
ZAIDI ya askari wanane wa Jeshi la Magereza, jana waliwazuia waandishi wa habari wasiingie mahakamani kuripoti kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Simon Mkango na wenzake watatu.
Askari hao, walitumia mabavu na kauli za vitisho kuwazuia wanahabari hao wasiingie kusikiliza kesi hiyo, ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwenye chumba kidogo cha mahakama mbele ya Hakimu Samwel Maweda.
Baada ya washitakiwa wa kesi hiyo kuingia katika chumba hicho cha mahakama, askari hao, walianza kuwasukuma wanahabari hao kutoingia katika chumba hicho bila kutoa sababu zozote za msingi.
Licha ya wanahabari hao kuwaomba askari hao kuwaruhusu kuingia ndani, askari wengine walizidi kuingia ndani na wengine kusimama mlangoni kuwazuia.
Kutokana na hali hiyo, wanahabari walilazimika kuzunguka nyuma ya jengo la mahakama na kuisikiza kesi hiyo kupitia dirishani.
Pamoja na wanahabari hao kuamua kwenda kusikiliza kesi hiyo kwa kutumia dirisha, bado askari wengine walikwenda eneo hilo na kuwafukuza huku wakiwatolea lugha za vitisho.
“Sisi ni wanausalama, tunawaambieni tokeni hapo dirishini kwa hakimu kwani mnaweza kumdhuru na sisi tupo hapa kwa ajili ya kulinda usalama,” alisikika askari magereza mmoja aliyekuwa amevalia sare za jeshi hilo.
Kauli hiyo ilisababisha waandishi wa habari kushikwa na hasira na kuanza kuwaambia askari hao kwamba hawatatoka katika eneo hilo kwani nao wapo kazini na kuwataka wawafanye chochote wanachotaka.
Wakati majibishano kati ya wanahabari na askari hao yakiendelea, Hakimu Maweda alilazimika kusitisha kuanza kusoma uamuzi wa kesi hiyo na kuwataka askari wawaache wanahabari wafanye kazi yao.
Hata hivyo, askari hao walionekana kudharau kauli ya hakimu huyo kwani waliendelea kuwanyanyasa wanahabari hao.
Hii ni mara ya pili kwa askari wa jeshi hilo kuwabughudhi waandishi wa habari wakiwa kazini. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2005, eneo la Ukonga katika nyumba za askari hao, ambapo waandishi wa habari wawili walijeruhiwa kwa kipigo na askari hao wakati wakitimiza majukumu yao ya kikazi.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Septemba 19,2009

No comments:
Post a Comment