Header Ads

MBARONI KWA KUKUTWA NA NOTI BANDIA

Na Happiness Katabazi

WATU wawili akiwemo mwanamke jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na tuhuma za kukutwa na noti bandia za mataifa mbalimbali kinyume na taratibu.


Mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana,Wakili wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Maina John (40), raia wa Kenya na Nuru Swalehe (31) ambao ni wafanyabiashara.

Akiwasomea mashtaka hayo, alidai kuwa Oktoba 9, mwaka huu, saa 9.00 alasiri, eneo la Kinondoni, walikamatwa na ofisa wa polisi Lugano, wakiwa na noti bandia za mataifa mbalimbali.

Kishenyi alidai walikutwa na euro mia 11300; euro miatano 41000; euro hamsini 3900; dola mia 1,408; na pauni hamsini 252.

Washtakiwa hao walikana tuhuma hizo na upande wa mashtaka ulipinga dhamana kwa washtakiwa hao kwa maelezo kuwa John ni raia wa kigeni na kwamba alipokamatwa alikutwa na hati mbili za kusafiria, hivyo akiachiwa kwa dhamana anaweza kutoroka.

Pia, waliiomba mahakama hiyo, iwapo itatoa dhamana kwa washtakiwa itumie kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambapo kinataka mshtakiwa kutoa nusu ya fedha anayodaiwa kuiba, kama dhamana.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Frank Malongo, aliiomba mahakama hiyo kuwapatia wateja wake dhamana, na kupinga sababu za upande wa mashtaka. Kesi hiyo itatajwa Jumatatu, kwa uamuzi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 17, 2009

No comments:

Powered by Blogger.