Header Ads

MASHAHIDI 17 KUWABANA MRAMBA,YONA KORTINI

Na Happiness Katabazi

JUMLA ya mashahidi 17 wanatarajiwa kuieleza mahakama jinsi aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba na wenzake walivyoisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya sh bilioni 11.7.


Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, akisaidiana na Frederick Manyanda, Ben Lincoln, Tabu Mzee na Oswald Tibabyekomya, mbele ya jopo la mahakimu wakazi, John Utamwa, Saul Kinemela na Sam Rumanyika, jana alitaja orodha hiyo ya mashahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Wakili Boniface kabla ya kuanza kutaja majina ya mashahidi hao, alidai kuwa mashahidi wote watatumia anwani za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Aliwataja mashahidi hao kuwa ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Absalaam Khatib na aliyekuwa Kamishna wa Madini wa Wizara ya Nishati na Madini, Gray Mwakalukwa.

Wengine ni Maria Kyejo, Nakuela Senzia, Kesisia Mbatia, Bertha Soka, George Kaindoa, Nyero Hizza, Geogre Tigiti, Agrey Temba, P. J. Mlindoko, Neema Kitalu, Mustapha Ismail, Ludovick Kandege, Saddy Kambona, P. N. Kasela na Christine Shekidele.
Baada ya kutaja orodha ya mashahidi hao, Wakili Boniface, aliuomba upande wa utetezi katika kesi hiyo nao kutaja orodha ya mashahidi wake na vielelezo watakavyovitumia katika kesi hiyo, kwa kuwa waraka namba 2 wa Jaji Mkuu wa mwaka 1999, unaelekeza upande wa utetezi kufanya hivyo.

Hata hivyo, ombi hilo la upande wa mashitaka liliibua mjadala, ambapo wakili wa Mramba, Hurbet Nyange, alidai kuwa
Mteja wake hapaswi kutaja mashahidi wake wala vielelezo, hadi upande wa Jamhuri utakapomaliza kutoa ushahidi.

“Kama sijakosea, anaamini mahakama hii inaendesha kesi za jinai na kesi inayowakabili washitakiwa hao, na kwa mujibu wa kifungu cha 230 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, mshitakiwa hapaswi kutaja mashahidi wake, hadi upande wa mashitaka utakapofunga ushahidi na mahakama kumuona mshitakiwa kama ana kesi ya kujibu,” alidai Nyange.

Wakili huyo aliendelea kudai kwamba kifungu cha 231(1)(a) cha Sheria ya Kesi za Jinai, kinamtaka mshitakiwa atoe ushahidi na kuita mashahidi wake.

“Mimi na mteja wangu tunaheshimu Waraka namba 2 wa Jaji Mkuu wa mwaka 1999, lakini Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 ndiyo msingi wa kesi za jinai, kwa sababu sheria hiyo pia imetungwa na Bunge, hivyo ni mapema mno mteja wangu kutaja idadi ya mashahidi wake, wakati upande wa mashitaka haujaleta shahidi hata mmoja kuanza kutoa ushahidi,” alidai Nyange.

Hata hivyo, Hakimu Utamwa alilazimika kuingilia kati malumbano hayo na kuuhoji upande wa utetezi kama umesoma na kuuona waraka namba 2 wa Jaji Mkuu wa mwaka 1999, ili kujua unataka nini katika hatua za usikilizwaji wa awali wa kesi za jinai kama hiyo.

Mawakili wote wa upande wa utetezi walijibu kuwa hawajawahi kuuona, ndipo Hakimu Utamwa alipomtaka Wakili Mwandamizi wa Serikali, Frederick Manyanda, kuusoma kwa sauti waraka huo ili mawakili wa utetezi waweze kuusikia na kuelewa.

Kabla Manyanda hajaanza kuusoma waraka huo, wakili Nyange aliinuka na kudai kwa msisitizo kuwa hajauona waraka huo, lakini hata kama atauona na kuusoma, msimamo wake utabaki kuwa ule ule.

“Mheshimiwa Hakimu, sijauona waraka huo, lakini hata kama nikiuona na kuusoma, msimamo wangu na mteja wangu upo pale pale, kwamba Sheria ya Makosa ya Jinai ndiyo sheria kubwa katika kesi za jinai kuliko waraka huo wa Jaji Mkuu,” alisisitiza madai yake na kusababisha watu waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo kuangua vicheko.

Hata hivyo, baada ya Manyanda kumaliza kuusoma waraka huo, Hakimu Utamwa alisema haitoshi kuwasomea mawakili wa utetezi, bali wajipe muda wa kuusoma wao wenyewe, unaohusu Sheria ya Makosa ya Jinai, maamuzi mbalimbali ya kesi na Sheria ya Mahakimu (Magistrate Court Act), ili waelewe vizuri sheria hizo zinataka nini, na kuongeza kwa kumtaka Nyange asijibu hoja kwa kutumia waraka ambao hajawahi kuuona wala kuusoma.

Hakimu Utamwa, aliahirisha kesi hiyo hadi leo, ambapo itaendelea kusikilizwa katika hatua za awali, na upande wa utetezi utatakiwa kueleza walichokibaini katika sheria hizo, kisha watumie fursa hiyo kujibu ombi la upande wa mashitaka lililoutaka upande wa utetezi kutaja orodha ya mashahidi wake.

Mbali na Mramba, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, wanaotetewa na mawakili Cuthbert Tenga, Peter Swai na Joseph Thadayo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Septemba 23, 2009

No comments:

Powered by Blogger.