Header Ads

KORTI YATUPA PINGAMIZI LA VIGOGO BOT

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Wilaya Ilala, Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 104 inayomkabili Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Simon Mkango na wenzake watatu, lililokuwa likitaka washitakiwa hao wafutiwe mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuendesha kesi hiyo.


Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Samwel Maweda, alisema hoja hiyo iliyowasilishwa na wakili wa utetezi, Mpare Mpoki, imeshangaza na kusema kwamba hakubaliani nayo kwani ina nia ya kupotosha kwa makusudi kifungu cha 29 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, na kifungu cha 245(1,2,3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Alisema kifungu hicho cha sheria kinatamka wazi kwamba, mtuhumiwa wa kesi ya aina hiyo anapokamatwa anapaswa kupelekwa katika mahakama za chini kwa ajili ya hatua za awali.

“Kwa sababu hiyo ya kisheria, natupilia mbali hoja hiyo ya upande wa utetezi kwa sababu ina lengo la kupotosha kifungu hicho cha sheria kwani kesi hiyo imefunguliwa kihalali na washitakiwa walisomewa mashitaka yao na hawakupaswa kujibu chochote kwa sababu mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza,” alisema Hakimu Maweda.

Pia alisema anatupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi lililotaka mahakama hiyo iwaachilie huru washitakiwa kwa sababu hawakupaswa kushitakiwa kwa kuwa wana kinga ya kutokushitakiwa kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 65(1)(c) cha Sheria ya BoT.

“Nakubaliana na hoja ya upande wa mashitaka kwamba washitakiwa hao wakati wanatenda makosa hayo walikuwa na nia mbaya, na ikumbukwe sheria hiyo ya BoT inaweka kinga ya kutoshitakiwa kwa wafanyakazi wanaotenda makosa wakiwa na nia njema...hivyo natupilia mbali pingamizi hilo,” alisema.

Baada ya kutolewa uamuzi huo, Wakili Mpoki aliomba kupatiwa mwenendo wa kesi, ili akakate rufaa mahakama ya juu.

Hata hivyo, waandishi wa habari waliokuwa wamehudhuria kesi hiyo, walizuiliwa kuingia mahakamani na askari magereza, hali iliyowalazimu kusikiliza kesi hiyo kwa kuchungulia dirishani.

Mbali na Mkango, washitakiwa wengine ni Simon Jengo na Naibu Mkurugenzi Fedha za Nje, Kisima Mkango, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Bosco Kimela pamoja na Mkurugenzi wa masuala ya kibenki, Ally Bakari.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanadaiwa kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2004 na 2007, waliisababishia serikali hasara hiyo kwa kudanganya miongozo kwa kuongeza gharama za uchapishaji wa fedha za noti ikilinganishwa na gharama halisi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Septemba 19,2009

No comments:

Powered by Blogger.